P. Diddy anaweza kukabiliwa na hadi kesi 300 – Wakili
Wakili anayewakilisha waathiriwa kadhaa wa Sean “Diddy” Combs, anasema idadi ya kesi za kisheria dhidi ya mwanamuziki huyo “huenda zikafika 300.”
Tony Buzbee aliiambia BBC kuwa timu yake ilipokea takribani simu 3,000 tangu alipofanya mkutano na waandishi wa habari kuwataka walioathiriwa wajitokeze mwezi Oktoba.
“Bado tunapata [simu] kila siku,” aliongeza. “Nadhani kuna uwezekano wa idadi ya kesi kufikia 300, lakini nadhani kiuhalisia, mwishowe tutakuwa na kesi 100 hadi 150,” amesema.
Combs amekanusha mashtaka yote dhidi yake, akiyataja mashtaka hayo kuwa “ya uongo” na matokeo ya watu wanaotafuta “pesa za haraka.”
Katika taarifa kwa BBC, wakili wake Erica Wolff alisema: “Combs ana imani katika ukweli na uadilifu wa mchakato wa mahakama. Mahakamani, ukweli utashinda.”
“Bw. Combs hakuwahi kumshambulia kingono au kusafirisha kingono mtu yeyote – mwanamume au mwanamke, mtu mzima au mdogo,” amesema.
Mwanamuziki huyo kwa sasa anazuiliwa katika gereza la Metropolitan huko Manhattan, akisubiri kufikishwa mahakamani kwa mashtaka tofauti ya utumwa wa ngono na utapeli, na yote anayakanusha.
Waathiriwa ni pamoja na idadi sawa ya wanaume na wanawake, ambao mashtaka yao yanarudi nyuma hadi miaka 20 iliyopita.
Miongoni mwao ni mwanamke anayedai Combs alimbaka katika chumba cha hoteli mwaka 2004 alipokuwa mwanafunzi wa chuo mwenye umri wa miaka 19.
Na mwingine ni mwanamuziki anayedai alipewa dawa za kulevya na kumlazimisha kufanya ngono ya mdomo alipokuwa na umri wa miaka 10.
Kesi hizo hadi sasa zimewasilishwa bila majina, huku wanaodaiwa kuwa waathiriwa wakitajwa kwenye hati za mahakama kama John Doe au Jane Doe.
Hata hivyo, wawakilishi wa Combs wameomba mahakama kutoa vitambulisho vyao ili waweze kujiandaa vya kutosha kwa kesi yoyote ile ijayo.
Katika kesi tatu kufikia sasa, ikiwemo ya mwanamke huyo mwenye umri wa miaka 19, jaji ameamua watalazimika kufichua majina yao ili madai yao yasonge mbele.
Buzbee aliambia BBC. “Ikiwa mlalamikaji atalazimika kufichua utambulisho wake, Combs anatumai walalamikaji wataondoka kimya kimya na hawataleta madai tena.”
“Habari njema ni kwamba, hilo halitatokea. Kwa hivyo ikiwa watalazimika kufichua utambulisho wao, watafichua utambulisho wao, na tutaendelea kusonga mbele.”
Watu mashuhuri huenda watatajwa
Kesi moja imepewa kipaumbele kwa sababu inadai watu wengine mashuhuri walihusika katika makosa dhidi ya Combs.
Kesi hiyo, iliyowasilishwa mjini New York mwezi Oktoba, inamhusu mtoto wa miaka 13 ambaye anadai alipata kizunguzungu baada ya kukubali kinywaji katika karamu moja ya Combs.
Muda mfupi baadaye, anadai mwanaume, ambaye ni mtu mashuhuri, alimvua nguo na kumbaka, huku Combs na mwanamke aliyetajwa kuwa ni mtu mashuhuri wakimtazama.
Siku ya Jumapili, mlalamikaji katika kesi hiyo, alimtaja mtu mashuhuri wa kwanza kama nguli wa muziki wa kufokafoka Jay-Z.
Katika taarifa yake pana, Jay-Z, ambaye jina lake halisi ni Shawn Carter, alitaja madai hayo kuwa “ya kijinga” na kumshutumu Buzbee kujaribu kumchafua kwa kutangaza jina lake hadharani.
Watu wasioaminika
Mitandao ya kijamii imekuwa na uvumi mwingi, unaohusisha madai ya uhalifu wa Combs – watu hutumia picha za sherehe na maonyesho katika miaka ya 1990 na 2000. Lakini hakuna ushahidi wa kuunga mkono madai hayo kupitia picha.
Pia kumekuwa na watu ghushi wasioaminika, ikiwa ni pamoja na wasifu wa uongo unaodaiwa kuandikwa na mpenzi wa zamani wa Combs, marehemu Kim Porter.
Pia wimbo maarufu, ambapo Justin Bieber anaodaiwa kuuwimba, “Nilipotea kwenye sherehe ya Diddy.” Lakini wimbo huo bandia uliozalishwa na AI.
Wanasheria wa Combs wamesema kuna madai “ya uwongo” yanayotolewa na “mawakala wa serikali, mawakili wa walalamikaji, na wengine wenye nia zao fiche.
Jennie VonCannon, mwendesha mashitaka wa zamani wa shirikisho na mwenye uzoefu na kesi za biashara ya ngono na kesi za utapeli, anasema kesi za jinai dhidi ya Combs itabidi kuhitimishwa kabla ya kesi za madai kuendelea.
“Ni lazima kesi ya jinai itangulie, kwa sababu kama utatoa matamshi katika kesi za madai ili ujitetee, unaweza kujitia hatiani.”
“Inaonekana kama serikali bado inazalisha ugunduzi, kwa hivyo inawezekana wataondoa, kubadilisha au kurekebisha hati ya mashtaka, na hata kuongeza washtakiwa zaidi.”