Marekani yamuwekea vikwazo mkuu wa jeshi la Sudan Burhan
Serikali ya Marekani imemuwekea vikwazo mkuu wa jeshi la Sudan na rais mteule Jenerali Abdel Fattah al-Burhan, wizara ya fedha ilisema.
Amekuwa akiongoza moja ya pande mbili katika vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miezi 21 ambavyo vimeua makumi ya maelfu huku zaidi ya milioni 12 wakilazimika kuhama makazi yao na kusukuma nchi hiyo kwenye janga la njaa.
Katika taarifa fupi, Marekani ilimshutumu Jenerali Burhan kwa “kuvuruga Sudan na kudhoofisha madhumuni ya kipindi cha mpito chenye kidemokrasia”.
Tangazo hilo linafuatia ripoti za mauaji ya raia katika mji wa kati wa Wad Madani katika siku za hivi karibuni, hata hivyo, hilo halikutajwa kwenye taarifa hiyo.
Wiki iliyopita, Mohamed Hamdan Dagalo, mkuu wa kundi la Rapid Support Forces (RSF) wanaopigana na jeshi, pia aliwekewa vikwazo na Marekani.
Marekani ilishutumu Kikosi cha Rapid Support Forces (RSF) kwa kufanya mauaji ya halaiki wakati wa mzozo huo.
Katika kutangaza vikwazo dhidi ya Burhan siku ya Alhamisi, Washington ilisema kuwa jeshi chini ya amri yake “limefanya mashambulizi mabaya kwa raia” ikiwa ni pamoja na kulenga “shule, masoko na hospitali”.