Kusitishwa vita Gaza kutamaliza mauaji lakini hakutamaliza mgogoro

Kusitishwa vita Gaza kutamaliza mauaji lakini hakutamaliza mgogoro

Afisa wa ngazi ya juu wa Palestina aliambia BBC kuwa Hamas itawaachilia wanajeshi watatu wanawake katika siku ya kwanza ya mapatano ya kusitisha vita.

Wapatanishi huko Doha wanajaribu kuyafanya mapatano ya kusitisha vita yaanze mapema, Alhamisi jioni badala ya Jumapili.

Hadi mapatano ya kusitisha vita yatakapotekelezwa, vita vilivyoanza baada ya Hamas kuishambulia Israel tarehe 7 mwezi Oktoba 2023 bado vinaendelea.

Wapalestina 12 waliuawa katika mashambulizi ya Israel kaskazini mwa Gaza wakati mapatano ya kusitisha vita yalipotangazwa.

Video kutoka kaskazini mwa Gaza zinaonyesha miili ya waathiriwa wa mashambulizi ikichukuliwa kutoka katika ambulansi na kisha kupangwa nje ya hospitali.

Mapatano ya kusitisha vita ni mafanikio makubwa ya kidiplomasia lakini yamechelewa kwa muda mrefu.

Toleo la makubaliano haya limekuwa likijadiliwa tangu yalipotangazwa na Rais wa Marekani, Joe Biden, mwezi Mei mwaka jana.

Hata hivyo, Hamas na Israel wanalaumiana kwa kuchelewesha utekelezaji wa makubaliano hayo.

Huko Khan Younis, Gaza, waandishi wa habari wa BBC walipiga picha Wapalestina wakifurahia kwa nyimbo baada ya kujua kuwa mapatano ya kusitisha vita yamekubaliwa.

Israel haitoi ruhusa kwa waandishi wa habari wa kimataifa kuingia Gaza na kuripoti kwa uhuru, hivyo BBC na mashirika mengine ya habari hutegemea waandishi wa habari wa Palestina walio jasiri ili kukusanya habari kwa niaba yetu.

Bila wao, ripoti za vita vya miezi 15 iliyopita zingekuwa vigumu kufanywa. Israel imeua zaidi ya waandishi wa habari 200 wa Palestina huko Gaza.

Umm Muhammad, ajuza mmoja huko Palestina, alimwambia mmoja wa waandishi wetu kuwa anajisikia furaha na kufarijika.

“Maumivu yamepungua kidogo, ingawa bado yapo. Tumaini ni kwamba dhiki zitakwisha na itakuwa furaha daima. Wacha wafungwa wetu waachiliwe na wale waliojeruhiwa wapate matibabu. Watu wamechoka.”

Mbali na kuishi, hakuna mengi ya kusherehekea kwa Wapalestina huko Gaza.

Israel imeua takribani watu 50,000.

Zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakilazimishwa kutoka nyumbani mwao kwa sababu ya mashambulizi ya kijeshi ya Israel.

Majibu ya Israel kwa mashambulizi ya Hamas tarehe 7 Oktoba 2023 yaliyoua watu takribani 1200, wengi wao raia wa Israel, yameacha Gaza ikiwa imeharibiwa.

Kulingana na wizara ya afya inayosimamiwa na Hamas, mashambulizi ya Israel yameua karibu watu 50,000, ikiwa ni pamoja na wapiganaji na raia.

Utafiti wa hivi karibuni uliochapishwa kwenye jarida la matibabu la Lancet unasema kuwa idadi hii huenda ni ndogo kuliko idadi yenyewe.

Huko Tel Aviv, ilikuwa ni wakati wa furaha kwa familia wa mateka wa Israel, walioko hai na waliokufa.

Katika awamu ya kwanza ya mapatano ya kusitisha vita, wanawake 33, wazee, wagonjwa na waliojeruhiwa wanatarajiwa kuachiliwa katika wiki sita zijazo kwa kubadilishana na mamia ya wafungwa wa Palestina – lakini mustakabali wa mateka wengine wa Israeli unategemea mazungumzo zaidi.

Mazungumzo kuhusu awamu ya pili ya makubaliano, ya kuwaachilia mateka wa Israeli waliobaki kwa kubadilishana na wapalestina waliokamatwa na kujiondoa kwa Israel kutoka Gaza, yanatarajiwa kuanza baada ya siku kumi na sita tangu makubaliano yatakapoanza.

Changamoto kubwa ya kwanza ni kuhakikisha kuwa mapatano ya kusitisha vita yanaendelea kudumu.

Mabalozi wakuu wa magharibi wana hofu kuwa baada ya awamu ya kwanza ya siku 42 vita vinaweza kuanza tena.

Vita vya Gaza vimekuwa na madhara makubwa kwa Mashariki ya Kati.

Hamas bado ina uwezo wa kupigana lakini haina nguvu kama ilivyokuwa hapo awali.

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na waziri wake wa zamani wa ulinzi wanakosolewa kwa uhalifu wa kivita na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu.

Mahakama ya Kimataifa ya Haki inachunguza kesi iliyowasilishwa na Afrika Kusini inayoshutumu Israel kwa mauaji ya kimbari.

Baada ya Hezbollah huko Lebanoni kuingilia vita, hatimaye ilishindwa katika vita na Israel.

Hii ilikuwa moja ya sababu zilizochangia kuanguka kwa utawala wa Assad nchini Syria. Iran na Israel zilishambuliana moja kwa moja. Mtandao wake wa washirika ambao Tehran inauita “Mhimili wa Upinzani” umeharibiwa.

Houthi nchini Yemen wamezuia meli nyingi za usafirishaji kati ya Ulaya na Asia kupitia Bahari ya Shamu. Sasa ripoti zinasema wametangaza kusitisha vita.

Tangu walipoanza kushambulia meli mwanzoni mwa vita, wamesema kuwa kusitishwa kwa vita huko Gaza ndio njia pekee itakayosimamisha mashambulizi yao.

Kwa bahati, joto la kisiasa, na juhudi za kidiplomasia, mapatano ya kusitisha vita yanaweza kuwepo licha ya uvunjaji mapatano unaoweza kutokea.

Huenda maafikiano ya kusitisha mapigano Gaza yakakomesha mauaji ya kiholela na kuwarejesha mateka wa Israel na mahabusu wa Palestina kwa familia zao.

Lakini baada ya miezi 15 ya vita huko Gaza, mgogoro ambao umedumu zaidi ya karne moja bado ni mchungu na mgumu kuutatua.

Mapatano ya kusitisha vita hayamalizi mgogoro huu. Madhara ya uharibifu na vifo vingi yataendelea kuhisiwa kwa vizazi vijavyo.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *