Rwanda bila misaada: Je, inaweza kujitegemea?

Hivi karibuni nchi za Ulaya, Marekani na Canada zimekuwa zikitangaza hatua ya kukata misaada dhidi ya Rwanda, kufuatia kile kinachoelezwa na nchi hizo za Magharibi kwamba inaunga mkono kundi la M23 liloteka maeneo ya mashariki mwa DRC, ikiwemo miji ya Goma na Bukavu.
Nchi hizo zinaituhumu Rwanda kuchochea ghasia katika eneo la Mashariki mwa DRC kwa kuwaunga mkono waasi wa kitutsi wa Congo wa kundi la M23, tuhuma zinazokanushwa vikali na Rwanda.
Lakini je, Rwanda inaweza kujitegemea bila misaada?
Kujibu swali hili ni vyema kuelewa ni kwa namna gani Rwanda inategemea misaada kutoka mataifa ya kigeni kwa ajili ya kuendesha uchumi wake.
Kulingana na takwimu za Benki ya Dunia, Rwanda ilikadiriwa kutegemea kwa kiasi kikubwa misaada ya kigeni mnamo 2024, huku makadirio yakionyesha kuwa misaada na mikopo kutoka nje inaweza kuchangia na karibu 27% ya jumla ya bajeti ya taifa hilo. Inakadiriwa kuwa Rwanda inapokea zaidi ya dola bilioni 1 ya msaada wa kigeni
Nchi za Ulaya kupitia Muungano wa Ulaya (EU) zimetangaza kusitisha misaada ya kifedha za maendeleo ya Umoja wa Ulaya kwa Rwanda na hatua hii, inatarajiwa kuathiri uendeshaji wa shughuli zinazodhaminiwa na misaada hiyo.
EU ni mdhamini mkubwa wa Rwanda ambapo ilitenga €260 milioni katika ufadhili wa ruzuku kwa ushirikiano na Rwanda katika kipindi cha 2021-2024. Rwanda pia inafaidika na programu kadhaa za nchi nyingi za EU.
Umoja wa Ulaya (EU) na Rwanda zina ushirikiano unaozingatia maendeleo ya kiuchumi, haki za binadamu na ukuaji endelevu. EU pia inafanya kazi na Rwanda katika masuala kama vile mabadiliko ya hali ya hewa na uhamiaji.
Fedha hizi zilizotolewa kwa ajili ya kufanikisha azma ya Rwanda ya kubadilisha uchumi wake, kuendeleza mabadiliko ya tabia nchi, kukuza jamii yenye usawa na kuwa nchi yenye kipato cha kati ifikapo 2035 kulingana na Mkakati wa Kitaifa wa Mabadiliko na Dira ya Rwanda 2050 na Mkakati wa Global Gateway wa EU.
Kando na EU, Uingereza ni moja wapo ya nchi zinazotoa kiwango kikubwa cha msaada kwa Rwanda. Rwanda hupokea msaada wa pauni milioni 32 kutoka Uingereza Lakini kutokana na tuhuma za kuwaunga mkono waasi wa M23, nchi hiyo imetishia kukata msaada huku.
Hili litaathiri shughuli zinazodhaminiwa na msaada huu ikiwa ni pamoja na mirambi mbali mbali ya kimaendeleo pamoja na bajeti ya ulinzi.
Akitoa tisho la vikwazo kwa Rwanda, Waziri wa mambo ya nje wa nchi hiyo David Lammy alisema Rwanda ilipokea zaidi ya $1bn ya misaada ya kimataifa kila mwaka, ikiwa ni pamoja na takriban £32m za msaada wa ushirikiano baina ya nchi mbili.
“Yote hayo yanatishiwa unaposhambulia majirani zako, na tuko wazi kwamba hatuwezi kuwa na nchi zinazopinga uadilifu wa eneo la nchi nyingine. Vile vile hatutaivumilia katika bara la Ulaya, hatuwezi kuivumilia popote inapotokea duniani. Tunapaswa kuwa wazi kuhusu hilo,” Lammy alisema.

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Inapokuja katika inapokuja katika suala la misaada ya maendeleo kwa Rwanda Ujerumani, Ujerumani kimekuwa na ushirikiano na Rwanda kwa muda mrefu.
Ujerumani ni mshirika wa mrefu wa Rwanda, ikidhamini miradi mbalimbali ya kimaendeleo hususa ni teknolojia na kilimo kupitia ushirikiano wa jimbo Ujerumani ya la Rhineland-Palatinate.
Waziri wa Ujerumani ilisema Berlin iliahidi kwa mara ya mwisho msaada wa euro milioni 93.6 (dola milioni 98) kwa Rwanda mnamo Oktoba 2022 kwa kipindi cha 2022 hadi 2024, pesa ambazo zimekuwa zikitumika katika shughuli za maendeleo ya nchi hiyo ikiwa ni pamoja na kilimo na mabadiliko ya tabia nchi.
Ujerumani pia imetoa msaada wa kiwanda cha uzalishaji chanjo cha kampuni ya Ujerumani ya BioNTech kilichozinduliwa Kigali mwaka 2022.
Ujerumani inatoa usaidizi mkubwa kuhusu kutoa mafunzo kwa wafanyakazi waliohitimu na usaidizi wa mikopo kwa Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda (kwa ushirikiano wa Paul-Ehrlich-Institute na kwa ushirikiano wa karibu na washirika wa Ulaya).
Juhudi za pamoja ni mchango muhimu katika kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya za hali ya juu, nafuu barani Afrika na kuimarisha utayari wa janga la bara hilo.
Iwapo vikwazo vilivyotolewa na ujerumani kwa Rwanda vitatekelezwa huenda shughuli hizi zikatatizika au kukwama.
Kama sehemu ya mazungumzo, Ujerumani na Rwanda pia zilikubali kupanua mfumo wa hifadhi ya jamii kupitia mchango wa sekta ya ufadhili wa bajeti.
Lakini je, Rwanda Rwanda yenyewe inaseje kuhusu vikwazo hivi?
Rwanda imekuwa ikizituhumu nchi za Magharibi kwa vikwazo hivi ikivitaja kuwekwa bila kuzingatia hali halisi ya mzozo wenyewe na usalama wa mipaka na watu wake.
Msemaji wa Serikali ya Rwanda, Yolande Makolo, alisema vikwazo hivyo havina msingi wowote na kusisitiza kwamba jumuiya ya kimataifa inapaswa kuunga mkono juhudi za kisiasa za mataifa ya kikanda kutafuta suluhu badala ya hatua alizozitaja kuwa “za kukatisha tamaa.”
Aliongeza kuwa vikwazo haviwezi kuwa suluhisho la tatizo la muda mrefu mwashariki mwa DRC,na kama vikwazo vingetatua matatizo hayo ,eneo lingekuwa na amani miaka mingi iliyopita.
Rwanda inayashutumu mataifa hayo ya Magharibi kwa kwa upendeleo kwa serikali ya Kinshasa huku wakipuuza usalama wa Rwanda na watu wake kwa msalahi yao ya madini ya DRC.
‘Hakuna jipya’

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES
Si mara ya kwanza kwa Rwanda kuwekewa vikwazo na nchi za Magharibi kwa kuhusishwa na DRC
Baadhi ya Wanyarwanda wanaojibu kuhusu vikwazo dhidi ya nchi yao kupitia mitandao ya kijamii, hakuna jipya kwani miaka ya 2000, baadhi ya nchi hizo ziliiwekea Rwanda vikwazo ilipodaiwa kuingia ndani ya DRC kuwasaka wanamgambo wa Kihutu wa kikundi la FDLR wanaoendesha mapambano dhidi ya utawala wa Kigali, na baadaye kurejesha ushirikiano na serikali ya Rwanda.
Akizungumza katika mkutano wa kimataifa jijini Kigali, Rais wa Rwanda Paul Kagame alisema.
”Rwanda imekuwa peke yake, tumeonja (hali hii , na hatutishi na uwezekano kwamba wakati mmoja tutakuwa peke yetu tena. Kwa hiyo kila mara tunapaswa kujiandaa, na Tumezoea kufanya kazi katika mazingira mabaya zaidi ambapo kiasi kwamba wakati mmoja tutaachwa peke yetu.. Tukiachwa peke yetu tutaikabili hali na tutaishi hata vizuri zaidi kuliko ilivyokuwa awali”
Ndani na nje ya Rwanda tayari baadhi ya watu na makundi wakiwemo wasanii wameanza kuonyesha mshikamano na Rais Kagame kufuatia kutolewa kwa kutangazwa kusitishwa kwa misaada ya kimataifa kwa Rwanda.
”Tulikumwe” ( ikimaanisha -Tupo pamoja ), ni neno linalosikika kwenye baadhi ya nyimbo za Kinyarwanda na kushuhudiwa kwenye mitandao ya kijamii, kuonyesha mshikamano na utawala wa Kigali katika kukabiliana na tuhuma na kusitishwa kwa misaada ya kigeni kwa Rwanda.
Hata hivyo, swali linabaki: Je, hatua na juhudi hizi zinatosha kuifanya Rwanda ijiendeshe bila misaada ya wafadhili, au itabidi itafute njia mbadala za ufadhili?