Mgogoro wa DR Congo: Je, tulifikaje hapa?
Tarehe 24 January 2025 Rais Tshisekedi alikatiza ziara yake mjini Davos baada ya mapigano makali kuzuka nchini mwake.
katika mji wa Goma mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambapo waasi wa M23 na jeshi walidaiwa kufyatuliana risasi.
Wakati huo wote wakazi walisambaza video za wapiganaji wa M23 wakishika doria katika maeneo muhimu ya mji wa Goma.
Na wakati ambapo maelfu ya raia walionekana kutorokea miji jirani, waasi walitangaza kuudhibiti mji wa Goma madai ambayo yamepingwa na mamlaka ya DR Congo.
Serikali ya DRC imesema bado vikosi vyake vinadhibiti maeneo ya kimkakati ikiwemo uwanja wa ndege.
Zaidi ya raia 200 wameuawa katika maeneo yaliyotekwa na M23, viongozi wa eneo hilo walisema Alhamisi.
Chanzo cha usalama kililiambia shirika la habari la AFP kwamba gereza linalowashikilia wafungwa 3,000 “liliteketezwa kabisa” na kwamba kizuizi hicho kilisababisha vifo.
Rais wa Kenya William Ruto, mwenyekiti wa sasa wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, alilazimika kuitisha kikao cha dharura kilichotarajiwa kuhudhuriwa na marais wa DRC na Rwanda siku ya Jumatano ili kutuliza mgogoro huo.
Rais Ruto alisema ni wajibu kwa viongozi wa eneo hilo kusaidia kuwezesha suluhu la amani kwa mzozo huo.
DR Congo na Rwanda zalaumiana
Hatua hiyo ilijiri saa chache baada ya waziri wa mambo ya nje wa DR Congo kuishutumu nchi jirani ya Rwanda kwa madai ya kutangaza vita na kutuma wanajeshi wake mpakani kuunga mkono wapiganaji wa M23.
Rwanda haikatai kuunga mkono M23 lakini inashutumu mamlaka ya Congo kwa kuunga mkono wanamgambo wanaojaribu kuipindua serikali ya Kigali.
Rwanda inadai mamlaka ya Congo ilikuwa ikifanya kazi na baadhi ya wale waliohusika na mauaji ya halaiki ya Rwanda mwaka 1994, ambao walitorokea mpakani kuelekea DR Congo.
Kundi la M23 limechukua udhibiti wa maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yenye utajiri wa madini tangu 2021.
Kufuatia utekaji huo, ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umewashutumu waasi wa M23 kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyofikiwa na DRC na Rwanda mwezi Julai mwaka jana.
Mkuu wa ujumbe huo Bintou Keita alielezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa mashambulizi na kuelezea kukamatwa kwa mji wa mashariki wa Masisi kama hatua ya kutisha.
Awali waasi hao waliwaamuru wanajeshi kusalimisha silaha zao na kuweka muda wa mwisho wa saa 48 ambao ulikamilika mapema Jumatatu.
Walinda amani wa Umoja wa Mataifa walisema kuwa baadhi ya wanajeshi wa Congo walisalimisha silaha zao pamoja nao kabla ya muda uliowekwa.
Umoja wa Mataifa watoa wito wa kusitishwa kwa mapigano
Tarehe 24 mwezi Januari 2025, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionya kwamba mzozo wa sasa una hatari ya kuongezeka na kuwa vita vya kikanda.
Bw Guterres alitoa wito kwa “wahusika wote kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kukomesha aina zote za uungaji mkono kwa makundi yenye silaha,” ilisema taarifa.
Aliitaka Rwanda kuondoa majeshi yake katika ardhi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na M23 kusitisha harakati zake.
Haya yanajiri baada ya wanajeshi 13 waliokuwa wakihudumu na vikosi vya kulinda amani kuuawa katika makabiliano na waasi hao.
Wakati huohuo takriban mamluki 280 wa Romania waliokuwa wakipigana upande wa jeshi la DR Congo walijisalimisha kwa M23, Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF) lilisema kwenye X kabla ya kupandishwa ndege na kutakiwa kurudi makwao.
Hatua hiyo inajiri baada mpango wa DRC kuwatumia vitani kufeli
Tshisekedi asusia mazungumzo huku Kagame akiionya Afrika kusini
Siku ya Jumatano tarehe 29.01.2025, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Félix Tshisekedi alisusia mazungumzo ya kikanda yaliyolenga kukomesha mashambulizi ya waasi katika mji muhimu wa mashariki wa Goma.
Hatua hiyo inajiri baada Rais wa Kenya William Ruto kumwalika bwana Tshisekedi na mwenzake wa Rwanda Paul Kagame kwenye mkutano huo.
Na wakati vita vikali vikiendelea kati ya M23 na Jeshi la DRC FARDC Rais wa Rwanda Paul Kagame alitoa onyo kali kwa Rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa, akisema kwamba Rwanda imejiandaa kwa makabiliano iwapo kutakuwa na ulazima wa kufanya hivyo.
Taarifa hiyo ya Bw Kagame ilikuwa ikijibu maoni ya Bw Ramaphosa kuhusu jukumu la Kikosi cha Ulinzi cha Rwanda na Kikundi cha Waasi cha M23 katika mapigano yanayoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Jibu la Rais Paul Kagame kwa Cyril Ramaphosa liliashiria mzozo mbaya wa kidiplomasia kati ya Afrika Kusini na Rwanda.
Katika taarifa ya Kagame iliyosheheni cheche kali za na maneno kwenye mtandao wa kijamii wa X, Kiongozi huyo alimshtumu Rais wa Afrika Kusini kwa kupotosha mazungumzo ya faragha juu ya hali tete mashariki mwa DRC.
Kagame alisema Bwana Ramaphosa alikuwa hajaonya Rwanda juu ya shughuli zake za kijeshi DRC lakini badala yake alikuwa ameomba msaada wa vifaa, pamoja na umeme, chakula, na maji kwa wanajeshi wa Afrika Kusini.
Wakati akikaribisha juhudi za Afrika Kusini za amani, Bwana Kagame alisisitiza kwamba nchi hiyo haikuwa katika nafasi ya kuwa mtafutaji amani wala mpatanishi na alionya zaidi kwamba ikiwa Afrika Kusini inataka makabiliano, Rwanda ingejibu ipasavyo.
Kwa upande wake Rais wa DR Kongo Félix Tshisekedi aliapa kurejesha mamlaka ya serikali mashariki mwa nchi, ambako waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda wameuteka mji wa Goma na wanaripotiwa kuelekea kusini kuchukua maeneo zaidi.
Katika hotuba yake kwa taifa kwa njia ya televisheni, alisema “majibu makali yaliyoratibiwa” dhidi ya kile alichokiita “magaidi” yatafanyika.
Tshisekedi aliikosoa jamii ya kimataifa kwa “kutochukua hatua” na kwa kutofanya juhudi za kutosha kufuatia mzozo huo unaozidi kuongezeka.
Wakati wa hotuba yake siku ya Jumatano usiku, Tshisekedi aliwahimiza Wacongo wote kuungana pamoja na kuunga mkono mapambano ya jeshi kukomboa mji wa Goma.
Mamia waachwa bila makao
Vilevile Mamia ya wakimbizi waliokimbia mji wa Goma wakitoroka mapigano mapema wiki hii sasa wanarejea nyumbani, kulingana na mwandishi wa BBC Idhaa ya Kinyarwanda, Jean Claude Mwambutsa.
Wengi wa wakimbizi hao ni wale waliowekwa katika kambi ya muda ya Rugerero iliyoko viungani mwa mji wa Rubavu kaskazini-magharibi mwa Rwanda.
Mamlaka inasema zaidi ya 600 wamerejea nyumbani kufikia Jumatano.
Mamlaka ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia wakimbizi linasema kuwa zaidi ya watu 500,000 wameyakimbia makazi yao mwezi huu wa Januari 2025 kutokana na mapigano mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
SADC yafanya kikao kuhusu DR Congo
Viongozi wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) wamefanya mkutano mjini Harare Zimbabwe kujadili vita vinavyoendelea huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Mkutano huo unafanyika wakati misheni ya kijeshi ya kikanda yenye kushirikiana na vikosi vya ulinzi vya Congo ilipata majeruhi wakati vikosi vya waasi vilichukua sehemu ya mji wa mashariki wa Goma.
Mkutano usio wa kawaida wa wakuu wa nchi na serikali unatarajiwa kujadili hatua za kumaliza mvutano katika eneo la mashariki mwa Congo na pia mustakabali wa operesheni ya kijeshi za SADC katika eneo hilo.
Mwenyeji wa mkutano huo Zimbabwe ilionyesha wasiwasi kwamba mzozo unaoendelea DRC unaweza kuwa na athari kwa nchi wanachama.
Wanajeshi kadhaa kutoka Afrika Kusini, Malawi na Tanzania wameuawa wakati wa makabiliano na waasi wa M23.
Upande mwingine, UN imeshutumu Rwanda kwa kuwasaidia waasi wa mashariki mwa DRC madai ambayo Rwanda iliyakanusha hapo awali.
DR Congo yataka Rwanda iwekewe vikwazo
Wakati huohuo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo imetoa wito kwa Rwanda iwekewe vikwazo na kupunguzwa kwa misaada na pia isimamishwe ushiriki wake katika misheni ya kulinda amani ya UN kwa jukumu ambalo inadaiwa kutekeleza katika mzozo wa Congo Mashariki.
Waziri wa mambo ya nje wa Congo aliiambia BBC, Rwanda inakalia eneo la nchi yake kinyume cha sheria.
Therese Kayikwamba Wagner alisema Rwanda inaunga mkono, kufadhili na kuandaa ujasusi ambao unalenga kupindua serikali iliyochaguliwa kisheria.
Ikijibu madai hayo, msemaji wa serikali ya Rwanda alisema nchi yake inatetea mipaka yake wala haina nia ya mabadiliko ya serikali.