Unajua joto kali la chumbani ni hatari kwa figo na moyo wako?

Unajua joto kali la chumbani ni hatari kwa figo na moyo wako?

Kuwa na joto kupita kiasi au baridi kupita kiasi kunaweza kuwa hatari kwa afya yako. Lakini, ni joto gani bora kwa nyumba yako?

Kama mtu anayehisi baridi sana lakini hapendi kuongeza kiwango cha joto mara kwa mara, chupa ya maji moto na koti nene ni marafiki wa wa watu wengi wa karibu. Kadri dhoruba za baridi zinavyovuma kwenye pwani ya mashariki ya Marekani na Canada na nchi nyingine duniani zikiwa katikati ya msimu mrefu wa baridi, unaweza pia kujiuliza, joto gani bora kwa afya na faraja ndani ya nyumba? Jibu, kwa kweli, si rahisi.

Katika miaka ya 1860, daktari wa Kijerumani Carl Wunderlich alipima joto la watu wapatao 25,000 na kupata wastani wa 37°C (98.6°F). Hili limekubalika kwa muda mrefu, lakini tafiti mpya zinaonyesha kuwa mwili wa binadamu una viwango tofauti vya joto. Joto la mwili hutofautiana kulingana na jinsia, kiwango cha metaboli, homoni, shughuli za mwili, umri na hata mzunguko wa hedhi. Hivyo basi, je, kuna kiwango sahihi cha joto cha kuweka nyumbani kwako?

a

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Kwa nchi zenye hali ya hewa ya wastani au baridi, Shirika la Afya Duniani (WHO) linapendekeza kuwa joto la chumbani liwe angalau 18°C (64.4°F) ili kulinda afya dhidi ya madhara ya baridi. Kuishi kwenye mazingira baridi na yenye unyevunyevu kunaweza kusababisha madhara kwa afya ya mwili na akili, ikiwemo kuongezeka kwa pumu, hatari ya ugonjwa wa moyo, wasiwasi na msongo wa mawazo.

Rebecca Wilson, mtaalamu mkuu wa afya ya umma nchini Wales, anasema:

“Tunatambua kuwa nyumba zenye afya ni nguzo muhimu za afya njema. Hii inamaanisha kuwa nyumba zinapaswa kuwa salama, zenye faraja na joto linalofaa ili kulinda afya na kusaidia jamii kuwa na ustahimilivu wa kiafya.”

Tafiti za msimu wa baridi za 2022 na 2023 za Public Health Wales zilionyesha kuwa watu walikuwa wakihisi msongo wa mawazo kutokana na kuongezeka kwa gharama za nishati. Wengi walipunguza matumizi ya joto nyumbani na badala yake walitumia chupa za maji moto na blanketi ili kupata joto.

Hata hivyo, kuwa na joto kupita kiasi pia ni hatari, hasa kwa wale wanaoishi kwenye maeneo yenye joto kali. Kuongezeka kwa joto kunaweza kusababisha uchovu wa joto (heat exhaustion) na kiharusi cha joto (heatstroke), ambavyo huongeza mzigo kwa moyo na figo. Joto kali pia linaweza kuathiri afya ya akili, na hata limehusishwa na ongezeko la hatari ya kujiua.

Makundi yaliyo hatari zaidi

a

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Wazee, watoto wachanga na watoto wadogo wako hatarini zaidi kwa sababu miili yao haiwezi kudhibiti joto kwa ufanisi. Kwa mfano, shirika la The Lullaby Trust nchini Uingereza linapendekeza kuwa joto la chumba cha mtoto mchanga liwe kati ya 16-20°C (60-68°F) ili kuzuia hatari ya kifo cha ghafla cha watoto wachanga (SIDS).

Kwa upande mwingine, wazee wanahitaji nyumba zao ziwe na joto zaidi kwa sababu kasi yao ya metaboli inapungua wanapozidi kuzeeka. Hii inamaanisha kuwa miili yao haitengenezi joto la kutosha. Pia, magonjwa kama kisukari yanaweza kuathiri mtiririko wa damu, hivyo kufanya iwe vigumu kwa mwili kupata joto. Tafiti zinaonyesha kuwa hata nyumba zilizo na joto la 18°C (65°F) zinaweza kusababisha baridi kali kwa wazee, na kuongeza hatari ya hypothermia.

Wanaume na wanawake wanahisi joto kwa njia tofauti. Wanawake huwa na mafuta mengi kati ya ngozi na misuli yao, ambayo huhifadhi joto ndani ya mwili lakini huzuia joto kufika kwenye ngozi na viungo vya nje kama vidole na pua. Tafiti zinaonyesha kuwa mikono ya wanawake inaweza kuwa baridi kwa takriban 3°C (37°F) kuliko ya wanaume wanapokumbwa na baridi.

Aidha, mzunguko wa hedhi pia huathiri joto la mwili, kwani joto la ndani ya mwili hufikia kiwango cha juu zaidi baada ya ovulation. Hata hivyo, kwa kuwa wanawake kwa kawaida wana kiwango cha chini cha metaboli kuliko wanaume, mara nyingi huhisi baridi zaidi hata kama wana joto la juu la mwili.

Joto gani sahihi na bora kwa kulala?

b

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

Kulala kwa starehe kunahusiana na joto la mwili. Dakika chache kabla ya kulala, joto la ndani la mwili hupungua, na hii husaidia mtu kupata usingizi mzito. Hii ndiyo sababu kuoga maji moto kabla ya kulala kunaweza kusaidia kupata usingizi.

Profesa Bill Wisden, mtaalamu wa usingizi kutoka Imperial College London, anasema:

“Kuwa na joto kupita kiasi unapolala ni jambo baya. Ni sawa na kelele au maumivu, kwani husababisha mihemko ya mwili na kukuamsha.”

Kwa hivyo, joto bora kwa chumba cha kulala ni kati ya 16-18°C (60-65°F). Wazee wanaweza kupendelea joto la juu kidogo, lakini chumba kilicho na joto kupita kiasi kinaweza kusababisha mtu kushtuka mara kwa mara usiku, hivyo kupunguza ubora wa usingizi.

Kwa kuhitimisha, hakuna joto moja linalofaa kwa kila mtu, kwani mambo mengi  kutoka umri hadi jinsia, kiwango cha metaboli hadi homoni  huathiri jinsi tunavyohisi joto au baridi. Hili linaeleza kwa nini mara nyingi watu hujikuta wakibishana kuhusu kiwango sahihi cha joto la thermostat nyumbani.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *