Wafanyakazi wa ubalozi wa Kenya mjini Kinshasa walilazimika kutoroka baada ya kuchomwa kwa ubalozi
Wafanyakazi wawili katika ubalozi wa Kenya katika mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kinshasa, walilazimika kutoroka na kutafuta hifadhi kwingine huku waandamanaji wakilenga jengo hilo mapema leo, serikali ya Kenya imesema.
Umati wa watu wenye hasira wakilalamikia shambulio la waasi dhidi ya Goma pia walishambulia balozi za Rwanda, Uganda, Ufaransa na Ubelgiji.
Katika taarifa yake, wizara ya mambo ya nje ya Kenya ilisema inasikitishwa sana na mashambulizi hayo ikiyataja kuwa “hayafai”.
Iliongeza kuwa kumekuwa na uporaji, na uharibifu wa mali.
Taarifa hiyo ilidai kuwa wakati shambulio dhidi ya ubalozi huo lilitokea “mchana” huku maafisa wa usalama wa Congo wakishuhudia na, “hawakuchukua hatua yoyote kuzuia hali hiyo”.
Ilielezea kile kilichotokea kama ukiukaji wa sheria za kimataifa kwani serikali za nchi wenyeji zinahitajika kulinda balozi.