Madrid kupindua meza dhidi ya Arsenal leo? Haya ni matokeo 5 yaliyowahi kushangaza Mabingwa Ulaya

Madrid kupindua meza dhidi ya Arsenal leo? Haya ni matokeo 5 yaliyowahi kushangaza Mabingwa Ulaya

Katika ulimwengu wa soka, kuna nyakati ambazo historia huandikwa kwa jasho, damu na imani. Arsenal waliipa Real Madrid kipigo kizito cha mabao 3-0 katika uwanja wa Emirates, kwenye mchezo wa kwanza wa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya. Baadhi wanaona kama matokeo hayo yamewaondoa tayari miamba wa Hispania, lakini historia ya michuano hii inaonyesha bado mechi mbichi na kwamba robo fainali haijamalizika hadi dakika 90 za mkondo wa pili zipite.

Real Madrid, klabu yenye historia ya mafanikio makubwa katika soka la Ulaya, wanakabiliwa na mlima mrefu wa kuupanda. Lakini kama kuna timu yenye rekodi ya kubadilisha matokeo kwa namna ya kushangaza, ni wao. Katika ardhi ya Santiago Bernabéu, ndoto zinaweza kutimia au kuporomoka.

Mechi ya marudiano kati ya Madrid na Arsenal si ya kawaida. Ni kipimo cha ujasiri, mbinu na moyo wa ushindani. Ili kuelewa uzito wa kinachowezekana kutokea, tunarudi nyuma na kuangalia mechi tano za kihistoria zilizoshuhudia kupinduka kwa matokeo, matokeo ya ajabu ambayo hakuna aliyetarajia.

1. Barcelona vs PSG – Raundi ya 16 Bora (2016/17)
.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Wachezaji wa Barcelona wakishangilia goli la Sergi Roberto pale Camp Nou lililowapa ushindi wa ajabu dhidi ya PSG, Machi 8, 2017

Katika moja ya matukio na matokeo ya kushangaza zaidi katika historia ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, ni mchezo wa FC Barcelona walipokumbana na Paris Saint-Germain katika hatua ya 16 bora msimu wa 2016/17. Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Parc des Princes, PSG waliitandika Barca mabao 4-0. Dunia iliamini kazi imeisha. Hakukuwa na matarajio yoyote ya Barcelona kupindua matokeo.

Hata hivyo, mchezo wa marudiano katika uwanja wa Camp Nou uligeuka kuwa hadithi ya kihistoria. Barcelona walipachika mabao 3 kupitia Luis Suárez, Layvin Kurzawa (bali la kujifunga) na Lionel Messi, kabla Edinson Cavani kuipatia PSG bao la ugenini lililoonekana kuzima matumaini. Lakini dakika za mwisho zilikuwa za miujiza Neymar alifunga mabao mawili (penalti na la mpira wa adhabu), na Sergi Roberto akafunga bao la sita dakika ya 95. Barcelona walishinda 6-1 na kusonga mbele hatua ya robo fainali kwa jumla ya mabao 6-5.

2. Liverpool vs Barcelona – Nusu fainali (2018/19)

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Miaka miwili baadaye, Barcelona walijikuta kwenye nafasi nyingine nzuri ya kutinga fainali ya michuano hii ya Klabu bingwa Ulaya. Katika nusu fainali ya kwanza dhidi ya Liverpool, walishinda 3-0 katika uwanja wao wa nyumbani Camp Nou, kwa mabao ya Lionel Messi (mawili) na Luis Suárez. Mashabiki walitazama mchezo wa mkondo wa pili wakiamini Barca walikuwa na nafasi nzuri na salama ya kusonga mbele.

Lakini mchezo wa marudiano katika uwanja wa Anfield uligeuka kuwa jukwaa la maajabu na miujiza mengine ya soka. Ikiwa bila ya wachezaji wake muhimu Mohamed Salah na Roberto Firmino Liverpool waliingia uwanjani kama timu inayokwenda kukamilisha ratiba. Lakini kupitia mabao mawili ya Divock Origi na mengine mawili kutoka kwa Georginio Wijnaldum, Liverpool walishinda 4-0. Utamu zaidi ulikuwa hasa bao la mwisho, lililotokana na kona ya haraka ya Trent Alexander-Arnold, ambapo mabeki wa Barcelona waliduwaa sekunde tu na kufungwa bao lililowapeleka Liverpool fainali.

Liverpool walienda mbali zaidi na kushinda mchezo wa fainali dhidi ya Tottenham Hotspur kwa mabao 2-0 na kutwaa taji la sita la Ligi ya Mabingwa Ulaya. Hii ilibaki kuwa moja ya matukio ya kupindua matokeo ama ‘comebacks’ kubwa zaidi katika historia ya michuano hiyo.

3. Deportivo La Coruña vs AC Milan – Robo Fainali (2003/04)

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Kipa wa AC Milan Nelson Dida akionekana kusononeka baada ya Deportivo kufunga bao lao la pili katika uwanja wa Estadio Municipal de Riazor, Aprili 7, 2004 huko La Coruna.

Katika msimu wa 2003/04, AC Milan, waliokuwa mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa, walikuwa na kikosi chenye nguvu kikiongozwa na Kaka, Shevchenko, na Pirlo. Katika mchezo wa kwanza wa robo fainali katika uwanja wa nyumbani San Siro, waliichapa Deportivo 4-1, na walionekana tayari wameshaingiza mguu mmoja nusu fainali.

Lakini mchezo wa marudiano Estadio Riazor uliandika historia. Deportivo walicheza kwa nguvu na nidhamu, wakiongozwa na Juan Carlos Valerón, Fran, na Pandiani. Walifunga mabao matatu kabla ya mapumziko, na kuongeza la nne kipindi cha pili na kupata ushindi wa mabao 4-0. Kwa jumla, waliibuka na ushindi wa 5-4 na kuwa timu ya kwanza katika historia ya Ligi ya Mabingwa kupindua matokeo ua kuwa nyuma kwa mabao matatu dhidi ya mabingwa watetezi.

Deportivo walienda hadi nusu fainali lakini walitolewa na FC Porto, ambao baadaye waliibuka mabingwa chini ya Jose Mourinho. Hata hivyo, kupindua matokeo dhidi ya Milan kulibaki kuwa tukio la nadra na la kusisimua.

4. AS Roma vs Barcelona -Robo Fainali (2017/18)

Barcelona waliingia katika mechi ya marudiano dhidi ya AS Roma wakiwa na uongozi wa mabao 4-1 walioupata katika mchezo wa kwanza uliopigwa nyumbani Camp Nou. Wakiwa na kikosi imara, walitarajiwa kumaliza kazi kwa urahisi katika uwanja wa Olimpico. Lakini mambo yalibadilika haraka. Meza ikapinduka.

Roma walitumia nguvu ya nyumbani pamoja na ufundi wa Eusebio Di Francesco kucheza kwa ari isiyo ya kawaida. Edin Džeko alianza kurejesha matumaini, kabla ya penalti ya Daniele De Rossi na goli la kichwa la Kostas Manolas kumaliza kazi. Roma wakashinda 3-0 na kusonga mbele kwa bao la ugenini.

Licha ya kuishangaza dunia, Roma walitolewa na Liverpool katika nusu fainali. Lakini hatua yao ilithibitisha kuwa hata klabu zisizotajwa sana zinaweza kubadilisha matokeo na kuweka historia.

5. AS Monaco vs Real Madrid – Robo Fainali (2003/04)

Real Madrid walikuwa na kikosi cha Galacticos, cha nyota wakali na wakuheshimiwa kama Zidane, Ronaldo Nazário, Figo, Beckham ambapo walishinda 4-2 nyumbani dhidi ya Monaco katika mechi ya kwanza. Ilionekana kuwa kazi rahisi katika marudiano. Hasa kutokana na ubora wao dhidi ya timu ya kawaida, Monaco.

Lakini Monaco, wakiongozwa na Didier Deschamps, walipigana uwanjani Stade Louis II. Mabao kutoka Ludovic Giuly (mawili) na Fernando Morientes (aliyekuwa kwa mkopo kutoka Real Madrid) yaliwapa ushindi wa 3-1. Matokeo ya jumla yakawa mabao 5-5, lakini Monaco ilisonga mbele kwa faida ya bao la ugenini.

Baada ya hapo, waliendeleza moto huo huo na kufika fainali, ingawa walifungwa na FC Porto. Ushindi dhidi ya Madrid ulionyesha kwamba hata miamba inaweza kuanguka dhidi ya timu zinazoonekana za kawaida.

Je, Real Madrid wanaweza kuweka historia ingine?

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Wakati dunia ya wapenda soka ikielekeza macho yake katika uwanja wa Santiago Bernabéu, swali linabaki, Je, Real Madrid wataongeza orodha ya historia ya matokeo ya ajabu ya kupindua meza kwenye Ligi ya Mabingwa?

Raphael Magoha mshabiki wa Arsenal, aliyepo Arusha anasema “nina matumaini na timu yangu, tutafungwa ila hatutatolewa”.

Mtazamo huu ni tofauti na mshabiki mwingine wa timu hiyo ya London, Lewis Kaisi: ” Wale jamaa wakiwa kwao ni habari nyingine, kukupiga 4 inawezekana”.

Kiungo wa Madrid, Jude Bellingham anaamini mchezo huu wa marudiano wa robo fainali dhidi ya Arsenal siku ya Jumatano wataandika historia.

“Nimesikia mara milioni tangu wiki iliyopita, nimeona video nyingi mno ni vitu vinavyotia hamasa sana,” alisema kiungo huyo wa kimataifa wa Uingereza katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne.

“Ni usiku ambao umetengenezwa kwa ajili ya Real Madrid.

Historia inawapendelea Madrid na inawapenda Arsenal

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Thierry Henry aliwanyanyasa Madrid na kufunga bao pekee lililowavusha Arsenal na kuingia robo fainali

Katika historia ya michuano ya Ulaya, Real Madrid wamewahi kupoteza mara tano kwa tofauti ya mabao matatu au zaidi katika mchezo wa kwanza wa hatua ya mtoano.

Lakini ni mara moja tu wakiwahi kupindua matokeo na kusonga mbele, ilikuwa mwaka 1975-76, miaka 50 iliyopita kwenye Kombe la Ulaya (European Cup), walipofungwa 4-1 na Derby County katika hatua ya 16 bora, kisha wakashinda 5-1 nyumbani katika mchezo wa mkondo wa pili na kufuzu kwa jumla ya mabao 6-5.

Katika historia ya michuano ya Ulaya, Madrid haijawahi kuifunga Araenal, na sio tu kuifunga, hata kupata bao la kufutia macbozi haijahi. Zimewahi kukutana mara mbili ukiacha mchezo wa juma lililopita Arsenal ikishinda 3-0, Arsenal ilimfunga Madrid nyumbani kwake Bernabeu, Hispania kwa bao 1-0 la Thierry Henry msimu wa 2005/2006 na kuwatoa kufuatia sare tasa ya 0-0 huko Highbury.

Hata hivyo katika miaka ya hivi karibuni, Real Madrid wameendelea kudhihirisha kuwa wao ni mabingwa wa kurejea mchezoni na kupindua meza katika Ligi ya Mabingwa.

Mwaka 2016, Cristiano Ronaldo alifunga hat-trick dhidi ya Wolfsburg na kugeuza kichapo cha 2-0 katika mchezo wa kwanza na kuibuka na ushindi wa 3-2 kwa jumla, baada ya kushinda 3-0 mchezo wa pili.

Mwaka 2022, walifanya maajabu mara mbili, wakianza kwa kuifunga PSG 3-1 na kusonga mbele baada ya kuwa nyuma kwa mabao mawili, kisha kuwashangaza Manchester City katika nusu fainali kwa mabao mawili ya Rodrygo dakika ya 90 kabla ya Benzema kukamilisha kazi kwa penalti. Katika fainali ya 2014, Sergio Ramos alisawazisha dakika za majeruhi dhidi ya Atlético Madrid kabla ya Madrid kushinda 4-1 katika muda wa nyongeza.

Wamefanya hivyo mwaka 2024, dhidi ya Bayern Munich. Ingawa Hawajawahi kufanya ‘comeback’ ya kiwango hiki (3-0) tangu kuitwa kwa michuano ya Ligi ya Mabingwa kutoka ile ya zamani, lakini Bellingham anaamini wanaweza kuinuka na kutimiza hilo nyumbani.

“Hakuna mengi unayoweza kufanya kwa Real Madrid katika Ligi ya Mabingwa ambayo hayajawahi kufanywa,” alisema kinda huyo mwenye umri wa miaka 21.

Historia na maoni mengi ya wachambuzi wa soka iko upande wao, lakini Arsenal wanaonekana kuwa tofauti msimu huu. Wanacheza kwa nidhamu, kasi, na kiu ya mafanikio.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *