Jinsi uhusiano na Rwanda unavyochochea ubaguzi dhidi ya Watutsi DR Congo

Kundi la waasi la M23 linaloongozwa na Watutsi, limeendelea kufanya uharibifu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, na kuteka majiji na miji muhimu katika uasi wa kumwaga damu.
Kiini cha uasi wao ni madai kwamba Watutsi wanaoishi DR Congo wananyanyaswa.
Serikali nyingi za kimataifa zinasema katika vita vyao wanavyodai kuwa ni dhidi ya ubaguzi, waasi hao wamefanya ukatili usiohalalishika. Umoja wa Mataifa na Marekani, kwa mfano, zimewawekea vikwazo viongozi wa M23 kwa tuhuma za uhalifu wa kivita, kama vile unyanyasaji wa kingono na mauaji ya raia.
Pia baadhi ya wachambuzi wa kikanda wanasema, badala ya kuwatetea Watutsi, M23 – na Rwanda, ambayo inawaunga mkono waasi hao – kimsingi wanalenga kunyonya utajiri wa madini wa mashariki.
Inafaa pia kuzingatia kwamba Watutsi wengi wa Congo hawaungi mkono vitendo vinavyofanywa na waasi kwa jina lao.
Licha ya hayo yote, wataalamu wa Umoja wa Mataifa wamerikodi ubaguzi wa miongo kadhaa dhidi ya Watutsi wa Congo na Banyamulenge – jamii ya wachache yenye uhusiano na Watutsi.
Ubaguzi huo unaanzia kwenye mauaji ya kikabila, ubaguzi wa mahali pa kazi na matamshi ya chuki kutoka kwa wanasiasa.
Msingi wa ubaguzi huu ni dhana kwamba Watutsi wa Congo na Banyamulenge ni wageni – au kama mtalaamu wa jamii ya Banyamulenge, Delphin R Ntanyoma alivyoandika – “wageni katika nchi yao wenyewe.”
Historia ya Banyamulenge na Watutsi
Kabila la Watutsi mara nyingi linahusishwa na Rwanda, kwani huko ndiko Watutsi wengi wanako ishi. Kwa upande wa Banyamulenge, wanahistoria wengi wanaichukulia jamii hiyo kuwa ni ya Watutsi kutoka Rwanda na Burundi ya sasa, huku wengine wakisema ni walowezi waliohamia mapema wakitokea nchi zinazoitwa Uganda na Tanzania kwa sasa.
Mtazamo wa kwamba watu hawa ni “wa kigeni” unaweza kuwa na matokeo mabaya. Bukuru Muhuzi, mtafiti na mwanauchumi mwenye umri wa miaka 36 kutoka eneo la Mwenga huko Kivu Kusini, anasema, mjomba wake na mtoto wa babake waliuawa na wanajeshi wa Congo na wanamgambo wa eneo hilo kwa kuwa ni Banyamulenge.
Wanajeshi wa Congo hawakujibu ombi la BBC la kutoa maoni yao.
Bw Muhuzi anasema familia yake imeishi katika Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo kwa vizazi vingi na anatamani “ulimwengu ujue kinachoendelea” kwa jamii yake.
Muragwa Cheez Bienvenue, mwanaharakati anayejitambulisha kama Mtutsi na Banyamulenge, anasema aliwahi kulengwa na wafanyakazi wa uwanja wa ndege wa jiji la Bukavu.
“Nilizuiliwa – waliniambia nafanana na [Rais wa Rwanda] Kagame na waliniamuru nilipe karibu dola za kimarekani 150 (£120) ili nisalimike na kifungo,” ameiambia BBC, akiongeza kwamba anaunga mkono harakati za M23.
Kabla ya ukoloni, sehemu ya eneo ambalo sasa ni DR Congo lilikuwa chini ya mfalme wa Rwanda. Watutsi waliishi miongoni mwa makabila mengine katika eneo hili tangu karne ya 19.
Lakini mataifa ya kikoloni yalipotengeneza mipaka barani Afrika, wale wote wanaoishi katika ufalme wa Rwanda waligawanyika kati ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na Rwanda ya sasa.
