Burundi yatoa onyo dhidi ya shambulio lolote kutoka Rwanda

Burundi yatoa onyo dhidi ya shambulio lolote kutoka Rwanda

Burundi imetishia kujibu vikali shambulio au uvamizi wowote utakaotokea nchini humo kutoka Rwanda.

” Tunafahamu Rwanda inajaribu kutuvamia kupitia ardhi ya DRC ili wasingizie kuwa ni waasi wa Red Tabara na M23. Lakini tunawaambia kwamba ikiwa mnaona kushambulia Bujumbura ni karibu kutoka Uvira basi nasi tunaweza kushambulia Kigali kutoka mji wa Kirundo” Alionya Rais Ndayishimiye.

Akiongea na BBC, Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye, amesema kuwa wamepata taarifa za kuaminika kuwa taifa la Rwanda linapanga kuishambulia Burundi.

Hata hivyo serikali ya Rwanda imekanusha vikali madai ya serikali ya Burundi.

”Matamshi ya Burundi ni ya kushangaza kwasababu idara za ulinzi za nchi hizi mbili zimekuwa zikikutana kujadili namna ya kulinda mipaka yao haswa wakati huu kuna mzozo Mashariki mwa DRC,”msemaji wa serikali ya Rwanda Yolanda Makolo aeleza.

Ndayishimiye amesema Rwanda itakuwa imefanya kosa kubwa kuivamia Burundi kwa njia yoyote ile akisema Burundi itajibu kwa njia ya Kijeshi, na hivyo kuonya uwezekano wa kuzuka kwa vita vya kikanda.

Rais huyo wa Burundi amesema pia “hatutakubali kuchinjwa kama mbuzi, kama vile Wakongomani”

Ndayishimiye aliifahamisha BBC kuwa serikali yake tayari imetuma ujumbe kwa rais wa Rwanda Paul Kagame ili mchakato kwa kutekeleza makubaliano yao ya maridhiano ili kupunguza uhasama kati yao.

“Tumefanya mazungumzo na Rwanda kwa muda mrefu na tukakubaliana na ilipofika wakati wa utekelezaji, Rwanda ikasita” aliongeza Rais Ndayishimiye.

Burundi imeishutumu Rwanda kwa kuwapa hifadhi watu wanaoaminika walijaribu kufanya mapinduzi ya serikali nchini Burundi mwaka wa 2015. Aidha Burundi imedai kuwa utawala wa wa Rais Paul Kagame inawapa misaada waasi wa Red Tabara, ambão mara kwa mara hufanya mashambulizi ya kuvizia nchini Burundi kutoka Mashariki mwa DRC .

Amesema Burundi imejiandaa vilivyo kulinda mipaka yake na kamwe haitaruhusu uvamizi wa aina yoyote na kuishutumu, Rwanda kwa kufadhili makundi ya waasi yanayosababisha maafa Mashariki mwa Congo.

Mashambulizi ya hivi karibu kutoka kwa waasi wa Red Tabara, nchini Burundi, yalisababisha nchi hiyo kufunga mipaka yake na Rwanda.

Utawala wa Burundi umesema kuwa mchakata wa kuwakamata na kuwafungulia mashtaka viongozi wa waasi wa Red Tabara unaendelea na kuwa serikali haina nia yoyote ya kufanya mazungumzo nao. Rais Ndayishimiye amesema kuwa jukumu la serikali yake sasa ni kuwasaka waasi hao na kuwafikisha mahakamani.

Rais Ndayishimiye amesema Burundi haina nia yoyote ya kuvamia nchi nyingine au kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine na hivyo inastahili kupewa heshima kama hiyo pia.

Burundi yataka mazungumzo kati ya Tshisekedi na makundi ya waasi

Ramani inayoonyesha ujirani kati ya Rwanda na Burundi

Kuhusu mzozo wa Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Rais Ndayishimiye ametoa wito kwa rais wa DRC, Felix Tshisekedi kuanzisha mazungumzo ya moja kwa moja na wadau wote wakiwemo viongozi wa makundi yote ya waasi, ili kujaribu kutafuta suluhishi la mzozo wa vita unaoendelea Mashariki na nchi Hiyo.

Rais Ndayishimiye amesema njia ya pekee ya kuaminika kutatua mzozo wa DR Congo ni kupitia mazungumzo ambayo yatashirikisha wakongomani wote.

Amesema Burundi inaunga mkono mazungumzo yanayoongozwa na wakuu wa jumuiya za SADC na Afrika Mashariki, za kuwaleta pamoja viongozi wa DRC na wale wa waasi kwenye meza moja ya mazungumzo.

“Kuna haja gani, kushiriki katika vita vinavyosababisha vifo vya raia, kisha wakati tumewapoteza mamilioni ya raia tunaanza mazungumzo. Hii sio haki. Mazungumzo yanapaswa kuwa hatua ya kwanza na vita kuwa hatua ya mwisho” alisema Rais Ndayishimiye.

Ndayishimiye amesema mzozo wa DRC ni suala ambalo linaweza kutatutiliwa ndani ya nchi ikiwa viongozi wote wa DRC watakuwa na dhamira njema. Ameonya kuwa mzozo huu unaweza kuendelea kwa muda mrefu ikiwa viongozi hawatajitolea kwa maslahi ya raia.

Amesema mataifa ya Afrika hasa DRC haipaswi kuwa katika hali ya umasikini kutokana na rasilimali zake za madini, udongo wenye rotuba na mvua inayonyesha kwa misimu kadhaa mbali na rasilimali zingine.

Ndayishimiye amesema mzozo wa DRC unaweza kutatuliwa ikiwa rasilimali za serikali zitatumika vyema kwa maslahi ya wanainchi wa DRC na viongozi kuwajibika.

” itakuwa shida kubwa sana ikiwa watu wachache watafaidika na rasimali za wanainchi huku wanainchi wakiwa masikini. Na hi inaweza kusababisha raia kuanzisha uasi na vita kwa sababu mali yao inafaidisha wachache” alisema Ndayishimiye”.

Waasi wa M23 wanaosadikika kuungwa mkono na Rwanda wameteka maeneo mengi ya mikoa ya Kivu ya Kaskazini na Kusini ikiwemo miji mikuu ya Goma na Bukavu. Rwanda hata hivyo imekanusha madai kuwa inaunga mkono waasi hao wa M23, ikisema haina nia wala dhamira ya kuunga kundi lolote la waasi nchini DRC.

Rwanda inasema vita vinavyoendelea Mashariki mwa DRC ni suala la ndani la nchi hiyo, lakini wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamebainisha uwepo wa wanajeshi wa Rwanda nchini DRC, suala ambalo Rwanda imekanusha.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *