Mzozo wa DRC: Muhoozi Kainerugaba atishia vikosi vyake vitateka mji wa Kisangani

Mwanajeshi mkuu wa Uganda Muhoozi Kainerugaba ambaye ni mtoto wa Rais wa nchi hiyo, amesema kuwa vikosi vyake vitadhibiti mji wa Kisangani iwapo waasi wa M23 watachelewa kuteka mji huo.
Kupitia mtandao wake wa kijamii wa X ambapo amezungumzia mengi kuhusu DRC, Kainerugaba, amesema jeshi lake au waasi wa M23 wataingai Kisangani kwa agizo la Rais Yoweri Museveni ili kuwaokoa wakaazi wa mji huo wakati wowote kutoka sasa.
Wanajeshi wa Uganda wamekuwa nchini DRC, wakishirikiana na jeshi la FARDC, kupambana na makundi yenye silaha wakiwemo waasi wa CODECO na ADF.
Akionekeana kuongelelea kuwa nia ya kulinda wakaazi wa DRC ameapa kuwa hataacha wakaazi wenye asili ya Uganda kama vile Alurs, Bahema, Banande na Batutsi wapitie changamoto na kusema ana haki ya kuwalinda.
Aidha pia amepedekeza Rais wa Marekani Donald Trump asiingie katika kataba wowote wa madini Afrika Mashariki bila Uganda na Rwanda.
Sio mara ya kwanza Kianerugaba kutoa kauli za kutatanisha katika mtandao wake wa kijamii wa X.
Licha ya waasi wa M23 kuchukua miji kadhaa ya mashariki mwa Congo, waasi hao hawajaonesha nia ya kutaka kudhibiti mji wa Kisangani, M23 ikidai inapanga kujiondoa katika mji wa Walikale ili kutoa nafasi ya mazungumzo na serikali.