Jinsi mpango wa DRC kuwatumia mamluki wa kizungu vitani ulivyofeli
Imekuwa wiki ya kufedhehesha kwa karibu mamluki 300 wa Kiromania walioajiriwa kupigana upande wa jeshi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Kujisalimisha kwao kunafuatia shambulio la waasi katika mji wa mashariki wa Goma pia kumekatiza ndoto za wale waliojiandikisha kufanya kazi hiyo ili kupata pesa nyingi.
BBC imeona kandarasi zinazoonesha kuwa wanajeshi hao waliokodiwa walikuwa wakilipwa karibu $5,000 (£4,000) kwa mwezi, huku wanajeshi wa kawaida wakipata karibu $100, au wakati mwingine bila kulipwa.
Raia hao wa Romania walipewa kandarasi ya kusaidia jeshi kupambana na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ambao wanasema wanapigania kulinda haki za Watutsi wa kabila dogo la DR Congo.
Wakati mashambulizi ya Goma yalipoanza Jumapili usiku, Waromania walilazimika kukimbilia katika kambi ya walinda amani wa Umoja wa Mataifa.
“Waasi wa M23 waliungwa mkono na wanajeshi na zana za kisasa za kijeshi kutoka Rwanda na walifanikiwa kufika katika maeneo yetu karibu na mji wa Goma,” Constantin Timofti, alielezea kama mratibu wa kundi hilo, alikiambia kituo cha TVR cha Romania. siku ya Jumatatu.
“Jeshi la taifa liliacha kupigana na tukalazimika kuondoka.”
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Romania Andrei Țărnea aliiambia BBC kuwa mazungumzo “tata” yalifuata, ambayo yalishuhudia M23 ikiwakabidhi wapiganaji wa Romania, ambao waliwataja kama wafanyakazi wa serikali ya DR Congo kwenye misheni ya mafunzo ya jesh kwa Rwanda.
Goma inapakana na Rwanda, na mamluki hao walirekodiwa na waandishi wa habari walipokuwa wakivuka, wakijisalimisha kwa upekuzi.
Kabla hawajavuka, picha za simu zinaonesha kamanda wa M23, Willy Ngoma, akimkemea raia wa Romania kwa lugha ya Kifaransa, akimwambia akae chini, akunje miguu yake na kuweka mikono kichwani.
Alimuuliza juu ya mafunzo yake ya kijeshi, alikuwa na Jeshi la Kigeni la Ufaransa, Mromania huyo alijibu.
“Walikuajiri kwa mshahara wa $8,000 kwa mwezi, unakula vizuri,” Ngoma alifoka, akionesha tofauti kati ya malipo hayo na malipo ya askari wa jeshi la Congo.
“Tunapigania maisha yetu ya baadaye. Usije kufanya mchezo hapa,” alionya.
Haijabainika ni wapi Ngoma alipata kiasi hicho cha dola 8,000, lakini mkataba uliooneshwa kwa BBC na mamluki wa zamani wa Romania mwezi Oktoba ulieleza kuwa “malipo ya siri” kwa wafanyakazi wakuu yalianzia $5,000 kwa mwezi wakati wa kazi na $3,000 wakati wa likizo.
Makubaliano hayo yanaeleza “muda usiojulikana” wa huduma, na wakandarasi wamepangwa kuchukua mapumziko ya mwezi mmoja baada ya kila miezi mitatu ya kupelekwa.
Nilikuwa nimekutana na askari wa zamani wa mamluki katika mji mkuu wa Romania, Bucharest, ambako nilienda kuchunguza Asociatia RALF, ambayo kundi la wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema ni biashara ya Kiromania na “Waromania wa zamani kutoka Jeshi la Kigeni la Ufaransa”.
Inaongozwa na Horațiu Potra, Mromania ambaye anajielezea kama mwalimu wa kijeshi.
Mnamo Juni nikiwa Goma, niliona mamluki kama hao kwenye vituo vya ukaguzi na kuzunguka jiji, nikifanya kazi kwa ukaribu na jeshi.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, wengine wameripoti kuwaona nawanajeshi wa Congo kwenye magari ya jeshi.
“Walipowasili, kila mmoja alimtaja Mrusi,” Fiston Mahamba, mwanzilishi mwenza wa kundi la habari la Check Congo, aliiambia BBC.
“Nadhani hii ilihusishwa na kundi la mamluki la Urusi, Wagner na uwepo katika nchi kadhaa za Afrika.”
