Kina nani wanaomchagua Papa ajaye na wanatoka wapi?

Kufuatia kifo cha Papa Francis mwenye umri wa miaka 88 na mazishi yake Jumamosi, makadinali kutoka kote ulimwenguni hivi karibuni watakusanyika Vatican kumchagua mrithi wake katika mchakato wa siri, wa karne nyingi unaojulikana kama kongamano. Lakini makardinali hawa wanatoka wapi na je, mabadiliko ya kijiografia ya Kanisa yataathiri kura?
Nani anaweza kupiga kura?
Kwa sasa kuna makardinali 252 ambao wanajumuisha Chuo cha Makardinali, 135 kati yao wako chini ya umri wa miaka 80 na kwa hivyo wanastahili kumpigia kura Papa mpya. Hii ndiyo idadi kubwa zaidi ya makardinali wenye umri wa kupiga kura katika historia ya Kanisa Katoliki.
Makardinali ni washiriki wakuu wa makasisi wa Kanisa Katoliki na kwa kawaida huwekwa wakfu kuwa maaskofu.
Papa Francis aliteua idadi kubwa ya makardinali wenye umri wa kupiga kura, 108, wakati wengine walichaguliwa na watangulizi wake Papa Benedict XVI na Mtakatifu John Paul II.
Wataalam wengine wa Vatikani wanasema Papa Francis, Papa wa kwanza wa Amerika Kusini na papa wa kwanza asiye wa Uropa tangu Karne ya 8, alijaza chuo hicho kwa makusudi katika jaribio la kuhakikisha kuendelea kwa urithi wake unaoendelea zaidi na unaojumuisha.
Kanisa linalobadilika
Uwakilishi wa kijiografia wa chuo hicho ulibadilika wakati wa upapa wa miaka 12 wa Papa Francis.
Kwa mara ya kwanza katika historia, Ulaya haina tena makardinali wengi wa umri wa kupiga kura – sasa wanawakilisha 39% ya makardinali wenye umri wa kupiga kura, chini kutoka 52% mnamo 2013.
Mchoro huu unaonyesha kusambaa kwa makardinali katika kila bara, na wale wanaostahili kupiga kura kwa rangi nyekundu na wale ambao hawastahiki katika rangi ya kijivu.
Kati ya makardinali 108 wa umri wa kupiga kura walioteuliwa na Papa Francis, 38% wanatoka Ulaya, 19% kutoka Amerika ya Kusini na Caribean, 19% kutoka eneo la Asia-Pasifiki, 12% kutoka Kusini mwa Jangwa la Sahara, 7% kutoka Amerika Kaskazini, na 4% kutoka Mashariki ya Kati na Afrika Kaskazini. Idadi ya wasio wazungu ni jumla ya 73.
Mabadiliko haya kuelekea Kanisa Katoliki lenye uwakilishi mkubwa zaidi ulimwenguni ni kuongeza kasi ya mwenendo ulioanza katika karne ya 19, anasema Dk Miles Pattenden, mwanahistoria wa Kanisa Katoliki katika Chuo Kikuu cha Oxford. Kabla ya hili, makardinali walikuwa karibu kabisa Ulaya na wengi wao wakiwa Waitaliano.
Pattenden anasema Papa Francis aliamini Chuo hicho kinapaswa kuwa na uwakilishi wa jamii zote za Kikatoliki ziwezekanazo haijalishi jamii ni ndogo kiasi gani.
Hii inaelezea ni kwa nini uteuzi ulifanywa katika nchi kama Mongolia, Algeria, na Iran wakati wa upapa wake badala ya Ireland au Australia, Pattenden anaelezea.
Je, jiografia inaathiri kura?

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Kwa umma, makardinali watasema kwamba jiografia haiathiri uamuzi wao, lakini katika uchaguzi kuna uwezekano wa kuwa sababu, anabainisha Pattenden.
Anasema makardinali wengi kutoka kusini mwa dunia wanaamini kwa faragha kuwa ni wakati wa papa mwingine kutoka eneo lao – haswa Asia au Afrika – wakati Wazungu wengi, haswa Waitaliano, wanahisi upapa unapaswa kurudi huko.
Pia kuna mgawanyiko kati ya makardinali wanaoishi Roma – iliko Vatican – na wale ambao hawana.
Makardinali wengi wa Italia watakuwa wamefanya kazi pamoja kwa muda mrefu zaidi kuliko wenzao, Pattenden adokeza, na wana uwezekano mkubwa wa kupiga kura kama kizuizi cha mshikamano.
Itikadi ya kisiasa pia itachukua jukumu muhimu katika kura.
“Kwa mfano, makardinali wengi wa Amerika Kusini wameendelea kabisa,” anasema Pattenden.
“Wao ni tofauti sana na makardinali wa Kiafrika ambao kwa ujumla ni wahafidhina kabisa – na miungano inapanuika katika jiografia.”
Jinsi kura inavyopoigwa

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Wakati wa mkutano huo, makardinali hutengwa na ulimwengu wa nje na kutopokea simu,na vyombo vya habari
Wanakaa Casa Santa Marta – nyumba ya wageni ya ghorofa tano katika Jiji la Vatican – na kutembea kila siku hadi Sistine Chapel, ambapo upigaji kura hufanyika kwa siri.
Kila kardinali anaandika chaguo lake kwenye kura na kuiweka kwenye chupa kubwa la fedha na dhahabu.
Mshindi anahitaji theluthi mbili ya wingi ili kuchaguliwa.
Wakati haya yote yanafanyika, Wakatoliki husubiri katika Uwanja wa St Peter’s ulio karibu, wakitazama moshi uinuke kutoka kwenye bomba la moshi la Sistine Chapel: Moshi mweusi inamaanisha hakuna uamuzi, mweupe unaashiria Papa mpya amechaguliwa.
Papa mpya, ambaye anapaswa kukubali rasmi jukumu hilo mbele ya Chuo cha Makardinali, kwa kawaida huonekana kwenye balcony (varanda) inayoangalia St Peter’s Square ndani ya saa moja baada ya kuchaguliwa kwake.
Kongamano refu zaidi katika historia lilidumu miaka miwili na miezi tisa, kuanzia 1268 – lakini katika siku za hivi karibuni mchakato wa kumchangua Papa mekuwa za haraka zaidi, kwa wastani wa siku tatu tangu mwanzoni mwa Karne ya 20.
Papa Francis na mtangulizi wake Papa Benedict XVI walichaguliwa katika kipindi cha siku mbili tu.
Hakuna mgombea anayefahamika dhahiri

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Tangu kifo cha Francis, majina mengi yamependekezwa kama warithi wanaowezekana – kutoka Italia hadi Canada na Ghana hadi Ufilipino.
Pattenden anasema majadiliano tayari yatafanyika kati ya makardinali ili kuona ikiwa kuna makubaliano yoyote yanayojitokeza nyuma ya mgombea mmoja au wawili.
Hata hivyo, anasema matokeo ni magumu kutabiri.
“Tofauti na uchaguzi wa uongozi katika chama cha siasa, ambapo kupata idadi inayohitajika ya kura inahakikisha ushindi, mchakato huo unahusisha zaidi ya sheria rahisi ya wengi,” anasema.
“Kuna hisia kwamba Kanisa linahitaji kusonga kwa kiwango fulani kupitia makubaliano, ambayo inamaanisha ni muhimu kutowatenga wachache.”