Jumuiya ya EAC, SADC katika mtihani wa kutatua mgogoro wa DRC

Jumuiya ya EAC, SADC katika mtihani wa kutatua mgogoro wa DRC

Kufuatia gharama kubwa wanayoilipa wakazi wa maeneo ya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, bila shaka macho, masikio na matumaini yao yote yamekuwa jijini Dar es Salaam kwa siku ya Ijumaa na Jumamosi.

Viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na ile ya Kusini mwa Afrika (SADC) watakuwepo nchini Tanzania katika mazungumzo ya kujaribu kuutatua mgogoro huo. Mawaziri wametangulia kukutana siku ya Ijumaa halafu Marais wanakutana Jumamosi.

Lakini swali kubwa ni; jumuiya hizi, zina meno ya kuutatua mgogoro huo?

Mtaalamu wa migogoro na usuluhisi na Balozi Dr Mohamed Omar Maundi anasema moja ya changamoto kubwa ya kuumaliza mgogoro wa Congo ni idadi ya wahusika wa mgogoro wenyewe

“Sasa hivi tunapozungumzia mgogoro wa Congo, hatuwazungumzii Wacongo wenyewe, tunawazungumzia na wadau wengine ambao mgogoro wa Congo umewahusisha. Nchi Jirani, maslahi ya watu wengine nje ya Afrika, kuna wadau wengi katika mazingira ya wadau wa Congo,” anasema Dr Maundi

Tshisekedi

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Mkutano unaofanyika mwisho wa wiki hii wa aina yake. Hii ni kwasababu unajumuisha jumuiya za kanda mbili tofauti kujaribu kutafuta suluhisho la mgogoro wa nchi moja

Imebidi mkutano huu ufanyike si tu kwasababu DRC ni mwanachama wa jumuiya zote hizi mbili, lakini pia inazungukwa na nchi nyingi za upande wa Mashariki na mbili za Kusini, hivyo mambo yakiharibika DRC, basi madhara yatasambaa kirahisi kwa nchi zote hizi za jirani

Kihistoria, Umoja wa Mataifa ndio umekuwa ukibeba jukumu la kutatua migogoro duniani kote.

Lakini tangu miaka ya 90′, Umoja wa Mataifa ulilemewa na jukumu hili, ukaanza kulipeleka zaidi kwa jumuiya za kikanda, hasa kwa nchi za Ulaya Asia na Afrika

Hata hivyo, jumuiya za barani Afrika zimekuwa na mafanikio kidogo kuliko zilivyotarajiwa.

Jumuiya ya Afrika Magharibi, ECOWAS, ilisifiwa baada ya kuzisimamishia uanachama nchi tatu – Mali, Niger na Burkina Faso – kufuatia mapinduzi ya kijeshi dhidi ya serikali zilizokuwepo madarakani

Lakini jumuiya za SADC na EAC, hazina rekodi ya kusisimua sana juu ya uwezo wao kutatua changamoto za kiusalama na kisiasa zinazotokea katika nchi wanachama wao

Msumbiji ilipoanza kukabiliwa na wanamgambo wa Al Shabaab, kwa mfano, SADC ilitarajiwa ingeisaidia Msumbuji, lakini ni Wanajeshi wa Rwanda ndio wameonekana kufanikiwa zaidi kuwakabili wapiganaji wa Al Shabaab

Hata huu mgogoro unaoendelea hivi hasa huko DRC, wengi wanaamini, kama Jumuiya EAC ingekuwa na uwezo na nyenzo za kutosha, ingeweza kusaidia kuutatua kabla ya kufikia katika hatua iliyofikiwa hivi sasa

Kwa ujumla, madhumuni ya uanzishwaji na muundo wa jumuiya hizi ni sababu kubwa ya kwanini jumuiya zingine zinafanikiwa zaidi kuliko zingine katika kudhibiti migogoro

Wasomi mbalimbali wanaona mantiki ya jumuiya hizi mbili kushughulikia mgogoro huu, lakini wanatahadharisha juu ya vigingi vingi vya kuvuka kabla mafanikio ya suluhisho hayajafikiwa

“Ingawa kuna uungwaji mkono mkubwa kwa juhudi za jumuiya za kikanda, tofauti kubwa za mbinu haziwezi kupuuzwa.

Nchi kadhaa za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zinachukulia mazungumzo kati ya Kinshasa na M23 kuwa njia pekee ya kupiga hatua katika kutatua tofauti zao, na zinajiepusha kusema hadharani kuhusu ushiriki wa Rwanda (katika mgogoro huo).

Kwa upande mwingine, Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) ilishutumu mashambulizi ya hivi karibuni ya M23 dhidi ya SAMIDRC, ilitaka Rwanda ijiondoe, na ilisisitiza tena uungwaji mkono kwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),” wanaandika wanazuoni Bram Verelst na Nicodemus Minde wa Institute for Security Studies

Kwa maneno mengine, wakati baadhi ya nchi wanachama wanasisitiza M23 ni Wakongo, na kwamba madai yao yashughulikiwe kisiasa, DRC na Burundi inakiangalia kikundi hiki kama waasi wanaotumika na Rwanda kuhatarisha amani ya Congo na hivyo namna pekee ya kushughulika nao ni kupitia nguvu ya kijeshi.

Utofauti wa itikadi miongoni mwa wanachama wa jumuiya hizi juu ya mzizi wa tatizo ambao ni utaifa wa waasi wa M23 ni kikwazo kikubwa na cha msingi katika kutatua mgogoro huu

Lakini kuna hali kubwa ya kutokuaminiani miongoni mwa viongozi mmoja mmoja na kati ya kiongozi mmoja dhidi ya jumuiya

Mwaka 2022 kikosi cha kulinda amani cha EAC kilipopelekwa DRC, wajibu wao mkubwa ulikuwa kusaidia kuwaondoa M23 katika maeneo ya Kivu Kaskazini.

M23

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Hata hivyo, Kinshasa ilitaka kikosi hiki cha EAC kupigane na kudhoofisha kabisa M23. Kikosi cha EAC kiliposhindwa kufanya hivyo, muda wake wa awali ulipoisha, DRC haikuongeza mkataba, na badala yake ikakikaribisha kikosi cha SADC

Lakini Kigali imekuwa ikikikosoa kikosi cha SADC kilichopo nchini DRC. Inasema uwepo wake hapo si tu kwamba haulengi kuleta amani, bali ni wa maslahi ya kiuchumi hasa kuinufaisha Afrika Kusini

“SAMIDRC si kikosi cha kulinda amani, na hakina nafasi yoyote katika mgogoro huu. Kiliidhinishwa na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) kama kikosi cha kijeshi, kufanya oparesheni za kijeshi ili kuisaidia DRC kupigana dhidi ya watu wake wenyewe,” amenukuliwa akisema Rais Paul Kagame

Kwa upande mwingine, Afrika ya kusini na Burundi imeilaumu Rwanda waziwazi kuchochea mgogoro huo kwa kuwasaidia waasi wa M23 na hata kuwa na wanajeshi wake nchini DRC, ili iendelee kunufaika kiuchumi. Shutuma hizi Rwanda inazikataa.

Lakini kuna changamoto ya rasilimali fedha ambayo inazikabili hizi jumuiya na kudhibiti uwezo wao wa kutekeleza majukumu yao kwa kiwango kinachotakiwa na kwa muda unaohitajika.

Katika mazingira ambayo kikundi cha M23 kinaendelea kuimarisha nafasi yao kisiasa miongoni mwa wananchi, hasa wa maeneo hayo ya Mashariki mwa Congo, nafasi ya jumuiya hizi kupata shuluhisho ambalo litaifurahisha nchi mwanachama wake anayehitaji msaada, yaani DRC, ni ndogo.

Matumaini ya wengi ni kwamba ikatokea hizi jumuiya zikafanikiwa hata kuzishawishi pande zote kusimamisha mapigano kwa muda fulani, kurudi mezani kwa ajili ya mazungumzo na kurudisha maeneo muhimu huku Kivu ya Kaskazini chini ya udhibiti wa serikali, basi hayo yatakuwa ni mafanikio makubwa sana.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *