Kuchangia damu hupunguza hatari ya saratani – utafiti

Watu wanao changia damu mara kwa mara wana uwezekano mkubwa wa kuwa na mabadiliko ya (jeni) vinasaba katika damu yao, mabadiliko ambayo yanaweza kupunguza hatari ya kupata saratani, unaeleza utafiti.
Watafiti kutoka Taasisi ya Francis Crick, wanasema matokeo hayo yanavutia na yanaweza kusaidia kuelewa kwa nini saratani ya damu huibuka.
Utafiti wao ulilinganisha damu ya makundi mawili ya wanaume wenye afya njema walio katika miaka yao ya 60 – kundi la kwanza lilikuwa ni la wale waliochangia damu mara tatu kwa mwaka kwa miaka 40, kundi jingine ni wale waliochangia damu mara tano katika maisha yao.
Mabadiliko ya vinasaba ambayo hupunguza hatari ya kupata saratani ya damu yalikuwepo katika makundi ya watu hao walio changia damu. Lakini kwa sababu watu wenye afya bora ndio wanao changia damu, matokeo hayo bado hayatoi picha kamili.
Kadiri mtu anavyozeeka, seli za mwili – ikiwa ni pamoja na za damu – kawaida hubadilika, na hilo huongeza hatari ya magonjwa kama vile saratani.
Lakini watu wanapochangia damu, seli zilizopo kwenye uboho (ndani ya mifupa) hutengeneza seli mpya za damu ili kuziba pengo la damu iliyopotea – mchakato huo unaweza kusababisha mabadiliko ya maumbile ya vinasaba katika uboho.
Watafiti waligundua kiwango cha mabadiliko ya vinasaba katika damu ya kundi la watu 217, waliochangia damu mara kwa mara na kundi la pili la watu 212 waliochangia damu mara tano tu katika maisha yao.
Lakini mabadiliko hayo katika seli za uboho yalikuwa tofauti: 50% ni kwa waliochangia damu mara kwa mara. 30% kwa waliochangia damu mara chache.
“Ni aina ya mabadiliko ambayo hupunguza hatari ya kupata sarakani ya damu (leukemia),” anasema mtafiti wa utafiti huo Dk. Hector Huerga Encabo.
Na panya walipodungwa chembechembe hizi za seli za damu ya binadamu kwenye maabara, seli hizo zilionekana kufanya kazi vyema katika kutengeneza seli nyekundu za damu, anasema Dk Encabo.
Utafiti zaidi unahitajika
Utafiti huo uliochapishwa katika jarida la Blood, ulifanywa na wanasayansi kutoka Heidelberg, kwa usaidizi wa kituo cha uchangiaji damu cha Msalaba Mwekundu cha Ujerumani.
Timu hiyo ya utafiti sasa inapanga kutafiti damu ya idadi kubwa zaidi ya watu, ikiwa ni pamoja na wanawake.
Matokeo ya sasa ni ukumbusho kwamba mambo madogo madogo ya kila siku, mabadiliko ya mazingira – pamoja na umri, huathiri tishu na damu, na kubadilisha seli za uboho, anasema Dk Encabo.
“Bilashaka watu wanaotoa damu wana uwezekano mkubwa wa kuwa na afya njema, ili kufaa kuchangia na hilo pia linaonekana katika seli zao za damu,” anasema mtafiti mkuu Dominique Bonnet, ambaye ni mkuu wa maabara ya seli za uboho katika taasisi ya Crick.
Kitengo cha damu na upandikizaji, cha Huduma ya Taifa ya Afya ya Uingereza (NHS), kinasema utafiti huo “unavutia” lakini kazi zaidi ya utafiti inahitajika, kwa sababu watu wenye afya bora ndio ambao huchangia damu kwa kawaida.
“Afya njema ya wachangia damu inafanya kuwa vigumu kuelewa afya jumla ya wachangiaji hao,” anasema mkurugenzi wa matibabu Dk Lise Estcourt.
“Hata hivyo, jambo muhimu zaidi ni kwamba watu wanaochangia damu huboresha afya za watu wengine.”
Nchini Uingereza, watu wenye umri kati ya miaka 17-65 walio na afya nzuri, wanaweza kuchangia damu – ikiwa wanakidhi vigezo vingine vyote muhimu.
Lakini sio wale waliougua saratani, kupandikizwa kiungo au kuwa na Virusi vya Ukimwi (VVU), miongoni mwa mambo mengine.
Na baadhi ya watu wanaweza kusubiri, kwa mfano ikiwa amejifungua mtoto katika miezi sita iliyopita au amechora tatuu hivi karibuni au kutoboa.