Athari za Trump kuiondoa Marekani katika shirika la Afya Duniani WHO
Rais wa Marekani Donald Trump ametia saini amri ya kuanza mchakato wa kuiondoa Marekani kuwa mwanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO).
“Hili ni jambo kubwa,” rais mpya wa Marekani aliyeapishwa alisema alipokuwa akiidhinisha hati hiyo baada ya kurejea tena katika Ikulu ya Marekani.
Ilikuwa ni moja ya amri kadhaa za utendaji alizotia saini siku ya kwanza madarakani.
Hatahivyo uamuzi wake huenda sio tu ukaathiri utandekazi wa shirika hilo la Afya bali hata huduma zake kote duniani.
Je, ni kwanini Trump ameamua kuchukua uamuzi huu?
Hii ni mara ya pili kwa Trump kuamuru Marekani kujiondoa kuwa mwanachama wa WHO.
Trump alikosoa jinsi shirika hilo la kimataifa lilivyoshughulikia janga la Covid-19 na kuanza mchakato wa kujiondoa kutoka kwa taasisi hiyo ya Geneva wakati wa janga hilo.
Rais Joe Biden baadaye alibatilisha uamuzi huo.
Agizo hilo lilisema Merekani inajiondoa “kwa sababu ya WHO kutoshughulikia janga la Covid-19 ambalo liliibuka Wuhan, China, na majanga mengine ya afya ya ulimwengu, kushindwa kwake kupitisha mageuzi yanayohitajika haraka, na kutokuwa na uwezo wa kuonyesha uhuru kutoka kwa yasiyofaa. ushawishi wa kisiasa wa nchi wanachama wa WHO”.
Amri hiyo ya utendaji pia ilisema hatua hiyo ilitokana na “malipo yasiyofaa” ambayo Marekani ilitoa kwa WHO, ambayo ni sehemu ya Umoja wa Mataifa.
Trump alipokuwa ofisini kwa mara ya kwanza alikosoa shirika hilo kwa “kuipendelea China” katika kukabiliana na janga la Covid-19.
Aliishutumu WHO kwa kuegemea China kwa jinsi ilivyotoa mwongozo wakati wa mlipuko huo.
Mwaka 2020 wakati wa janga la Covid Tramp alisema: “Ikiwa WHO ingekuwa imefanya kazi yake ya kutuma wataalamu wa kitabibu nchini China ili kutathmini hali ilivyo, na kuikosoa China kwa kutokuwa wazi, ugonjwa huo ungeweza kudhibitiwa na kutokea kwa idadi ndogo ya vifo.”
WHO imekuwa ikifadhiliwa vipi?
Shirika hilo liliundwa 1948 kama sehemu ya mfumo wa Umoja wa Mataifa, likilenga kuendeleza afya bora, kuhakikisha dunia inakuwa salama na kuhudumia wale walio katika hatari zaidi.”
Taasisi hiyo, ambayo makao yake makuu ni Geneva (Uswizi), imekuwa ikipata Ufadhili wa lazima na ule wa kujitolea
Kwanza, kuna pesa ambazo ni lazima zitolewe na nchi washirika 194.
Kila nchi inatakiwa kulipa kiwango fulani kulingana na Umoja wa Mataifa kupitia mfumo ambao ni vigumu kuelezeka kwasababu unazingatia utajiri wa nchi na idadi ya watu.
Ni pesa ambayo kwa msingi huwa inasimamia mishahara na utawala wa shirika hilo.
Pili ni ufadhili wa kujitolea unaowezesha nchi na maeneo kuahidi pesa watakazochangia kwa maswala maalum, kama vile chanjo ya ugonjwa wa polio, afya ya wanawake au ukabilianaji na matumizi ya tumbaku.
Marekani ilichangia dola za Marekani bilioni 1.284 katika kipindi cha 2022-2023, kuwezesha WHO, Marekani na nchi nyingine na washirika kutambua na kukabiliana na dharura, kuzuia vitisho vya magonjwa kuenea katika mipaka na kuendeleza vipaumbele vingine muhimu vya afya duniani.
WHO ilipokea dola za Marekani milioni 363 kama fedha za ufadhili kipindi cha 2022-2023 kulingana na taarifa katika wavuti wa shirika hilo.
Hatahivyo idadi ya wafadhili imendeelea kuongezeka huku mataifa kama vile , Ujerumani, Tume ya Ulaya, Norway, Jamhuri ya Korea zikijiunga na Marekani , Luxembourg, India na Uhispania katika kulifadhili shirika hilo.
Baada ya Marekani, ni shirika la kibinafsi la Bill and Melinda Gates Foundation, ambalo hutoa ufadhili mkubwa kupitia hazina ya the Global Fund
Mchangiaji mkubwa wa tatu ni GAVI, shirika ambalo linajumuisha mashirika ya umma na serikali ambayo yanapigia upato kuongeza upatikanaji wa chanjo kwa nchi 73 katika maeneo ya kaskazini kote duniani.
Athari ya kuondolewa kwa ufadhili wa Marekani
Ikiwa Marekani itafanikiwa kuondoa mchango wake , WHO itakuwa na changamoto.
“Uamuzi wa Trump kusitisha ufadhili kwa WHO utakuwa na athari kubwa”, Jack Chow, aliyekuwa balozi wa Marekani katika kukabiliana na ukimwi na aliyekuwa Naibu Mkurugenzi wa WHO alisema mwaka 2020 wakati Marekani ilipojaribu kuchukua hatua kama hiyo.
“Hili linasababisha matatizo kwasababu ni wafadhili ndio wanaoandaa ajenda zitakazofuatwa na shirika hilo badala ya kufanya maamuzi yao kwa kuzingatia taaluma,” Chow amesema katika mahojiano na BBC Mundo.
Maeneo yanayopokea ufadhili mkubwa wa WHO
Kulingana na takwimu za hivi karibuni zilizochapishwa na WHO, raslimali iliyotolewa na Marekani kwa miaka miwili 2018-2019 kiwango kikubwa cha ufadhili wake umeelekezwa mashariki ya eneo la Mediterranean, kwa nchi 22 kutoka Morocco hadi Pakistan.
Eneo hilo limepokea karibia dola milioni 201 za Marekani, sawa na asilimia 36 ya pesa zilizotolewa na Washington.
Eneo la pili lenye kupokea kiwango cha juu cha pesa hizo ni Afrika, ambayo inajumuisha nchi 47 kwa bara hilo huku ufadhili kutoka Marekani ukiwa ni jumla ya dola milioni 151 za Marekani.
Eneo la tatu linalopokea ufadhili wa Marekani ni makao makuu ya WHO, ambayo yanapokea karibia dola milioni 101 za Marekani, kiasi hicho kikitumiwa kwa uendeshaji wa shughuli zake na kampeni kadhaa za masuala ya afya.
Ni asilimia kidogo tu ya ufadhili wa Marekani karibia dola 280,000 sawa na takriban asilimia 0.5, ambazo zimetumika kufadhili shughuli za WHO kwa nchi za Amerika ya Kusini na zile za Caribbean.
Upande wa kampeni za afya, zaidi ya robo ya ufadhili wa Marekani zimetengwa kukabiliana na polio duniani (dola milioni 158 sawa na asilimia 27 ya pesa ilizotoa kwa ujumla).
Pesa nyingine dola milioni 100 zimetumika katika miradi ya kuwezesha watu kupata afya bora na ulaji sahihi, huku dola milioni 44 za Marekani zikitumika katika miradi ya utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa yanayoweza kuzuilika.
Na dola milioni 33 zinazohitajika kukabiliana na kifua kikuu zikiwa zimeen delea kutumika.
Lakini hiyo ni baadhi tu ya miradi kwasababu pia kuna fedha zilizotengwa kukabiliana na Ukimwi na hepatitis hadi uzuiaji na udhibiti wa kutokea kwa majanga pamoja na pesa za kukabiliana na magonjwa ya kitropiki hadi afya ya uzazi, upatikanaji wa dawa na miradi mingine mingi.