Wafahamu wanamgambo ‘wanaochochea uhasama’ baina ya DRC na Rwanda

Wafahamu wanamgambo ‘wanaochochea uhasama’ baina ya DRC na Rwanda

Kama umekuwa ukifuatilia mzozo unaoendelea wa DRC, bila shaka umesikia herufi FDLR zikitajwa mara kwa mara hasa Rwanda inapohusika . FDRL ni kifupi cha maneno ya Kifaransa (Forces démocratiques de libération du Rwanda), ikimaanisha, Jeshi la Ukombozi wa Rwanda), linalotuhumiwa na Rwanda kuhatarisha usalama wake na hata kupanga kuung’oa mamlakani utawala wa Kigali.

Licha ya kwamba si mara ya kwanza kwa kundi hili kutajwa katika mzozo wa Kongo, halijawa maarufu sana hapo awali kama sasa kutokana na mzozo wa mashariki mwa Kongo kugubikwa na machafuko yanayotekelezwa na vikundi mbalimbali vya wapiganaji, FDLR wakimwemo.

Hata hivyo katika mzozo unaoendelea, kundi la FDLR limesikika sana hususani katika kauli kali za Rais wa Rwanda Paul Kagame, alipoishutumu serikali ya Kinshasa kuwaunga mkono wapiganaji hao na mamluki ili kuung’oa utawala wake mamlakani.

Lakini Je, FDLR ni akina nani hasa ?

g

CHANZO CHA PICHA, AFP

Maelezo ya picha, Wapiganaji wakiwa katika msitu wa Congo. Kundi la FDLR limekuwa likifanya mashambulizi likitokea katika maeneo ya misitu

Kundi la FDLR ni kundi linalohusishwa moja kwa moja na mauaji ya kimbari ya Mwaka 1994 yaliyosababisha vifo vya Wanyarwanda takribani milioni moja, wengi wao wakitoka katika jamii ya Watutsi. Wahutu wachache waliokuwa na msimamo wa kati pia waliuawa.

Baadhi ya wafuasi wa kundi hili walikuwa wanajeshi wa zamani wa Rwanda ( X-FAR ) na wanamgambo wa serikali hiyo, maarufu kama Interahamwe waliopigana na vikosi vya Rwandan Partiotic Front (RPF- Inkotanyi), jeshi lililokuwa la wapiganaji wakimbizi wa Rwanda waliokuwa uhamishoni.

Jeshi la RPF ambalo liliongozwa na rais wa sasa wa Rwanda Paul Kagame, lilipata ushindi katika vita hivyo mwaka 1994 na kuwalazimisha wanajeshi wa zamani wa Rwanda na wanamgambo wa Interahamwe kukimbilia katika Zaire (DRC ya sasa), huku baadhi yao wakichangamana na raia wakimbizi na wengine wakijificha katika misitu ya Kongo na kuanzisha uasi na kutekeleza ukatili na mauaji dhidi ya raia wa Kongo na kuwashambulia ndani ya mipaka ya Rwanda.

Mnamo mwaka 2000, kundi la FDLR liliundwa rasmi na baadhi ya wanajeshi hawa wa zamani wa Rwanda, wanamgambo wa Interahamwe pamoja na makundi mengine madogo ya wapiganaji wa Kihutu.

Tangu wakati huo kundi la FDLR limekuwa likitekeleza maasi kama vile ubakaji wa watoto na wanawake pamoja na mauaji ya kikatili ndani ya DRC .

FDLR pia imekuwa ikifaya mashambulizi ndani ya mipaka ya Rwanda, hayo ni pamoja na yale waliyoyafanya katika msitu wa Mbuga ya Wanyama ya Virunga, mwaka 1998 ambapo watu zaidi ya 10 waliuawa katika mji wa Gisenyi uliopo mpakani mwa Rwanda na DRC na yale waliyoyafanya katika wilaya ya Nyaruguru Juni 2018, eneo la Nyungwe, na Wilaya ya Nyamagabe Disemba 2018.

Wafuasi wa kundi hili wamekuwa wakisakwa na mahakama ya kimataifa kwa ajili ya mauaji ya kimbari ya Rwanda kujibu mashtaka ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, huku Marekani ikilitaja kundi hili kuwa la ugaidi kutokana na ukatili na mauji yanayotekelezwa na wafuasi wake.

‘FDLR kiini cha mzozo kati ya DRC na Rwanda’

h

CHANZO CHA PICHA, AFP

Maelezo ya picha, Kundi la FDLR limeshutumiwa kwa kufanya ukatili dhidi ya raia wa Kongo na kushambulia raia wa Rwanda wanaoishi katika maeneo ya mpaka wa Rwanda na DRC

Rwanda mekuwa ikiishutumu serikali ya Kinshasa kushirikiana na kuwaingiza baadhi ya wapiganaji wa FDLR ndani ya jeshi lake la FRDC kwa njama za kuitoa mamlakani serikali ya Rwanda, shutuma ambazo DRC inakanusha.

Ripoti za Monusco, Umoja wa Mataifa na mashirika ya haki za binadamu zimekuwa zikiwashutumu wafuasi wa kundi hili kutekeleza mauaji, kupora maliasili za Congo, ubakaji na kuwaingiza watoto jeshini.

Katika ripoti zake kuhusu uhalifu na mauaji DRC, Shikrika la hali za binadamu la Human Rights Watch limelishutumu kundi la FDLR mara kwa mara kwa kutekeleza maasi likiungwa mkono na jeshi la DRC.

Katika ripoti yake mwaka 2022, Human Rights Watch ilisema ”ilipata taarifa za kuaminika kwamba wanajeshi wa Congo kutoka kikosi cha 3411 cha Tokolonga walitoa zaidi ya masanduku kumi na mbili ya risasi kwa wapiganaji wa FDLR huko Kazaroho, moja ya ngome zao katika Hifadhi ya Taifa ya Virunga, Julai 21.

” Wapiganaji wa FDLR wamewaua mamia ya raia kwa miaka mingi mashariki mwa Kongo, wakati fulani waliwakatakata hadi kufa kwa mapanga au majembe, au kuwachoma majumbani mwao. Wapiganaji hao wamefanya ubakaji usiohesabika na vitendo vingine vya ukatili wa kingono,” ilielezea ripoti hiyo.

Wenyeji katika Maeneo ya Mashariki mwa DRC wanashutumu jeshi la Kongo kwa kushirikiana nao, na kuwaacha wenyeji wakiishi na kujitafutia riziki hatarini.

“Wakati mmoja, [FDLR] walikuja kuchoma vijiji … zaidi ya nyumba 200,” alisema Eric Kambale, kasisi mwanafunzi katika parokia ya Luofu…Watu waliungua ndani. Jeshi la Congo lilikuwa umbali wa kilomita moja wakati hayo yakitokea.”

Bwana Kambale anasema watu wa Luofu waliishi chini ya tishio la vita vya mara kwa mara hadi majeshi ya Umoja wa Mataifa yalipodhibiti tena eneo hilo mwaka 2010.

‘Hatukatai kuwa FDLR ipo’

g

CHANZO CHA PICHA, PATRICK MUYAYA/X

Maelezo ya picha, Patrick Muyaya alisema ni lazima DRC iondoe “sababu zote ambazo Rwanda inatoa ili kuondoa wanajeshi wake katika nchi yetu,” ikiwa ni pamoja na kuliangamiza kundi la FDLR linalopigana na serikali ya Rwanda.

Serikali ya Kinshasa haikani kuwa wapiganaji hawa wanaoendesha harakati zao katika misitu ya nchi hiyo ni tisho kwa usalama wa Rwanda.

Katika mazungumzo ya amani ya Luanda yaliyofanyika Oktoba 2024, Msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Patrick Muyaya alisema ni lazima DRC iondoe “sababu zote ambazo Rwanda inatoa ili kuondoa wanajeshi wake katika nchi yetu,” ikiwa ni pamoja na kuliangamiza kundi la FDLR linalopigana na serikali ya Rwanda.

Mambo mawili muhimu ya mkataba wa amani wa Luanda unaojadiliwa hivi sasa ni “kuwaangamiza FDLR”, na Rwanda “kusitisha operesheni za kijeshi / kuacha hatua za kujihami”, alisema.

Katika mahojiano na BBC, Patrick Muyaya alisema: “Hatukuwahi kusema kwamba [FDLR] haipo, kuna mabaki yake ambayo hayajaangamizwa na yanasababisha tatizo la usalama kwa Rwanda, kama wanavyodai. Ni lazima tutatue hilo pia”.

Alipoulizwa awali na BBC iwapo serikali ya DRC iko tayari kuwasambaratisha FDLR, Patrick Muyaya alisema kuwa serikali yao iko tayari kuondoa visingizio vyote vinavyotolewa na serikali ya Rwanda.

Mwishoni wa mwezi Septemba mwaka jana , kulikuwa na ripoti za mashambulizi ya jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo “yakilenga kumuua Jenerali Pacifique Ntawunguka almaarufu “Omega”, kamanda wa kijeshi wa FDLR, kulingana na ripoti ya Shirika la Ujasusi la Afrika.

Wakati huo, msemaji wa FDLR aliiambia BBC kwamba ni kweli wameshambuliwa, akisema kwamba mashambulizi hayo “yaliendana na yale yaliyojadiliwa huko Luanda ili kulitokomeza FDLR”, lakini akasema kwamba wanaowashambulia ni “vikosi vya Rwanda na washirika katika vikosi vya FARDC”, ukweli ambao BBC haikuweza kupata uthibitisho kutoka kwa vyanzo huru.

Patrick Muyaya aliiambia BBC: “Hatukuwahi kusema kwamba [FDLR] haipo, kuna mabaki yake ambayo hayajaangamizwa na yanasababisha tatizo la usalama kwa Rwanda, kama wanavyodai.”

“Wanachama wa FDLR waliobaki sio sababu kubwa ya Rwanda kuendelea kuishambulia DRC , ndiyo maana tulikubali kufanya kazi ya kuwaangamiza waliobaki DRC kwasababu watu hawa wanafanya madhara makubwa kwa watu wa Congo kuliko wanavyowafanyia Rwanda, ndiyo maana tulikubali kumaliza tatizo hili,” alisema Muyaya.

Kwa Rwanda ‘FDLR ni itikadi ya mauaji ya kimbari’

g

CHANZO CHA PICHA, MINISTRY OF FOREIGN AFFAIRS/RWANDA

Maelezo ya picha, Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe anasema “FDLR sio idadi ya watu tu, si jeshi tu, ni itikadi ya mauaji ya kimbari…”

Mamlaka ya Rwanda inalielezea kundi la FDLR kama “kundi la kigaidi la mauaji ya kimbari ambalo linaleta tishio kubwa kwa Rwanda,” na inashutumu serikali ya Kinshasa na jeshi lake kwa kushirikiana na kundi hilo kuleta ukosefu wa usalama. Kinshasa pia imekanusha hili.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Rwanda Olivier Nduhungirehe alisema kuwa ni muhimu kwa serikali ya Kongo kuwa na nia ya kulitokomeza kundi hilo “kwasababu ndilo linaloleta matatizo katika ukanda huu”, aliiambia Rwanda televisheni katika mahojiano kuhusu mzozo wa DRC.

“FDLR sio idadi ya watu tu, si jeshi tu, ni itikadi ya mauaji ya kimbari ambayo imeenea katika kanda nzima na katika vikundi vingine vyote vinavyofanya kazi pamoja kama Wazalendo [Wanamgambo wa serikali ya DRC],” alieleza Nduhungirehe.

Rwanda inalishutumu kundi la FDLR kwa kushirikiana na jeshi la Congo kuwatesa na kuwauwa Watutsi wa Mashariki mwa Congo kutoka kabla la Banyamulenge, kwa lengo la kuwafukuza ili “warudi kwao Rwanda,” na matokeo yake kulazimisha maelfu yao kuwa wakimbizi ndani na nje ya nchi.

Rwanda imekataa wito wa mazungumzo na FDLR, ikiwataja kuwa ni maadui wa nchi wanaotaka kurejea Rwanda kutekeleza mauaji mengine ya kimbari. Japo Rwanda inakanusha kutuma wanajeshi wake kupambana bega kwa bega na wanamgambo wa M23 ndani ya DRC, baadhi ya vyanzo vinaaminini kuwa Rwanda inawatumia wanamgambo wa M23 ili kiupa presha serikali ya Kinshasa kufanya mazungumzo ambayo hatima yake itajumuisha kumalizwa kwa kundi la FDLR.

‘Juhudi za kuhamasisha FDLR kurejea Rwanda’

g

CHANZO CHA PICHA, MONUSCO

Maelezo ya picha, Vikosi vya Umoja wa Mataifa ulidondosha vijikaratasi hivi vya kuwashawishi FDLR kuwa ni salama kurejea Rwanda

Baada ya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994, Rwanda ilianzisha tume maalum ya kuwahamasisha Wanyarwanda waliokimbilia uhamishoni kurejea nyumbani. Baadhi walirejea na walioshtakiwa kwa mauaji ya kimbali walihukumiwa chini ya mfumo wa mahakama za jadi maarufu kama Gacaca na wengine kusamehewa na kurejea katika jamii zao.

Wengi waliorejea nyumbani walikuwa ni raia, wanajeshi wa vyeo vya chini na waliokuwa wanamgambo wa Interahamwe [wanamgambo wa serikali ya Juvenari Habyarimana waliotekeleza mauaji ya kimabari dhidi ya Watutsi mwaka 1994)

Lakini maafisa wa ngazi ya juu wa kisiasa na kijeshi wamebaki DRC zamani ikiitwa Zaire na kuendeleza harakati za kijeshi na mapigano dhidi ya Watutsi wa Congo wanaounda kundi la M23.

Mwaka 2014 pia kikosi cha walinda amani cha Umoja wa Mataifa MONUSCO kilianzisha mpango wa kuwahamasisha wapiganaji wa FDLR kurejea nyumbani.

Monusco ilianzisha vituo vya redio vinavyohamishika katika maeneo ya mbali, ikitangaza ujumbe wa kutia moyo na hadithi za mafanikio kutoka kwa wapiganaji wa FDLR walioamua kurejea nchini Rwanda.

Aidha ilitoa nambari zake za simu kwenye redio, na katika vipeperushi vinavyorushwa kutoka kwa helikopta za Umoja wa Mataifa katika maeneo ya waasi .

Timu za kuwachukua kutoka maeneo ya msituni zilielezea mahala pa kukutana nao kwa siri na kuwatoa kabla ya makamanda wao kugundua mipango yao, ilieleza Monusco katika mazungumzo na BBC. Hata hivyo mipango hii kwasasa imekwama kutokana na usalama mbaya katika maeno ya mashariki mwa Kongo.

Je FDLR wanaweza kurudi Rwanda?

g

CHANZO CHA PICHA, SADC

Maelezo ya picha, Juhudi za viongozi wa kikanda barani Afrika za kuutatua mzozo wa sasa wa DRC zimekwama

Wakati juhudi za Angola, SADC pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki zikiendelea kutafuta amani bado kuna tofauti za kimawazo kati ya pande hizo mbili katika matamshi ya viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda kuhusu suala la FDLR.

Kulingana na mchambuzi wa masuala ya Afrika Ezekiel Kamwaga njia pekee ya kufanikisha FDLR kurejea Rwanda na hatimaye kuchukuliwa hatua zozote zile ni kupitia mazungumzo: ” Wanamgambo wa FDLR hawawezi kurudi Rwanda kwasababu mpaka saasa hakuna mazungumzo au majadiliano ambayo yameshafanka ya kuwaruhusu kurejea Rwanda, na kuwaruhusu wao wawe sehemu ya kuijenga Rwanda mpya. Kwa hiyo mpaka sasa hivi wao wanaonekana kama watu waliofanya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ingawa ni kitu kigumu.”

”Mara kadhaa Rais Kagame amekataa kuzungumza na FDLR kwahiyo jambo hili litaendela miaka na miaka. Ni lazima ifike wakati mamlaka za Rwanda zikubali kufanya mazungumzo na FDLR kupitia usuluhusho ambalo pande mbili zitakubaliana nao” anaeleza Kamwaga.

Akizungumzia kuhusu uwezekano wa kuzungumza na FDLR, Rais wa Rwanda Paul Kagame: “Tutakachofanya ni kuwafungulia milango [mpakani],” Kagame alisema. “Wale wanaotaka kuja wanakaribishwa. Wale wanaotaka kubaki, ni chaguo lao. Na wale wanaotaka kuendelea kupigana wanaweza kufanya hivyo.”

Vita vya Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo vimesababisha zaidi ya mamilioni ya watu kuyahama makazi yao katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, na kuwaua idadi isiyojulikana ya raia, na kuvuruga biashara na biashara kati ya Rwanda na DRC.

Matokeo ya mzozo huu ni makubwa kwa maisha ya raia wa kawaida, ambao sasa wana matumaini tu katika juhudi za amani kurejesha amani ambazo kwa sasa zimekwama.

picha, Wapiganaji wa FDLR wamekuwa wakiendeleza vitendo vya ukatili na mauaji DRC na Rwanda

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *