Mzozo wa DRC: M23 yakabidhi ‘wanachama wa FDLR’ kwa Rwanda, huku serikali ya Congo ikikanusha

Jeshi la Rwanda (RDF) linasema limekabidhiwa kundi la wapiganaji wa FDLR linalopigana na serikali ya Kigali, lenye uhusiano na mauaji ya kimbari ya Rwanda ya mwaka 1994.
RDF inasema kuwa wapiganaji hao walikamatwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na waasi wa M23 ambao wamekuwa wakiteka maeneo ya nchi hiyo kwa muda mrefu.
Serikali ya Congo inakanusha taarifa hizi, ikisema ni upotoshaji wa Rwanda “ili kuhalalisha uvamizi wao katika sehemu ya nchi yetu”.
Taarifa iliyotolewa jana na jeshi la Rwanda inaonyesha orodha ya watu 14 na picha za video za watu inaosema kuwa ni wapiganaji wa FDLR ambao M23 iliwakabidhi kwa serikali ya nchi hiyo jana, Jumamosi, kwenye mpaka wa Grande Barriere wilayani Rubavu, huku Brigedia Jenerali Jean-Baptiste Gakwerere akiwa kinara wa orodha hiyo.

CHANZO CHA PICHA, THE NEW TIMES RWANDA
Vyombo vya habari vinasema kuwa afisa huyo mkuu wa kijeshi alihusika katika mauaji dhidi ya Watutsi karibu na mji wa Butare nchini Rwanda wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka 1994.
Katika taarifa hii, jeshi la Rwanda linasema kuwa taarifa za awali zinaonyesha kuwa “waliokamatwa walikuwa wakifanya kazi kwa muda na jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wapiganaji wa Wazalendo (wapiganaji wa serikali ya DRC) na vikosi vya SADC [SAMIDRC]”.
Jeshi la Rwanda pia linasema kuwa “baadhi ya wapiganaji wa FDLR wanasemekana kuhamia Walikale, Lubero, na Mwenga, huku wengine wakiwa bado wamejificha katika maeneo yanayodhibitiwa na M23”.

Jeshi la Congo, FARDC, linasema hii ni “njama iliyopangwa kudhoofisha vikosi vyetu na vya SADC”.