‘Wezi walipora misalaba kwenye kaburi la mwanangu, mama na ndugu zangu’

Hatua kwa hatua katika Makaburi ya Manispaa ya Morogoro nchini Tanzania kumeshuhudiwa kaburi moja baada ya jingine yakiwa yameharibiwa.
Zaidi ya makaburi 250 tuliyoyashuhudia kwenye eneo moja la Kola yalilengwa huku mengine mengi nayo yakiwa hayana misalaba.
Uhalifu huu unadaiwa kufanyika zaidi usiku wakati wale wanaofanya kazi kwenye makaburi hayo wanapokuwa wameondoka.
Familia zimeachwa na majonzi makubwa huku maeneo hayo yakiharibiwa vibaya, jambo ambalo limezua hasira miongoni mwa watu kwenye jamii.
“Hili ni kaburi la mwanangu wa nne, alifariki mwaka 1997 nikamzika hapa lakini baada ya kumzika miaka ikapita, nikakuta msalaba haupo…
“…Kaburi la mama yangu mzazi liko limengolewa msalaba, ndugu zangu kama 10 waliozikwa hapa napo wamevunja na misalaba hii inadaiwa kuuzwa kama vyuma chakavu,” anaeleza Pudensiana Chumbi mkazi wa Morogoro nchini Tanzania.
Uharibiru kwenye sehemu ya makaburi umeripotiwa kuwa changamoto kubwa katika mji huo ambao uko takribani kilometa 100 kutoka jiji la kibiashara la Dar es Salaam.
Pudensiana anasema kuwa kila anayefika kuangalia kaburi la mpendwa wake, anaondoka na manunguniko kutokana na uharibufu anaoukuta.
Anasema, “Kila mtu ana manunguniko na masikitiko. Hii ni laana kabisa, misalaba wanaiba na kuuza, ukiweka mwingine wanaiba na hata sasa ukiweka tiles (vigae) wanaiba…
“… Na ndio maana kabla hujaondoka makaburini kuna vijana watakuambia mama sisi tupo, tupe chochote tulinde kaburi kwa siku moja ili wasingofoe ’tiles’ ziweze kukauka,” anaeleza.
Hata hivyo, Serikali imedai kujipanga kuweka ulinzi katika eneo hilo.
BBC ilifika katika eneo hilo na kushuhudia uharibifu uliofanyika huku ikielezwa kuwa uvunjaji hufanyika majira ya usiku.
Takwimu sahihi za makaburi yaliyotolewa misalaba haikuweza kufahamika mara moja lakini katika eneo moja BBC ilishuhudia makaburi zaidi ya 250 yakiwa yamengolewa misalaba.
Wauza vyuma chakavu watuhumiwa kuhusika

Augustine Remmy ambaye ni kaka wa Pudensiana anasema kuwa biashara ya vyuma ndiyo chanzo cha makaburi kuvunjwa.
“Sisi wengine, hilo suala limeshatukuta tayari. Kuna baadhi ya makaburi ya ndugu zangu ninayoyaona na wewe sasa hivi hayana misalaba. Misalaba iliwekwa lakini watu wa chuma chakavu wakaja wakachukua na kwenda kupima. Kwa kweli kwa eneo hili ni tatizo sugu,” anasema na kuongeza kuwa inamuumiza sana.
Remmy anasema kuwa kwa mtazamo wake, maeneo hayo yanapaswa kuheshimiwa. ” Inaumiza sana kwasababu maeneo kama haya yanayostahili heshima lakini unakuta matendo ya kihuni yanafanyika maeneo hayo, kwa kweli si vizuri.
Mawakala wa vyuma chakavu katika mkoa huo hununua vyuma kwa shilingi 700 hadi 870 (sawa dola za kimarekani 0.30) kwa kila kilo ya vyuma.
Hata hivyo wauzaji vyuma wanasema hao wananua nyuma mbalimbali isipokuwa hawachukui vile vinavyokana na miundombinu ya kama reli, madaraja na hata misalaba ya makaburi.
Izire Ramadhani, ambaye ni mfanyabiashara ya vyuma chakavu kwa miaka mingi anasema zamani walikuwa wananunua vyuma vya kila aina na misalaba ilikuwa ni mingi.
Ramadhani anasema “Kwangu hapa kwasasa ukiniletea msalaba nakupeleka polisi na tena kuwa kuna mtu mmoja tuliwahi kumpeleka polisi na badae akafungwa miaka mitatu na nusu jela.
“Baada ya matukio hayo, uhalifu huo ulipungua lakini sasa umerudi kwa kasi,” alisema.
Wadai wezi hufanya matukio usiku

Peter Mataba amekuwa akifanya shughuli za uchimbaji makaburi katika eneo hilo ambapo yeye anasema kuwa misalaba huvunjwa mida ya usiku.
Mataba anasema, “Tunaingia asubuhi, sisi tunatoka saa 12 jioni. Sasa tukishatoka sisi hapa kuna wengine wanaingiaa wanavunja makaburi.Misalaba imechukuliwaa mingi sana na changamoto ni kuwa hatutali huku hivyo misalaba huibiwa usiku.”
Dkt Ndimile Kilatu, Afisa Afya wa Manispaa ya Morogoro anasema kuwa tatizo hilo lipo na linachangiwa na kutokuwepo kwa walinzi katika eneo hilo.
Anasema, “Tatizo hili lipo na ofisi yetu imekutana na hili jambo mara kadhaa… Hatuna walinzi wa usiku na pia eneo halina fensi japo sio leo au kesho.”
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, BBC pia ilishuhudia eneo moja lenye uzio likiwa limengolewa milango ambayo yote ilikuwa ya chuma.
Viongozi wa dini walia na maadili
Steven Msigara, ambaye ni mchungaji wa Kanisa la Jesus Assembles of God, anasema kuwa mmonyoko wa maadili miongoni mwa vijana umechangia uhalifu kuongezeka kwenye jamii
Kiongozi huyo wa kiroho anasema, “Maadili ya vijana yamebadilika. Leo wanangoa mpaka misalaba ambayo ni kumbukumbu ya waliotangulia mbele za haki. Nafikiri wazazi wamelegea katika kusimamia maadili.”
Mamlaka zinaeleza kuwa hatua za kisheria ziliwahi kuchukuliwa

Dkt Ndimile Kilatu anasema kuwa baadhi ya watu waliokuwa wakingoa misalaba na kuuza kwenye vyuma chakavu walishachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kufikishwa mahakamani.
Dkt Kilatu anasema kuwa mwaka 2019 kulikuwa na kesi mahakamani na hukumu ilitoka kwa mujibu wa sheria. Sambamba anasema kuna watu wengine kadhaa waliwahi kufikishwa polisi kwa tuhuma za wizi wa misalaba.
Naye Naibu Waziri Mkuu wa Tanzania, Dotto Biteko alisema katika kukabiliana na uwepo wa vyuma chakavu vilivyopatikana kwa njia isiyo sahihi, serikali itaendelea kutekeleza sheria zake lakini pia kuwaelimisha wananchi kuhusu jambo hili.