CCM yampitisha rasmi Rais Samia kuwania urais 2025
Chama tawala nchini Tanzania, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepitisha azimio la kumteua Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wa nafasi ya urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika baadae mwaka huu.
Azimio hilo limepitishwa na Mkutano Mkuu wa CCM ambao ndiyo chombo cha mwisho cha maamuzi ya uteuzi wa mgombea wa tiketi ya urais kupitia chama hicho. Chama hicho pia kimempitisha Dkt. Hussein Mwinyi kugombea Urais kwa upande wa Zanzibar.
Uamuzi huo umefanyika mapema kuliko kawaida, na katika mkutano ambao awali haukupangwa kufanya maamuzi hayo katika ajenda zake. Mkutano huo ulikuwa na ajenda kuu moja ya kupitisha jina la Makamu wa Mwenyekiti (Bara) ambapo mwanasiasa mkongwe Stephen Wasira alipitishwa kushika wadhifa huo jana Jumamosi.
Hii leo, baadhi ya wajumbe waliokuwa wakitoa michango yao juu ya utekelezwaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM walipendekeza mkutano huo kuwapitisha Rais Samia na Rais Mwinyi kama wagombea wa urais kutokana na maendelea walioyasimamia.
Rais mstaafu Jakaya Kikwete, akizungumza kama mmoja wa wazee wa chama, alisisitiza kuwa CCM ina mamlaka ya kujichagulia mgombea wao kwa wakati wowote. “Hili lipo ndani ya uwezo wetu, kuamua muda wowote, kwamfano wenzetu (wa Swapo) Namibia wao wanafanya uchaguzi kumpitisha mgombea wao mwaka mzima (kabla ya uchaguzi). Sasa na sisi tunaweza kuamua. Jambo la Msingi azimio lipite na tupate ushauri wakisheria ili uendane na matakwa ya tume ya uchaguzi.”
Hii ni mara ya kwanza kwa CCM kupitisha wagombea wa nafasi za urais mapema katika mwanzo wa mwaka na katika kikao ambacho ajenda yake mahsusi haikuwa hiyo. Kawaida, maamuzi hayo hufanyika miezi michache kabla ya kuanza kwa kampeni rasmi za uchaguzi mkuu.
Nchimbi mgombea mwenza wa Samia
Rais Samia pia amemteua Katibu Mkuu wa CCM Emmanuel Nchimbi kuwa mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu utakaofanyika baadae mwaka huu.
Nchimbi ni mwanasiasa mwandamizi na ameshika nafasi mbali mbali ndani ya CCM na serikali yake kwa miongo mitatu iliyopita. Amewahi kushika nafasi ya Waziri wa Mambo ya Ndani katika serikali ya Kikwete na aliteuliwa kuwa balozi na hayati John Pombe Magufuli na kuiwakilisha Tanzania nchini Brazil na baadae Misri.
Kwa mujibu wa Rais Samia, Makamu wa Rais wa sasa Philip Mpango alimuomba apumzike na ameridhia na ndio maana amemteua Nchimbi.
Mpango ataendelea na majukumu yake kama Makamu wa Rais mpaka uchaguzi utakapofanyika, sawia na Nchimbi ambaye ataendelea na majukumu yake ndani ya chama kwa sasa.
Awamu ya mwisho kwa Samia na Mwinyi
Marais wote wawili Samia na Mwinyi wanamaliza awamu zao za kwanza za uongozi mwaka huu. Na kwa mujibu wa utamaduni wa chama hicho, marais walio madarakani huwa hawapatiwi ushindani katika kupewa tiketi ya kugombea urais kwa awamu ya pili.
Rais Samia aliingia madarakani mwezi Machi 2021 mara baada ya kifo cha aliyekuwa rais wa Tanzania John Pombe Magufuli. Aliingia madarakani kwa mujibu wa katiba akiwa ndiye mrithi wa urais, kwa nafasi aliyokuwa nayo kipindi hicho ya Makamu wa Rais.
Kwa mujibu wa katiba ya Tanzania, kwa kuwa amekaa madarakani kwa zaidi ya miaka mitatu toka kufariki kwa Magufuli basi kipindi hiki kinahesabika kama muhula wake kamili na ataruhusiwa kugombea urais mara moja tu.
“Endapo Makamu wa Rais anashika kiti cha Rais kwa mujibu wa masharti ya ibara ya 37(5) kwa kipindi kinachopungua miaka mitatu ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara mbili, lakini kama akishika kiti cha Rais kwa muda wa miaka mitatu au zaidi ataruhusiwa kugombea nafasi ya Rais mara moja tu,” inaeleza katiba ya Tanzania.
Mkala hii imebeba madhui yaliyotoka kwenye mitandao ya kijamii. Tunaomba ruhusa yako kabla kitu chochote hakija pakiwa, sababu wanaweza wakawa wanatumia Cookies na tekinolojia nyingine. Unaweza ukasoma sera sera ya kutumia cookies katika mitandao ya kijamii kabla ya kukubali. Kutazama maudhui haya chagua accept and continue.
Hivyo baada ya kupitishwa kuwa mgombea leo na endapo atashinda urais katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu, ukomo wa Rais Samia kushika Madaraka ya urais utakuwa nim waka 2030.
Hivyo hivyo itakuwa kwa upande wa Zanzibar kwa Rais Mwinyi ambaye aligombea kwa mara ya kwanza urais mwaka 2020, baada ya kupitia mchujo wa ushindani ndani ya chama.