Fahamu nchi zinazosheherekea Eid Al-Fitr leo

Fahamu nchi zinazosheherekea Eid Al-Fitr leo

Wakati nchi za Afrika Mashariki zikiwemo Tanzania, Kenya na Uganda zikisubiri Mamlaka kutangaza rasmi kuonekana kwa mwezi na kuanza kwa sherehe za Eid al-Fitr kwa baadhi ya madhehebu, nchi nyingi za Kiislamu duniani zinasherehekea Eid Al Fitr leo Jumapili, Machi 30, 2025, baada ya kuona mwezi wa Shawwal (Eid al-Fitr 1446 AH) siku ya Jumamosi, Machi 29, 2025.

Hata hivyo, zipo baadhi ya nchi zingine za kiislamu zitasherehekea Eid Jumatatu, Machi 31, 2025, kwa sababu zitafanya uchunguzi wa hilali ya mwezi siku ya leo Jumapili, Machi 30, 2025.

Nchi za Ghuba, isipokuwa Oman, zinasherehekea Eid Al Fitr Jumapili, Machi 30, 2025, baada ya kuthibitisha kuona hilali ya Shawwal huko Saudi Arabia na Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE).

Huko Oman, taifa hilo litakamilisha siku 30 za kufunga na kusherehekea Eid Jumatatu, Machi 31, 2025.

Utofauti wa kutangazwa kwa Eid duniani

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Zipo nchi hutumia vifaa maalumu vya kuuonea mwezi kabla ya kutangaza kuonekana kwake na kuanza kwa sherehe za Eid

Eid kusheherekewa siku tofauti imekuwa mjadala wa miaka nenda rudi. Tofauti hii, ambayo ni ya kawaida katika kalenda ya Kiislamu, inatokana na tofauti za kuona hilali za mwezi zinazohusiana na kumalizika kwa mwezi wa Ramadhani, ambao ni mwezi wa kufunga na tafakari ya kiroho inayosherehekewa na Waislamu duniani kote.

Hilali za mwezi maana yake ni mwezi mpya au mwezi mchanga unaoanza kuonekana tena baada ya hali ya kutoonekana kwe takribani mwezi mmoja na uonekana kwa umbo la upinde mwembamba. Hiali hii huashiria pia kuanza kwa mwezi Mpya wa kiislamu wa Shawwal.

Zipo nchi ambazo zenyewe hutumia vifaa maalumu vya kuuonea mwezi kabla ya kutangaza kuonekana kwake na kuanza kwa sherehe za Eid. Nchi nyingine nyingi hasa za Afrika husubiri kuona mwezi kwa macho katika maeneo yao kupitia mamlaka zilizopewa hadhi ya kufanya hivyo na kutangaza kwa niaba ya waislamu wa nchi au maeneo husika.

Ingawa ni kawaida pia kuona nchi moja, Eid ikaswaliwa katika siku mbili tofauti, mfano wengine wanaswali leo, wangine kesho. Ni mjadala wa siku nyingine lakini kwa ufupi linabebwa na utofauti wa kimamlaka kwenye utambuzi wa kuuona mwezi.

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Baadhi ya nchi na waumini wake zikiwemo za Afrika Mashariki wanasubiri kutangazwa kuonekana kwa mwezi kupitia mamlaka maalumu, kabla ya kusheherea Sikukuu ya Eid al-Fitr.

Huko Oman, Kamati ya Uangalizi wa Hilali ilitangaza kuwa hilali ya mwezi inayotangaza kuanza kwa Shawwal, mwezi unaofuata Ramadhani, haikuonekana usiku wa Jumamosi. Nchi hiyo itakamilisha siku 30 za kufunga, na Eid rasmi inaanza Machi 31, 2025.

Matangazo kama hayo yalitolewa nchini Misri, Syria, Jordan, Morocco, Tunisia, na Libya ambapo mamlaka za kidini zilithibitisha kuwa Jumapili itakuwa siku ya mwisho ya Ramadhani.

Indonesia, nchi yenye Waislamu wengi duniani, pamoja na Pakistan, Malaysia, Brunei, India, Bangladesh, na Australia, pia ilitangaza Jumatatu kuwa siku ya kwanza ya Eid.

Nchi kama Pakistan, Japani, Ufilipino, Malaysia, na Brunei zitafanya uchunguzi wa hilali ya mwezi Jumapili.

Katika nchi nyingi hizi, Jumamosi ilikuwa ni siku ya 28 au 29 tu ya Ramadhani, hivyo kwao sherehe za Jumapili zilikuwa za kisayansi zisizowezekana.

Maombi ya Eid Al Fitr katika nchi za Kiarabu

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waislamu wametekeleza sala ya asubuhi karibu na Kaaba katika Msikiti Mkuu mjini Makkah, Saudi Arabia, kuashiria mwanzo wa Sikukuu ya Eid al-Fitr, ambayo inaashiria kumalizika kwa mwezi mtukufu wa kufunga wa Ramadan, mapema asubuhi ya Machi 30, 2025.

Nchi za GCC, Baraza la Ushirikiano la Nchi za Ghuba (Gulf Cooperation Council), ambalo linajumuisha nchi sita za Kiarabu za eneo la Ghuba. Nchi hizo ni Saudi Arabia, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Qatar, Bahrain, Kuwait na Oman. Nchi nyingi hizi zimesheherekea Eid leo Jumapili.

Nchi za Saudi Arabia, UAE, Kuwait, Bahrain, Yemen, pamoja na nchi zingine za Uturuki, Palestina, Sudan, na Lebanon zilithibitisha kuona hilali za mwezi Jumamosi na zinasherehekea Eid Jumapili.

Huko Saudi Arabia na UAE, Mahakama Kuu ya kifalme na Mahakama ya Rais wa UAE walitoa taarifa rasmi baada ya kamati zao za uangalizi wa hilali kukutana na kuthibitisha kuanza kwa Shawwal.

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waislamu hasa kutoka nchi za Kiarabu waishio Ulaya nao wameswali swala ya Eid al-Fitr. Huko Madrid Hispania leo, Machi 30, 2025 waislamu hawa walitekeleza swala hiyo katika eneo la Julian Marias Square

Huko Iraq, ingawa ofisi za Sunni Endowment na ofisi ya Grand Ayatollah Ali Al Sistani, mamlaka kuu ya Shiite nchini humo, zilitangaza kuwa Eid itasherehekewa Jumatatu, Serikali ya Kikurdistan ilitangaza Jumapili kama siku ya kwanza ya sherehe, ikinukuu kuona kwake hilali.

Nchini Lebanon, mamlaka za Sunni zilithibitisha Jumapili kama Eid, huku Baraza Kuu la Kiislamu la Shiite likichelewesha uamuzi wake hadi Jumapili jioni, na kuashiria kuwa Eid inaweza kufanyika Jumatatu au Jumanne kwa jamii za Shiite, kulingana na uwazi wa hilali.

Kwa wakati wa kuandika makala hii, jumla ya nchi 11 zilikuwa zimethibitisha kuwa zitasherehekea Eid Jumapili, huku 15 zingine zikitangaza Jumatatu kama siku ya kwanza ya Eid. Nchi nyingine nyingi zilikuwa bado zinangojea kuona hilali za mwezi au hazikutoa taarifa rasmi.

Baadhi ya nchi zinazozosherehekea Eid Jumapili, Machi 30, 2025

.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Waislamu katika mji mkuu wa Umoja wa Falme za Kiarabu, Abu Dhabi, wakitekeleza swala ya Eid al-Fitr katika Msikiti Mkuu wa Sheikh Zayed, leo tarehe 30 Machi, 2025.

– Saudi Arabia

– UAE

– Qatar

– Bahrain

– Kuwait

– Uturuki

– Yemen

– Palestina

– Sudan

– Ethiopia

– Lebanon (mamlaka za Sunni)

– Iraq – Serikali ya Kikurdistan pekee

Baadhi ya nchi Zitakazosherehekea Eid Jumatatu, Machi 31, 2025

m

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Maelezo ya picha, Sudan na Ethiopia ni miongoni mwa nchi zilizosheherekea Eid leo, Machi 30, 2025

– Oman

– Misri

– Syria

– Jordan

– Morocco

– Indonesia

– Pakistan

– Malaysia

– Brunei

– India

– Bangladesh

– Australia

– Iraq – Sunni na mamlaka za Shiite

– Tunisia

– Libya

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *