Sam Nujoma: Mwanamapinduzi aliyeikomboa Namibia alifaliki

Sam Nujoma: Mwanamapinduzi aliyeikomboa Namibia alifaliki

Rais wa kwanza wa Namibia afariki akiwa na umri wa miaka 95, Rais huu, Sam Nujoma, amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95 katika mji mkuu wa Windhoek, kiongozi wa sasa wa nchi hiyo ametangaza.

Aliheshimika na kufahamika kama “Baba wa taifa” na ishara ya mapambano ya kuikomboa Namibia. Maisha ya Sam Nujoma yalikidhi matarajio ya mtu mwenye hadhi kama yake kwa njia tofauti.

Alipendwa na wengi kutokana na muonekano wake wa kuwa mchangamfu na mwenye tabasamu.

Alikuwa mtu wa watu, iwe ni wakati ambapo alivaa nguo za kukimbia na kujiunga na raia wakifanya mazoezi katika barabara ya Independence Avenue katika mji mkuu wa taifa hilo Windhoek, au wakati mwingine alipoamua kutotumia misafara rasmi ya magari.

Sasa, miongo minne baada ya kuiongoza Namibia katika vita vikali vya msituni dhidi ya serikali ya ubaguzi wa rangi ya Afrika Kusini hadi taifa hilo kupata uhuru, Nujoma amefariki akiwa na umri wa miaka 95.

Alifariki siku ya Jumamosi baada ya kulazwa hospitalini kwa muda wa wiki tatu alipokuwa akiugua, kwa mujibu wa tangazo la Rais Nangolo Mbumba, ambaye amesema kuwa kifo hicho “kimelitikisa” taifa.

Kupigania Uhuru

Shujaa huyu ambaye aliipa Namibia utambulisho wa kitaifa anaacha pengo ambalo ni wachache wanaoweza kulijaza.

Namibia, awali ikifahamika kama South West Africa, ilipitia mateso kwa miongo kadhaa ikiwemo uporaji na unyanyasaji wa kikoloni chini ya mikono ya wazungu kutoka bara Ulaya ambao walifika nchini humo kwa wingi mwanzoni mwa karne ya 20.

Kuanzia mwaka wa 1904, wakoloni wa Ujerumani waliua maelfu ya raia wa Namibia katika kile kinachofahamika kama “mauaji ya halaiki yaliyosahaulika” duniani.

Maafisa wa Ujerumani waliwatumia Waafrika weusi kama mfano wa kufanyia majaribio katika uhalifu wa kutisha ambao baadaye ulitekelezwa na Wanazi wakati wa mauaji ya Wayahudi maarufu kama ‘Holocaust’ katika vita vya pili vya dunia.

Namibia ilikuwa chini ya ukoloni wa Wajerumani kutoka 1884 hadi 1915, wakati Ujerumani ilipopoteza koloni hilo katika vita vya kwanza vya dunia.

Baada ya hapo Namibia ilikuwa chini ya utawala wa wazungu wa Afrika Kusini, ambao walitekeleza sheria zao za ubaguzi wa rangi nchini humo, na kuwanyima raia weusi wa Namibia haki zozote za kisiasa, pamoja na kuwanyima haki za kushiriki masuala ya kijamii na kiuchumi.

Kuanzishwa kwa sheria nyingi za ubaguzi wa rangi kulisababisha vita vya msituni kuzuka mwaka wa 1966, raia wa Namibia wakitafuta uhuru wa nchi yao.

Kufikia wakati huu, Nujoma alikuwa tayari anahusika katika vita dhidi ya utawala wa wazungu waliokuwa wachache nchini humo.

Alipenda kujiita “mtoto wa kwanza katika familia maskini ya wakulima” kutoka kijiji cha kaskazini cha Etunda ambapo alianza maisha ya kawaida, akiwa na elimu ndogo tu ya shule ya msingi.

Alimuoa Kovambo Theopoldine Katjimune na pamoja wakajaliwa kupata watoto wanne, akafanya kazi kwenye shirika la reli, akiwa na shauku kubwa ya kujiunga na siasa na alitamani kuona watu wake wakiwa huru kutokana na dhuluma na aibu ya ukoloni.

Msukumo wake ulitokana na hadithi za viongozi wa awali wa upinzani wa Namibia, kama vile Hendrik Witbooi, ambaye alipigana dhidi ya Wajerumani katika miaka ya 1880.

Kufikia 1959, Nujoma alikuwa mkuu wa shirika la Owamboland Peoples organisation, vuguvugu la kupigania uhuru ambalo lilikuwa mtangulizi wa chama cha Swapo.

Mwaka mmoja baadaye, akiwa na umri wa miaka 30, Nujoma alilazimishwa kukimbia nyumbani na kwenda uhamishoni. Akiwa hana hati ya kusafiria, alitumia ujanja wake na kuchukua hulka ya watu tofauti ili kuingia kwenye treni na ndege – akafanikiwa kuingia Zambia na Tanzania kabla ya kuelekea Afrika Magharibi.

Kwa usaidizi wa mamlaka za Liberia ambao tangu zamani waliunga mkono azma ya Wanamibia weusi kutaka uhuru wao, Nujoma alisafiri kwa ndege hadi New York na kuomba Umoja wa Mataifa kusaidia kuipa Namibia uhuru wake – lakini Afrika Kusini ilikataa kufanya hivyo.

Nujoma alitajwa kuwa “gaidi wa ki-Marxist” na viongozi wa wazungu wa Afrika Kusini kwa kuongoza vikosi vilivyopigana pamoja na vuguvugu la kupinga ubaguzi wa rangi, na kusababisha changamoto kubwa kwa utawala dhalimu katika nchi kadhaa za kusini mwa Afrika.

Akisaidiwa na wanajeshi wa Cuba waliokuwa wakipigana katika nchi jirani ya Angola, wapiganaji wa msituni wa Swapo walishambulia kambi za Afrika Kusini nchini Namibia.

Aliporejea kutoka uhamishoni, Nujoma alikamatwa tena na mamlaka za Afrika Kusini na kusafirishwa hadi Zambia miaka sita baadaye.

“Tulijua kwamba ni nguvu za kijeshi tu na uhamasishaji mkubwa wa kisiasa wa watu ambao ungeilazimisha Afrika Kusini kuondoka Namibia,” Nujoma alisimulia katika wasifu wake wa Where Others Wavered, uliochapishwa mwaka 2001.

Aliongoza vikosi vya Swapo kutoka uhamishoni, kabla ya kurejea nchini mwaka 1989, mwaka mmoja baada ya Afrika Kusini kukubali kuikabidhi Namibia uhuru wake.

Afrika Kusini ilikuwa ikitengwa zaidi kimataifa na gharama ya kijeshi ya kushiriki vita ilikuwa ikiongezeka. Hatimaye Namibia ilipata uhuru mwaka 1990 baada ya takriban miaka 25 ya vita.

Kujenga taifa

.

CHANZO CHA PICHA, AFP

Katika uchaguzi wa kwanza wa kidemokrasia nchini Namibia mwaka 1990, Swapo ilipata kura nyingi zaidi na Nujoma akawa rais wa kwanza wa nchi hiyo.

Nujoma alijali sana maslahi ya watoto, na alianzisha malipo ya kuwatunza yaliyowalazimu akina baba waliowatelekeza watoto wao kuchangia gharama za malezi.

Pia alitetea maendeleo ya wanawake, na kusaidia kubadilisha itikadi za mfumo dume ambazo ziliwafukuza wajane kutoka kwenye ardhi za familia mara tu waume zao walipopofariki.

Pia alihakikisha juhudi za maendeleo zinaungwa mkono na wafadhili wa kimataifa.

Nujoma alichaguliwa tena kwa mihula miwili zaidi mwaka 1994 na 1999 – alipokosolewa kwa kubadilisha katiba ili aweze kugombea muhula wa tatu madarakani.

Alipokosolewa kwa mtindo wake wa uongozi au kuhojiwa kuhusu vitendo vya hapo nyuma vya chama chake cha kisiasa, tabasamu lake pana liliweza kugeuka na kuwa mkali. Wakati mwingine angemnyooshea kidole yeyote aliyethubutu kuhoji au kukosoa waziwazi masuala hayo, na kuna wakati fulani ambao angerusha matusi.

Alichukia waziwazi mahusiano ya watu wa jinsia moja, lakini hakuwahi kufikia hatua ya kubadilisha katiba au sheria ili kuyafanya kuwa haramu.

Nujoma daima alithamini urafiki wake wa karibu na Robert Mugabe wa Zimbabwe, lakini kama rais wa Namibia aliepuka uchokozi wa hadharani dhidi ya wakosoaji wake.

Hata hivyo angetumia mifumo ya Swapo kutoa shinikizo kwa mwananchi wa kawaida kutii chama chake na pia kuruhusu chama hicho kutumia fedha za serikali ili kuhakikisha utawala wake unaendelea.

Alikuwa na uwezo mkubwa, ikiwemo kuamuru baraza lake la mawaziri la Nujoma kufikia maamuzi badala ya wote kushiriki mijadala ili kuamua jambo.

Alipoondoka uongozini mwaka 2005 na baadaye kama rais wa Swapo mwaka 2007, baada ya kuhudumu kama kiongozi wa chama hicho kwa miaka 47 – alikabidhi madaraka kwa mrithi wake, Hifikepunye Pohamba.

Hata baada ya kuondoka madarakani, Nujoma bado alikuwa na ushawishi mkubwa kwa maamuzi ya chama na serikali.

Hata hivyo mafanikio yake akiwa madarakani yako wazi, wananchi wengi wa Namibia wakimsifu kwa kuongoza nchi hiyo kujikita kwenye utawala wa kidemokrasia.

Tangu uhuru wake, Namibia imeonekana kuwa mojawapo ya mataifa yenye hadithi za mafanikio barani Afrika, kwasababu ya kuandaa chaguzi za mara kwa mara za amani na demokrasia.

Na, licha ya udhalilishaji na dhuluma za wakoloni weupe dhidi ya raia weusi wa Namibia, Nujoma alishikilia katiba ya nchi hiyo katika kulinda haki za kimsingi za Wanamibia wote bila kubagua kabila wala rangi yao.

Sera ya umoja wa kitaifa iliwashawishi wazungu nchini humo kusalia, na bado wanaendelea kutoa mchango mkubwa katika kilimo na sekta nyingine za kiuchumi.

Uwezo wa Nujoma wa kuunganisha taifa la watu milioni tatu – kutoka jamii 10 tofauti – ulimfanya kupendwa na wengi.

Kwa kutambua mafanikio yake makubwa, bunge la Namibia lilimpa hadhi rasmi ya “Baba Mwanzilishi wa taifa la Namibia” mwaka 2005. Pia alipata tuzo nyingi za kimataifa kama vile Tuzo ya Amani ya Lenin, Tuzo ya Amani ya Indira Gandhi na Tuzo ya Amani ya Ho Chi Minh.

Katika miaka yake ya mwisho, Nujoma hakuonekana sana hadharani, akipendelea kutumia wakati mwingi akijumuika na familia yake kubwa.

Anakumbukwa kwa haiba yake na maono yasiyoyumba – akiwa baba sio tu kwa familia yake bali kwa taifa zima.

Imetafsiriwa na Peter Mwangangi

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *