Mzozo wa DRC: Rwanda yalaani vikwazo vya Marekani dhidi ya maafisa wake

Serikali ya Rwanda imelaani vikwazo vilivyowekwa na Marekani dhidi ya Waziri wa Rwanda anayehusika na Muungano wa Kikanda Jenerali Mstaafu James Kabarebe, ikimtuhumu kuhusika katika vita kati ya kundi la M23 na serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Jenerali Kabarebe amewekewa vikwazo pamoja msemaji wa kundi hilo Lawrence Kanyuka.
Rwanda imekuwa ikishutumiwa kwa kuunga mkono kundi la M23, lakini inakanusha madai hayo.
Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alisema vikwazo hivyo havina msingi wowote na kusisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kuunga mkono juhudi za kisiasa za mataifa ya kikanda kutafuta suluhu badala ya hatua alizozitaja kuwa “za kukatisha tamaa.”
Aliongeza kuwa vikwazo haviwezi kuwa suluhisho la tatizo la muda mrefu mwashariki mwa DRC,na kama vikwazo vingetatua matatizo hayo ,eneo lingekuwa na amani miaka mingi iliyopita.

Marekani hapo jana ilitangaza vikwazo dhidi ya Jenerali Kabarebe, ambaye sasa ni Katibu wa Nchi katika Wizara ya Mambo ya Nje, akihusika na ushirikiano wa kikanda.
Vikwazo hivyo ni vya kiuchumi, na pia vimewekewa msemaji wa kundi la M23, Lawrence Kanyuka.
Vikwazo vya Marekani dhidi ya afisa mkuu wa Rwanda vimefuatia kura ya Bunge la Umoja wa Ulaya, ambalo lilitaka Rwanda iwekewe vikwazo.
Rwanda imepinga vikali hatua hiyo na kukata ushirikiano wa kimaendeleo na Ubelgiji, ambayo ilishutumiwa kwa kuchochea vikwazo hivyo.
Kabarebe ni nani?

CHANZO CHA PICHA, RWANDA GOV
Jenerali mstaafu James Kabarebe ni mwenye ushawishi mkubwa Rwanda – alipata umaarufu katika jeshi la Rwanda lilopigana vita kumsaidia rais wa zamani wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo marehemu Laurent Desire Kabila kuung’oa utawa wa marehemu Mobutu Sseseko.
Alipata sifa ya kuwa mtu wa kwanza katika historia kuongoza majeshi ya nchi mbili tofauti kwa wakati mmoja ,Rwanda na Jamuhuri ya kidemokrasia ya Congo alikojulikana kama jenerali James Kabare.
Marekani inamshutumu Kabarebe kwa kuwa mratibu kati ya Serikali ya Rwanda na kundi la M23.
Rwanda imekuwa ikionyesha kuwa haina uhusiano wowote na waasi wa M23, ikisema ni raia wa Congo walioazimia kupinga ubaguzi na mauaji dhidi yao.
Rwanda inasema kuwa jumuiya ya kimataifa inaendelea kupuuza dhulma ambayo watu hao wamekuwa wakitendewa kwa miaka mingi na utawala wa RDC, kikiwa ndio chanzo cha vita na migogoro ya muda mrefu.
Rwanda ikisisitiza kuwa wasiwasi wake mkuu ni usalama wake na kuzuia vitisho kutoka kwa DRC mnamo wakati ambapo nchi hiyo ilifanya muungano na Burundi, na kundi la FDLR na wote wakakubaliana kuwa nia yao ni kuiondoa serikali ya Rwanda.
Vikwazo vya Marekani dhidi ya afisa mkuu wa Rwanda vimefwatia kura ya Bunge la Umoja wa ulaya siku chache zilizopita kutaka Rwanda kuwekewa vikwazo, hatua ambayo Rwanda imepinga vikali na hata kukatiza ushirikiano wake wa kimaendeleo na Ubelgiji ikiishtumu kwa kuchochea vikwazo hivyo.
Serikali ya Marekani inasema kwamba vikwazo hivi vinamaanisha kwamba “mali na maslahi yote” ya watu hawa walioko Marekani, au wanaomilikiwa lakini wanadhibitiwa na watu nchini Marekani, yamezuiliwa, na mali zao lazima ziripotiwe kwa OFAC.
Hii si mara ya kwanza kwa Marekani au nchi za Ulaya na Umoja wa Ulaya kuwawekea vikwazo watu binafsi wanaoshutumiwa kuhusika na shughuli zinazozusha ukosefu wa usalama mashariki mwa DR Congo.