Kwa kweli, Asociatia RALF inaweza pia kufanya kazi kote Afrika, mkataba wake ulielezea kuwa ilikuwa na “maeneo mbalimbali ya kazi”, ikiwa ni pamoja na “Burkina Faso, DR Congo, Ivory Coast, Niger, Senegal, Sierra Leone, Gambia na Guinea”.
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa wanasema kuwa kampuni mbili za binafsi za kijeshi zililetwa ili kuimarisha vikosi vyake mnamo 2022, muda mfupi baada ya kundi la M23 kujikusanya tena na kuanza kuteka eneo la Kivu Kaskazini.
Jimbo hilo limekuwa na hali ya utulivu kwa miongo kadhaa huku wanamgambo kadhaa wakiendesha shughuli zao huko wakijipatia pesa kutoka kwenye madini yake kama dhahabu na coltan, yanayotumika kutengeneza betri za magari ya umeme na simu za mkononi.
Kampuni ya kwanza iliyosainiwa ilikuwa Agemira RDC, iliyoongozwa na Olivier Bazin, raia wa Ufaransa na Congo.
Wataalamu wanasema kampuni hiyo ya emplo, iliajiri raia wa Bulgaria, Belarus, Georgia, Algeria, Ufaransa na Congo.
Ilipewa jukumu la kukarabati na kuongeza mali za kijeshi za DR Congo, kukarabati viwanja vya ndege na kuhakikisha usalama wa ndege na maeneo mengine ya kimkakati.
Mkataba wa pili ulisainiwa kati ya Congo Protection, kampuni ya Congo inayowakilishwa na Thierry Kongolo, na Asociatia RALF. Kwa mujibu wa wataalamu wa Umoja wa Mataifa, mkataba huo ulibainisha kuwa Asociatia RALF ilikuwa na utaalamu na uzoefu mkubwa katika utoaji wa huduma za usimamizi wa usalama.
Ilitoa mafunzo na maelekezo kwa wanajeshi wa Congo kwa njia ya kikosi cha wakufunzi 300, wengi wao wakiwa Waromania.
Nilipozungumza na Bwana Potra mwezi Julai kuhusu kiwango cha ushiriki wa kundi lake katika ardhi ya DRC na kama kilihusika katika mapigano, alisema: “Tunapaswa kujilinda. Kama M23 itatushambulia, hawatasema tu: ‘Oh, wewe ni mwalimu tu nenda nyumbani’.”
Bw Potra alikuwa mjumbe wakati wa misheni ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hadi miezi michache iliyopita aliporejea Romania – na tangu wakati huo amehusishwa kwenye mzozo wa wakati wa kufutwa kwa uchaguzi wa rais nchini humo.
Alikamatwa mwezi Desemba na tangu wakati huo amekana kutoa usalama kwa mgombea anayeunga mkono Urusi, mgombea wa siasa kali za mrengo wa kulia Călin Georgescu. Na tangu Oktoba, amekataa kushika simu za BBC.
Mamluki huyo wa zamani ambaye alikuwa na umri wa karibu miaka arobaini na kwamba alizungumza na BBC kwa sharti la kutotajwa jina, alisema amejiuzulu kwa sababu hakufurahishwa na jinsi Asociatia RALF inavyofanya kazi.
Alisema Waromania walifanya mengi zaidi katika mkoa wa Kivu Kaskazini: “Ni idadi ndogo sana kati yetu tuliokuwa wakufunzi.
“Tulifanya kazi kwa zamu ndefu za hadi saa 12, tukilinda nyadhifa kuu nje ya Goma.”
Alisema malipo waliopata hayakuwa na thamani ukilinganisha na hatari ambazo wakandarasi wa kijeshi walipitia.
“Misheni hazikuwa na mpangilio, mazingira ya kazi yalikuwa duni. Waromania wanapaswa kuacha kwenda huko kwa sababu ni hatari.”
Pia alidai kuwa ukaguzi sahihi wa haukufanywa, na baadhi ya waajiriwa wa Kiromania hawakuwa na mafunzo ya kijeshi – akitoa mfano kuwa mmoja wa wafanyakazi wenzake wa zamani alikuwa afisa wa zima moto.
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo haijajibu ombi la BBC la kutaka maoni yao kuhusu iwapo ukaguzi wa nyuma ulifanyika, au kuhusu tofauti ya mishahara kati ya wakandarasi binafsi na wanajeshi wa Kongo.
Familia ya Vasile Badea, mmoja wa Waromania wawili waliouawa Februari mwaka jana wakati msafara wa jeshi ulipovamiwa na wapiganaji wa M23 ukiwa njiani kuelekea Sake, mji ulio mstari wa mbele karibu na Goma, aliiambia BBC kuwa alikuwa afisa wa polisi.
Afisa huyo mwenye umri wa miaka 46 alichukua muda wa mapumziko kutoka kwa kikosi chake cha Jeshi nyumbani ili kuchukua nafasi hiyo nchini DR Congo kwa sababu ya ofa ya mshahara mnono.
Polisi huyo alikuwa akihangaika kulipia nyumba ambayo alikuwa amenunua na alihitaji pesa zaidi.
Waromania wengi zaidi walivutiwa na kazi zenye malipo mazuri.
Nilikutana na mwanamume mmoja huko Bucharest mwezi Oktoba, ambaye alikuwa amerudi nyumbani akitafuta waajiriwa zaidi wa kwenda Goma. Alikuwa na historia ya kijeshi na alikuwa amefanya ziara za Nato nchini Afghanistan na jeshi la Romania.
“Tuna shughuli nyingi sana kujaribu kutafuta watu 800 ambao wanahitaji kuwa tayari kiakili kwa kazi hiyo na kujua jinsi ya kupigana,” msajili huyo wa mamluki aliambia BBC.
Alisema hakuifanyia kazi Asociatia RLF, lakini alikataa kusema alikuwa na kikundi gani cha wapiganaji.
“Waajiriwa watawekwa katika nafasi zinazolingana na kiwango cha mafunzo yao, wakipata kati ya $400-$550 kwa siku,” alifafanua.
Alipoulizwa kuhusu mchakato wa kuajiri, alisisitiza usiri wake.
“Kazi kama hizo hazichapishwi popote,” alisema, akiongeza kuwa mitandao kama WhatsApp ilipendelewa.
Alinionyesha kikundi cha WhatsApp ambapo zaidi ya Waromania 300 walikuwa wamejiandikisha, wengi wao wakiwa wanajeshi wa zamani.
Mwezi Juni mwaka jana, msemaji wa serikali ya Rwanda Yolande Makolo alikashifu kuhusu kuwepo kwa mamluki mashariki mwa DR Congo, akisema ni ukiukaji wa Mikataba ya Geneva, ambayo inakataza matumizi ya wapiganaji waliokodiwa.
Katika kujibu, msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya alipuuzilia mbali kile alichokiita malalamiko ya kudumu ya Rwanda.
“Tuna baadhi ya wakufunzi wanaokuja kutoa mafunzo kwa vikosi vyetu vya kijeshi kwa sababu ya hali hii ya dharura tuliyonayo ,” aliambia BBC.
Lakini mwanajeshi wa Kongo niliyekutana naye mwezi Juni alionyesha kusikitishwa kwake na mkakati wa jeshi hilo.
“Malipo si ya haki. Linapokuja suala la vita, sisi ndio tunapelekwa mstari wa mbele kwanza,” aliambia BBC kwa sharti la kutotajwa jina.
“Wao [mamluki] huja kama waungaji mkono tu.”
Alithibitisha malipo yake yalikuwa karibu $100 kwa mwezi lakini mara nyingi alichelewa au kutolipwa kabisa.
Mara ya mwisho niliwasiliana naye wiki moja iliyopita alipothibitisha kuwa bado yuko Kibati, karibu na Goma, ambako jeshi lina kambi.
“Hali ni mabaya sana,” alinijibu kwa ujumbe wa sauti.
Sijaweza kumpata tangu wakati huo – na kituo cha Kibati kimezidiwa nguvu na M23 huku askari wengi wakiuawa akiwemo kamanda wake.
Wachanganuzi wa mambo wanasema kuanguka kwa haraka kwa Goma kunaonyesha mkakati wa ulinzi uliofeli wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo .
Richard Moncrief, mkurugenzi wa mradi wa International Crisis Group katika Maziwa Makuu, anaeleza kuwa pamoja na mamluki, jeshi la Kongo linafanya kazi likishirikiana na askari wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), wanamgambo wa ndani wanaojulikana kwa jina la Wazalendo, pamoja na askari kutoka Burundi. .
“Inasababisha hali ambapo ni vigumu kuweka mikakati ya kijeshi ambapo kuna idadi kubwa ya wasimamizi na amri zinazokinzana ,” aliiambia BBC.
“Nadhani ni muhimu kufanya kazi kuelekea uwiano mkubwa zaidi katika juhudi za kijeshi katika Kivu Kaskazini na pengine kupunguza idadi ya makundi yenye silaha .”
Kwa mamluki huyo wa zamani, hatima ya wenzake wa zamani wa Kiromania haijashangaza.
“Uongozi mbaya husababisha jeshi kufeli katika majukumu yake,” aliambia BBC.