Rais Tshisekedi akatiza ziara yake Davos huku mapigano yakipamba moto DR Congo

Rais Tshisekedi akatiza ziara yake Davos huku mapigano yakipamba moto DR Congo

Katika wiki chache zilizopita, M23 imeteka miji ya Masisi na Minova huko Kivu Kaskazini.

Zaidi ya raia 200 wameuawa katika maeneo yaliyotekwa na M23, viongozi wa eneo hilo walisema Alhamisi.

Na kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, watoto wawili walifariki baada ya mabomu kuanguka kwenye kambi ya watu waliokimbia makazi yao.

Kuanguka kwa Goma, jiji la zaidi ya milioni ambalo liko karibu na mpaka na Rwanda , itakuwa mapinduzi makubwa kwa waasi.

Walichukua jiji hilo kwa muda mfupi wakati wa uasi mwaka 2012, lakini walijiondoa baada ya makubaliano na kusuluhishwa.

Barabara nyingi zinazoelekea mjini kwa sasa zimefungwa, na hivyo kuzua wasiwasi kwamba chakula kinaweza kuisha.

“Mji wa Goma unazuiliwa katika hali mbaya, mji umedhibitiwa, hakuna viingilio tena, hakuna njia za kutoka … idadi hii inateseka sana” kiongozi wa muungano wa eneo hilo Bahala Shamavu Innocent aliiambia BBC.

Espoir Ngalukiye, mwanachama wa chama cha upinzani cha Ensemble pour la Republique, pia ana wasiwasi kuhusu upatikanaji wa chakula.

“Huku Goma hatuko salama kwa kweli,” Bw Ngalukiye alisema. “Hakuna mtu anayeishi Goma anayeweza kukuambia kwamba hana woga.”

Siku ya Alhamisi waasi hao waliuteka mji wa karibu wa Sake, kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, Uingereza na vyanzo vingine mbalimbali.

Lakini jeshi la Congo lilisema kuwa limezuia shambulio la Sake, ambalo liko kilomita 20 tu kutoka Goma.

Wakazi wa Sake na eneo pana, ambao wengi wao walikuwa tayari wamehama kutokana na mzozo – wamekimbia makazi yao.

Watu wanatoroka wakiwa wamebeba magodoro na vitu vingine muhimu migongoni mwao, huku kadhaa wakirundikana kwenye boti za mbao zilizojaa kupita kiasi.

Maelfu ya familia zilizojawa na hofu zimekimbia kuelekea Goma, ambako hospitali zimezidiwa na raia waliojeruhiwa.

Kundi la M23 limechukua udhibiti wa maeneo mengi ya mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo yenye utajiri wa madini tangu 2021. Kutokana na hali hiyo, mamia ya maelfu ya watu wameyakimbia makazi yao.

Mwaka jana, ilihofiwa pia waasi wangeiteka Goma. Kulikuwa na utulivu mwishoni mwa Julai, lakini mapigano makali yalianza tena mwezi Oktoba, na kuwa mbaya zaidi kuelekea mwisho wa mwaka.

DR Congo na Umoja wa Mataifa wanasema M23 inaungwa mkono na Rwanda. Mamlaka ya Rwanda haithibitishi wala kukanusha hili.

Siku ya Ijumaa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres alionya kwamba mzozo wa sasa una hatari ya kuongezeka na kuwa vita vya kikanda.

Bw Guterres alitoa wito kwa “wahusika wote kuheshimu mamlaka na ukamilifu wa eneo la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kukomesha aina zote za uungaji mkono kwa makundi yenye silaha,” ilisema taarifa.

Raia wakikimbia mapigano

CHANZO CHA PICHA, AFP

Zaidi ya watu 400,000 wameyakimbia makazi yao tangu mwanzoni mwa mwaka huu wakati M23 ikipiga hatua kuelekea mji mkuu wa mkoa wa Goma, Umoja wa Mataifa unasema.

Rais Felix Tshisekedi alirejea kutoka Uswizi kwa mikutano ya dharura ya usalama na maafisa wakuu.

Bw. Tshisekedi anatarajiwa kutangaza hatua za kulinda mji wa Goma na kushughulikia mzozo wa kibinadamu unaozidi kuwa mbaya.

Mapigano mapya yaliyozuka Sake, takribani kilomita 23 kutoka Goma, yamesababisha watu wengi kuhama makwao na kuzua hofu ya hali mbaya zaidi ya kibinadamu.

M23 ni nani? Wanataka nini?

Ukizungumzia M23, inawakumbusha wengi kuwahusu watu kama Sultani Makenga na wengine kama Bosco Ntaganda, huku wengine wakirudi nyuma na kumkumbuka Laurent Nkunda.

Tangu mwaka 2004, Jenerali Nkunda amejiondoa katika jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pamoja na wanajeshi wake katika vilima vya Rutshuru na kuunda CNDP, ambayo imekuwa ikifanya mashambulizi dhidi ya vikosi vya serikali na mji wa Goma.

Sababu za vita vyake ni kulinda watu wa kabila lake na aliendeleza mapambano dhidi ya makundi mengine ya waasi ambayo pia yanatokana mapigano ya kikabila na ni miongoni mwa sababu zilizotolewa na Nkunda na wapiganaji wake wakiwemo Makenga na Ntaganda.

Wote watatu walikuwa wanachama wa waasi wa zamani wa APR waliochukua mamlaka nchini Rwanda mwaka 1994, kabla ya kuendeleza vita vyao nchini DR Congo mwishoni mwa miaka ya 1990.

Nkunda alikamatwa nchini Rwanda mapema mwaka 2009 na kufungwa, huku CNDP ikiongozwa na Ntaganda ikijadiliana na serikali ya Kabila katika makubaliano ya Machi 23, 2009.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *