Mzozo wa DRC: Congo yakiri kutekwa kwa Bukavu

Mzozo wa DRC: Congo yakiri kutekwa kwa Bukavu

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inasema Rwanda inapuuza wito wa kusitishwa kwa mapigano baada ya waasi wa M-23 kuuteka mji wa pili mashariki mwa nchi hiyo.

Waziri wa Mawasiliano Patrick Muyaya, alisema Rwanda inakiuka uadilifu wa eneo la DRC kwa nia ya kujitanua na bila kujali ukiukaji wa haki za binadamu unaoendelea.

Alisisitiza kuwa serikali yake inajitahidi kurejesha utulivu mjini Bukavu na kulinda mipaka yake.

Mvutano unazidi kuongezeka mashariki mwa DRC huku waasi wa M23 wakiungwa mkono na Rwanda wakipanua udhibiti wao katika miji muhimu.

Wanamgambo hao wameapa kuudhibiti mji wa Bukavu mashariki mwa Congo- ili kurejesha usalama baada ya vikosi vya jeshi la Congo kutoroka.

Kwa mujibu wa taarifa yao, ukosefu wa usalama na wizi wa kimabavu ulitokea baada ya jeshi la FARDC, FNDB, FDLR na wandani wao kuondoka, na kuwalazimu kuingilia kati kusaidia wakaazi.

Watu kadhaa walionekana wakiwalaki mitaani wakishangilia baada ya kundi hilo linaloungwa mkono na Rwanda kuingia eneo hilo bila pingamizi.

Mamlaka mjini Kinshasa hata hivyo inasema inafuatilia kwa karibu hali ya usalama katika Kivu Kusini, karibu maili elfu moja.

Bukavu ni mji wa pili kutekwa baada ya Goma kuangukia mikononi mwa waasi hao wiki chache zilizopita.

Upande wa serikali ya Congo wamekiri kuanguka kwao na kutekwa kwa mji wa pili mkubwa nchini humu ikiwaomba wakaazi wasalie nyumbani wasijipate katika makabiliano ya kijeshi.

Mataifa ya Umoja wa Afrika na Ulaya wameonya mzozo huo, ambao umesababisha maelfu ya watu kutoroka makazi huenda yakazua vita vya kikanda.

Wameeleza kuwa juhudi zao zimekubaliwa na wakaazi wa Bukavu na kwamba wanataka serikali ya Congo ianzishe mazungumzo ya maridhiano ili kutatua mgogoro na kudumisha amani nchini.

Pia wameitaka serikali kusitisha mapigano ya kijeshi ili kuwe na utulivu na amani.

Mkaazi mmoja wa Bukavu, ambaye jina lake limefichwa kwa sababu za kiusalama ameiambia BBC kuwa watu wengi bado wanahofia kutoka majumbani mwao kuendeleza shughuli za kawaida.

”Tangu jana vijana na watoto wamechukua silaha. Wanafyatua risasi kiholela na kuiba,” anasema.

”Asubuhi ya Jumapili M23 waliingia mjini na walilakiwa na watu, waliofurahia kuwaona.Haijulikani wanawaogopa ama ni kwasababu hakukuwa na mamlaka mjini humo.

”Eneo ninaloishi bado nasikia milio ya risasi ” anasema mwanamke huyo.

Ijumaa, wanamgambo wa M23 walidhibiti uwanja wa ndege wa Bukavu, ulio takriban kilomita 30 kaskazini mwa jiji, na kuanza kusonga polepole kuelekea katikati ya mji, ambao ni mji mkuu wa jimbo la Kivu kusini.

Gavana wa jimbo, Jean-Jacques Purusi Sadiki, alithibitisha kwa shirika la habari la Reuters kuwa wanamgambo walifika katikati ya mji wa Bukavu asubuhi ya Jumapili, akiongeza kuwa vikosi vya Congo vilijiondoa ili kuepuka mapigano katika eneo linaloishi watu wengi.

Hali ya usalama ilizidi kuwa tete Jumamosi, ambapo kuliripotiwa tukio la wafungwa kutoroka kutoka gereza kuu.

Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) lilisema kuwa ghala moja lililokuwa na takriban tani 7,000 za chakula liliporwa.

Bukavu, yenye wakaazi wapatao milioni mbili na iliyo katika ukingo kusini ya Ziwa Kivu, inapakana na Rwanda na ni kituo muhimu cha biashara ya madini.

Kuanguka kwa mji huu kunatokea ikiwa ni upanuzi mkubwa wa eneo la M23 tangu kuanza kwa uasi wao mpya mwishoni mwa mwaka 2021, na ni pigo kubwa kwa serikali ya Rais Félix Tshisekedi.

Msemaji wa serikali, Patrick Muyaya, alisema kuwa Rwanda inavunja uhuru wa kisheria wa DRC kwa matamanio ya upanuzi na ukiukaji wa haki za binadamu.

Serikali ya Congo inalaumu Rwanda kwa kueneza machafuko katika eneo hilo, ikiwa na askari wake nchini DRC, ili kunufaika na rasilimali zake asili, jambo ambalo Kigali linakanusha.

Rais Tshisekedi anataka Rais Paul Kagame wa Rwanda akabiliwe na vikwazo kutokana na machafuko haya, lakini Rais Kagame amekataa vitisho hivyo, akisisitiza kuwa kipaumbele cha Rwanda ni usalama wake.

Rais Kagame amekuwa akikasirishwa na kile anachoona kama kushindwa kwa mamlaka ya Congo kushughulikia kikundi cha waasi cha FLDR, kinachotishia usalama wa Rwanda.

FLDR inaundwa na baadhi ya wanamgambo wa kabila la Hutu waliohusika na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 nchini Rwanda, ambapo watu 800,000, wengi wao kutoka kabila la Tutsi, waliuawa kwa zaidi ya siku 100.

Wanamgambo wa Tutsi wa M23 walikusanyika kwenye Place de l’Indépendance katikati ya Bukavu Jumapili, ambapo mmoja wa makamanda wao, Bernard Byamungu, alionekana akizungumza na wakaazi na kujibu maswali yao kwa Kiswahili.

Aliwataka wanajeshi wa serikali “waliokimbilia kwenye nyumba” kujisalimisha na alilaumu wanajeshi waliokimbia kwa kueneza hofu kwa kuwapa silaha vijana wa mtaa, ambao walikuwa wameingia katika wimbi la uporaji.

Ramani ya DR Congo ikionyesha mji wa Goma na Bukavu
Maelezo ya picha, Ramani ya DR Congo ikionyesha mji wa Goma na Bukavu

Pia, M23 imewataka makundi ya kijamii na kisiasa yanayopinga utawala wa sasa kuungana nao katika mapambano ya kisiasa yanayolenga mabadiliko ya kikatiba na utawala mpya wa serikali.

Umoja wa Afrika (AU) -ambao umekuwa ukiendeleza vikao vyake nchini Ethiopia wikendi kwa mara nyingine iliwasihi kundi la M23 lijisalimishe.

”Sisi sote tumeingiwa na wasiwasi kutokana na vita vinayoendelea DRC ambavyo huenda vikachochea vita vya kikanda,” shirika la Reuters likinukuu kamishna wa usalama na amani wa AU Bankole Adeo akieleza.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *