Zijue nchi za Afrika zisizoruhusu uraia pacha, zipo za Afrika Mashariki
Uraia wa nchi mbili ni kinyume cha sheria katika nchi kadhaa za Kiafrika. Lakini uraia huo hutoa manufaa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na usafiri bila viza, fursa bora za maisha, na ulinzi.
Kwa ufupi, uraia wa nchi mbili unamaanisha kuwa raia wa nchi mbili kwa wakati mmoja. Kimsingi, kila nchi zina sheria tofauti kuhusu uraia wa nchi mbili.
Zifuatazo ni nchi za Afrika ambazo bado hazijaruhusu kabisa au hazijaruhusu kwa ukamilifu uraia wa nchi mbili, kwa lugha nyingine ili ni ima ubaki kuwa raia wa nchi hiyo au ukane uraia na uende kwenye uraia wa nchi yako nyingine utakayo.
Cameroon
Cameroon, rasmi inajuulikana kama Jamhuri ya Cameroon, ni nchi iliyoko Afrika ya Kati yenye wakaazi takribani milioni 28.65. Imepakana na Nigeria upande wa magharibi na kaskazini, Chad upande wa kaskazini mashariki, Jamhuri ya Afrika ya Kati upande wa mashariki, na Guinea ya Ikweta, Gabon na Jamhuri ya Congo upande wa kusini.
Hakuna kifungu cha kisheria nchini Cameroon ambacho kinaruhusu uraia wa nchi mbili. Uraia wa Cameroon unaweza kupotea ikiwa mtu atapata uraia wa nchi nyingine au kukataa uraia wake wa Cameroon.
Lakini kwa mtoto aliyezaliwa nje ya nchi kutoka kwa wazazi wa Cameroon, anaweza kuwa na uraia pacha, ingawa baada ya kufikia umri wa miaka 21, lazima achague uraia mmoja kati ya Cameroon na hiyo nchi nyingine.
DR Congo
DRC yenye utajiri mkubwa wa maadini kobalti na shaba, dhahabu, ina msitu wa pili kwa ukubwa duniani, msitu wa Congo baada ya Amazon wa Amerika Kusini, na ni nyumbani kwa mbuga kadhaa za Wanyama.
Ingawa DRC haitambui uraia pacha, lakini watoto wanaozaliwa nje ya nchi wanaruhusiwa kuwa na uraia pacha, hadi wafike umri wa miaka 21. Kisha hulazimika kuchagua.
Equatorial Guinea
Equatorial Guinea ni mzalishaji na muuzaji nje wa mafuta ghafi na gesi asilia. Mafuta ya petroli ndiyo yanaunda sehemu kubwa ya mauzo ya nje ya nchi. Pia ina rasilimali nyingi za madini, ikiwa ni pamoja na dhahabu, urani na almasi.
Equatorial Guinea haitambui uraia wa nchi mbili, isipokuwa katika kesi maalumu za kimkataba.
Kuwa raia wa nchi hiyo ni lazima, ni lazima uchague taifa hilo na utumie pasipoti ya Equatorial Guinea.
Eritrea
Eritrea ni nchi ya kaskazini-mashariki mwa Afrika kwenye pwani ya Bahari ya Shamu. Inapakana na Ethiopia, Sudan na Djibouti. Mji mkuu, Asmara, unajulikana kwa majengo yake ya kikoloni ya Italia, kama vile Kanisa Kuu la St. Joseph na Kanisa Kuu la Mtakatifu Mariam na Jumba la Kifalme.
Uraia nchini Eritrea unaelezwa na Katiba ya 1997, ambayo inasema mtu yeyote aliyezaliwa na baba au mama wa Eritrea anapewa uraia wa Eritrea.
Kulingana na sheria za nchi hiyo hakuna kifungu cha wazi cha urai wa nchi mbili kwa Waeritrea
Ethiopia
Ethiopia, uko katika Pembe ya Afrika, ni nchi tambarare, isiyo na bahari iliyogawanyika na Bonde Kuu la Ufa. Ni mahali pa utamaduni wa zamani na makanisa yake ya Kikristo. Fauka ya yote, mji mkuu wake Addis Ababa ndio penye makao makuu ya Umoja wa Afrika.
Sheria ya Ethiopia ya 1930 inasema Waethiopia wanaopata utaifa wa nchi nyingine watakoma kuwa Waethiopia. Wageni wanaotaka kuwa Waethiopia wanahitaji kuthibitisha kwamba tayari wameukana au wanaweza kuukana uraia wao wa asili.
Tanzania
Tanzania ni kivutio maarufu wanyama wengi, ikiwa ni pamoja na wale watano wakubwa; simba, faru, chui, tembo na nyati. Pia ndipo unapopatikana mlima mrefu zaidi barani Afrika, ukiwa na mita 5,895 juu ya usawa wa bahari.
Tanzania pia hairuhusu uraia pacha, isipokuwa kwa watu walio chini ya umri wa miaka kumi na minane ambao walizaliwa katika mataifa mengine. Wanapofikia utu uzima, watu hawa hupoteza moja kwa moja uraia wao wa Tanzania au waamue kuukana uraia wa hiyo nchi nyingine.
Watoto waliozaliwa nje ya nchi wanaruhusiwa kuwa na uraia pacha hadi umri wa miaka 21, na baada ya hapo wanapaswa kuchagua.
Mchakato wa kupata uraia wa nchi unatofautiana kutoka nchi moja hadi nyingine. Njia maarufu za uraia ni pamoja na kuzaliwa, pia mtu anaweza kupata uraia kwa idadi fulani ya miaka kama mkazi wa kudumu, kwa baadhi ya nchi ndoa pia hukupa hadhi ya ukaazi wa kudumu baada ya kufunga ndoa na raia, jambo ambalo huharakisha muda unaohitajika ili kuwa raia rasmi, vilevile uwekezaji, baadhi ya nchi sasa zinatoa uraia kwa uwekezaji wenye thamani ya juu.