Je, binadamu anaweza kujifungua mtoto kwenye anga za juu?

Je, binadamu anaweza kujifungua mtoto kwenye anga za juu?

Shirika la Anga za Juu la Marekani (NASA), limekuwa likidai kwa muda mrefu kwamba wanadamu wataweza kusafiri hadi katika sayari ya Mirihi (Mars) na kuishi huko katika miongo michache ijayo.

Wanasayansi wamekuwa wakijaribu kwa miaka mingi kutengeneza teknolojia ambayo itawawezesha wanadamu kusafiri mamilioni ya kilomita bila matatizo yoyote na kuishi huko.

Wanasayansi wamepata mafanikio makubwa katika hili. Ndio maana leo, wanaanga kama Sunita Williams waliweza kurudi salama duniani baada ya kukaa angani kwa miezi 9.

Ikiwa wanadamu wanataka kuanzisha makazi kwenye Mirihi, lazima waweze kuunda mazingira ya kuishi huko kama duniani. Tatizo likitokea, haitawezekana kurudi tu mara moja duniani kutoka Mihiri ili kulitatua. Dunia iko umbali wa kilomita milioni 22.5 kutoka Mirihi na inatuchukua angalau miezi 7 kufika.

Angani si mahali penye mazingira mazuri kwa wanadamu kuishi kama dunia ilivyo. Kwa mfano, kiasi cha mionzi katika anga za juu ni kikubwa zaidi kuliko duniani. Mionzi hii ina athari mbaya kwa manii na mayai, ambayo ni muhimu kwa uzazi.

Uharibifu wa DNA na misuli

Earth

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Dunia iko umbali wa kilomita milioni 22.5 kutoka Mirihi na inatuchukua angalau miezi 7 kufika.

Hivi karibuni NASA ilituma sampuli za mbegu za binadamu angani. Mbegu hizi zilizogandishwa zilipelekwa angani, na ikabainika kuwa DNA za mbegu hizo ziliharibika kutokana na mionzi ilioko.

Pia mienendo ya mbegu hizo iligundulika kubadilika. Hii ina maana kwamba uwezo wa manii kuchakata na kurutubisha yai baada ya kwenda angani ulipungua.

NASA ilifanya jaribio kama hilo kwa panya. Sampuli zilizogandishwa za manii ya panya pia zilitumwa angani. Sampuli hizi ziliwekwa angani kwa miezi kadhaa na zilipojaribiwa baada ya kurudishwa duniani, kuna matokeo chanya yalionekana.

Mbegu ya mnyama huyu, baada ya kuwa angani kwa miezi kadhaa, ilizaa watoto wenye afya na wenye nguvu. DNA ya mbegu hizi pia ilikuwa na uharibifu fulani. Lakini wakati mbegu hizi zilipounganishwa na yai kwa ajili ya uzazi, uharibifu huu wa DNA ulirekebishwa moja kwa moja.

Hata hivyo, ikiwa kijusi cha mwanadamu kitaweza kuzaliwa na afya angani, litakuwa jambo la lazima kumkinga kutokana na mionzi yenye madhara, kwa sababu baada ya kuathiriwa na mionzi hiyo, chembe za mwili wa kijusi zitaanza kukua bila mpangilio.

Hilo linaweza kusababisha mabadiliko ya kijeni na kuongeza hatari ya mtoto mchanga kupata matatizo makubwa kama vile saratani ya kuzaliwa.

Kando na mionzi hii hatari, kuna changamoto nyingine: Tunajua kwamba kukaa angani ambako hakuna graviti, misuli ya wanaanga hudhoofika. Pia, uzito wa mifupa yao huanza kupungua.

Mtiririko wa damu katika mwili pia hupungua. Yote hii kwa asili ina athari mbaya kwa mwili wa binadamu katika anga za juu.

Graviti na Upasuaji

kid

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Hata kama mwanadamu atafanikiwa kuzaa mtoto angani, mtoto aliyelelewa angani atakuwa tofauti na mtoto aliyezaliwa na kukulia duniani.

Graviti ina jukumu kubwa katika ukuaji wa mwili wa mtoto mchanga. Kwa mfano, muundo wa ndani wa sikio la mwanadamu huundwa kutokana na athari chanya ya graviti.

Sehemu hii ya mwili husaidia wanadamu kuwa una uwezo wa kukaa tuli na kuamua mwendo na mwelekeo wao. Wanasayansi waligundua kuwa baada ya panya ambao mimba zao zilitungwa angani, waliporudi duniani, hawakuwa na ufahamu wa wazi wa mwelekeo gani ni juu na mwelekeo gani ni chini. Na hivyo, hawakuwa na uwezo mzuri wa kutembea.

Ikiwa kuna matatizo yoyote wakati wa kujifungua, daima kuna chaguo la upasuaji. Lakini kufanya upasuaji kwenye mwili wa mwanadamu wakati kukiwa hakuna graviti itakuwa kazi kubwa. Damu itatoka nje ya mwili kutoka pande zote kutokana na ukosefu wa graviti.

Kutokana na matatizo hayo yote, bado haijawezekana kwa binadamu kufanyiwa upasuaji wa mwili kwenye anga za juu hadi sasa.

Kwa sasa, ikiwa mwanaanga aliye angani ataugua ghafla na anahitaji upasuaji, anarudishwa kutoka angani na kuletwa duniani, ambako anatibiwa.

Hata kama mwanadamu atafanikiwa kuzaa mtoto angani, mtoto aliyelelewa angani atakuwa tofauti na mtoto aliyezaliwa na kukulia duniani.

Kwa mfano, mtoto mchanga duniani hujifunza kwanza kutambaa kwa miguu yake. Mtoto mchanga angani hujifunza kwanza kuelea angani kwa mikono yake. Mifupa na misuli ya chini ya mtoto huyu itakuwa dhaifu na midogo, wakati mifupa na misuli ya sehemu ya juu ya mwili itakuwa na nguvu na mikubwa.

Katika anga za juu, mtu hatembei kutoka sehemu moja hadi nyingine, lakini huelea. Hii ina maana kwamba mikono hufanya kazi zaidi angani kuliko miguu. Uzito wa mwili wa watoto hawa utakuwa zaidi sehemu ya juu ya mwili (kama vile kifua na kichwa).

Kutokana na mrundikano wa umajimaji kupita kiasi kuzunguka uso, uso wao utaonekana kuwa na uvimbe zaidi kuliko ule wa watoto/watu w duniani, kama ilivyo kwa wanaanga wanaorejea kutoka angani.

Kwa hiyo, mtoto aliyezaliwa na kukulia angani hawezi kuishi atakapoletwa duniani. Itakuwa vigumu kutembea, kusimama, na hata kupumua duniani. Mwili wake haujakua ili kukabiliana na graviti kubwa ya duniani.

Matatizo ya kimaadili

k

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Changamoto za kimaumbile katika misheni hii ya kuzaliwa na kuishi angani, ni kubwa, na pia matatizo ya kimaadili ni magumu vile vile.

Mbali na athari hizo, pia kutakuwa na athari za kimaadili. Labda idhini ya wazazi wa mtoto inaweza kupatikana kwa ajili ya jaribio hili. Lakini vipi kuhusu matakwa ya mtoto mwenyewe?

Kumpeleka mtoto angani bila uwezo wa kuamua kama yuko tayari kushiriki au kutoshiriki katika jaribio hilo itakuwa ni makosa kimaadili. Utawezaje kupata ridhaa kutoka kwa mtoto ambaye hana maamuzi?

Kwa hivyo, changamoto za kimaumbile katika misheni hii ya kuzaliwa na kuishi angani, ni kubwa, na pia matatizo ya kimaadili ni magumu vile vile.

Kwenda angani kuzaliana na kulea mtoto huko inaonekana kama matamanio tu kwa sasa. Mwanadamu ameunda dhana nyingi kuhusu wazo hili kwa njia ya hadithi za kisayansi, riwaya, na filamu.

Lakini ikiwa mwanadamu anataka kuanzisha maisha nje ya dunia na kuacha alama huko, ni lazima ategue kitendawili cha maswali haya kwanza.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *