Afrika inafaidishwa vipi na marufuku ya TikTok Marekani?
TikTok inatarajiwa kupigwa marufuku Marekani Januari 19 baada ya mahakama ya juu zaidi nchini humo kupinga ombi lililowasilishwa na mmiliki wa mtandao huo ByteDance, kutaka marufuku hiyo ibatilishwe.
Mahakama hiyo imeamua kuwa sheria inayopiga marufuku mtandao huo wa kijamii haikiuki haki msingi za mtandao huo na watumiaji wake kama inavyodai Tiktok.
Rais mteule Donald Trump anayetarajiwa kuapishwa rasmi Januari 20 anasema, mustakabali wa Tiktok atauamua yeye.
TikTok inapokewaje Afrika?
TikTok imekabiliwa na upinzani kutoka kwa baadhi ya serikali duniani ikiwemo nchi kadhaa za Afrika.
Senegal na Somalia zimepiga marufuku mtandao huo wa kijamii huku kukiwepo maombi ya hatua kama hiyo kuidhinishwa katika nchi nyingine kama Kenya.
Sababu kubwa inayotolewa na walalamikaji binafsi na hata baadhi ya serikali za Afrika, ni hatari kwa usalama wa taifa pamoja na kudorora kwa maadili katika jamii wakitaka hatua ichukuliwe dhidi ya TikTok.
Mtandao huo umeshutumiwa kutumika kusambaza propaganda, kutumika kama chombo cha kuendeleza ulaghai lakini pia kusambaza maudhui yasiyo na staha.
Kenya ni miongoni mwa nchi zenye matumizi makubwa ya TikTok duniani ikiwa na 54% ya matumizi jumla na 29% ya watu wakiutumia mtandao huo kupata taarifa za habari.
Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya kidijitali ya 2023 ya taasisi ya Reuters. Misri ina watumiaji milioni 33 na Nigeria wateja milioni 28.
Mnamo Agosti, bunge nchini Kenya liliafiki kutopiga marufuku TikTok kufuatia ombi la mlalamikaji, raia nchini humo aliyetaka mtandao huo upigwe marufuku.
Badala yake serikali ilikubali kuzingatia udhibiti wa maudhui. Katika kikao kati ya rais William Ruto, mkurugenzi mkuu mtendaji wa TikTok Shou Zi Chew alikubali kufungua ofisi nchini Kenya kuwajibika kusimamia ipasavyo maudhui yanayochapishwa.
Marufuku ya TikTok Marekani itaifaidisha vipi Afrika?
Licha ya wasiwasi unaoongezeka kuhusu usalama wa mataifa, Tiktok bado inaendelea kupata umaarufu miongoni mwa vijana wa Afrika.
Mitandao ya kijamii kama TikTok hutumika sio tu kwa burudani lakini pia kupata taarifa na hata kama njia ya kujiinua kiuchumi.
Fikra nyingi, ubunifu na hata ujuzi mwingi vimetokana na TikTok.
Moses Kemibaro, muasisi na katibu mkuu mtendaji wa Dotsavvy Africa ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya teknolojia anasema, marufuku ya Tiktok Marekani itaondosha fursa ya kuona na kutumia maudhui yenye manufaa kwa watumiaji kutoka Marekani.
“Muhimu zaidi ni kwamba idadi kubwa ya watumiaji wenye fikra nzuri za kiabisahara itapotea.”
Kemibaro anaeleza kuwa kibiashara au kiuchumi huenda marufuku ya Marekani ni fursa kwa masoko mengine duniani ikiwemo Afrika, ambapo waendesha maudhui au ma influensa wamekuwa na changamoto katika kufaidi ipasavyo kifedha kutokana na maudhui yao.
“Huenda TikTok sasa ikalazimika kuelekeza mapato haya katika masoko mengine ambako kuna wateja, ili kuziba pengo litakaloachwa” anaeleza Kemibaro akiashiria nchi kama Marekani na India zilizopiga marufuku Tiktok.
Mtaalamu na mtafiti wa masuala ya digitali na usalama mitandaoni Yusuf Kileo, anakubaliana na hilo.
“Kwenye ajenda ya sasa inayokuzwa na nchi za Afrika maarufu ‘Digital Economy’ unakuta vijana wengi wamejiajiri kupitia TikTok kwa kurekodi na kuuza maudhui ya video. Kwahivyo TikTok ikifungwa Marekani na uwekezaji huo mkubwa ukaja Afrika, maana yake faida hiyo kubwa itakuwa imesogea karibu na manufaa mengi huenda yakatokea kifedha kutokana na maudhui hayo kwenye TikTok.
Hatahivyo anatahadharisha kuwa kwa kuona nchi kubwa kama Marekani imeamua kuifungia TikTok baada ya kuonekana kuwa hatua hiyo haijaathiri uhuru wa kujieleza – nchi za Afrika zinaweza kujitathmini na pengine kufuata mkondo huo. Na sio kwa TikTok tu lakini pia kuishia kufungwa kwa majukwaa mengine kwa kigezo hicho cha kutishiwa usalama wa taifa.
Hili Kileo anasema huenda likiashia kutishia uhuru wa kujieleza.