Watutsi wengine walihamia DR Congo. Kuanzia 1941 hadi 1960, utawala wa kikoloni wa Ubelgiji uliwapeleka baadhi ya Watutsi katika mpaka ili kufanya kazi kwenye mashamba makubwa na mwishoni mwa miaka ya 1950 wakimbizi wa Kitutsi walikimbia ghasia za kikabila nchini Rwanda na Burundi na kwenda Congo. Watutsi waliongezeka Congo mwaka 1994 – mwaka wa mauaji ya kimbari ya Rwanda.
Ushahidi wa Ubaguzi
1972, Rais wa wakati huo Mobutu Sese Seko alitoa uraia kwa makabila yote ambayo yalitoka Rwanda au Burundi, mradi tu yalikuwepo katika eneo la Congo kabla ya 1950.
Lakini miaka tisa baadaye, bunge liliondoa haki hizi na Watutsi wengi, Banyamulenge na watu kutoka makundi mengine madogo “waliachwa bila utaifa,” inabainisha ripoti ya Umoja wa Mataifa.
Katika miaka ya 90, Watutsi na Banyamulenge walikabiliwa na mauaji. Kwa mfano, ripoti ya Umoja wa Mataifa inasema mwaka 1996 jeshi la Congo lilisaidia makundi yenye silaha kuua karibu watu 300 wa Banyamulenge katika mji wa Baraka.
Waraka huo pia unasema Watutsi “wengi” na Banyamulengele walipoteza kazi na kukabiliwa na ubaguzi na vitisho mwaka 1993.
Leo hii, katiba inavihesabu vikundi vya Watutsi na Banyamulenge kuwa ni Wacongo na watu wachache kutoka jamii hizi wanashikilia nyadhifa za juu za kijeshi na utawala. Jenerali Pacifique Masunzu, mtu anayeongoza mapambano dhidi ya M23 kama kamanda wa Kivu Kaskazini na Kusini, ni Banyamulenge.
Lakini bado kuna ushahidi mkubwa wa ubaguzi. Mwaka 2022, wataalamu wa Umoja wa Mataifa, walisema huko Kivu Kusini, Banyamulenge wanaonekana kama waharibifu katika jamii za jirani. Mitazamo hii huchochea “chuki, ubaguzi, uadui na vurugu,” walisema wataalamu.
Pia kumekuwa na taarifa za hivi karibuni za kuuawa kwa wanajeshi wa Watutsi na Banyamulenge katika jeshi la Congo. Kulingana na Human Rights Watch. Kundi la watu lilimuua afisa wa kijeshi wa Banyamulenge mwaka 2023 “katika kesi inayoonekana kuwa ni ya chuki ya kikabila.”
Wanasiasa – wa zamani na wa sasa – pia wamesukuma hisia za kibaguzi. Martin Fayulu, kiongozi wa upinzani ambaye aligombea urais mara mbili, amekanusha mara kwa mara kwamba Banyamulenge ni kabila la Congo, akiwaita “wavamizi.”
Serikali ya Congo inakiri uwepo wa aina fulani ya ubaguzi. Mapema mwaka huu Rais Felix Tshisekedi alisema “amechoshwa” na kauli za chuki dhidi ya Banyamulenge na kauli kama hizo huipa Rwanda kisingizio cha kuivamia DR Congo.
Msemaji wa serikali Patrick Muyaya aliambia BBC: “Tuna makabila 450 na kuna mizozo kati ya baadhi yao katika maeneo mengi ya nchi. Msimamo wa serikali ni kupinga aina yoyote ya ubaguzi au matamshi ya chuki dhidi ya jamii nyingine.”
Kwa upande mwingine, Bw Bienvenue aliambia BBC anaamini kabila lake linabaguliwa, akitoa mfano dadake alitimuliwa kazini baada ya kuambiwa “anaonekana kama jasusi wa Rwanda.”
Licha ya familia yake kuishi katika hilo kwa karne nyingi.
“Banyamulenge wamekuwa hapa tangu Congo ilipoanza kuwa Congo!” anasisitiza.