Netanyahu katikati ya changamoto za madaraka na matarajio ya kujitanua kikanda

Netanyahu katikati ya changamoto za madaraka na matarajio ya kujitanua kikanda

Vyombo vya habari vya kimataifa vinaendelea kufuatilia maendeleo ya vita kati ya Israel na Hamas, baada ya Syria kugonga vichwa vya habari katika siku chache zilizopita kufuatia kuanguka kwa utawala wa Bashar al-Assad.

Magazeti ya Marekani yanaeleza kushangazwa na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kung’ang’ania madarakani licha ya hati ya kukamatwa iliyotolewa dhidi yake, huku magazeti ya Israel yakipingana na hayo, yakimwona kuwa “kiongozi mpya” katika eneo la Mashariki ya Kati.

Kwa upande wa vyombo vya habari vya Kiarabu vinajadili dalili kutokea vita ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi na Lebanon na kugeuka kuwa mzozo mkubwa wa kikanda.

Trump na Netanyahu wana maono ya utaifa

Kumtuhumu Netanyahu, Waziri wa Ulinzi wa zamani Yoav Galant, na kiongozi wa zamani wa Hamas Mohammed Deif kwa kufanya “uhalifu dhidi ya ubinadamu,” ndilo jambo kuu ambalo Noah Landau alianza nalo makala yake, yenye mukhtasari”Netanyahu ang’ang’ania madaraka kwa njia ya ajabu.”

Makala iliyochapishwa na gazeti la Marekani la “The New York Times” linatoa uchanganuzi wa hali ya kisiasa nchini Israel baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu mjini The Hague kutoa hati ya kukamatwa isivyo kawaida dhidi ya Netanyahu, Galant na Al-Daif.

Tishio hili lina maslahi madogo tu kwa Israeli, kwa mujibu wa mwandishi, ambaye aliona kwamba Waisraeli walikuwa na nia zaidi ya kumfukuza Galant, wakati ambapo Washington ilikuwa na wasiwasi na uchaguzi wa Marekani.

Licha ya “mapungufu makubwa ya kiusalama” yaliyoshuhudiwa nchini Israeli mnamo Oktoba 7, 2023, kwa mujibu wa mwandishi, Netanyahu “aliweza kuijenga tena nguvu yake ya kisiasa na kuzidisha mzozo wa kikanda.”

Makala hayo yanaangazia mafanikio ya Netanyahu katika kukaidi majaribio ya utawala wa Biden ya kumaliza vita huko Gaza, na pia kukabili ukosoaji wa kimataifa.

Pia inajadili jinsi Netanyahu alivyoweza kuepa kesi zake za ufisadi zilizoanza mwezi huu, ambapo kwa mujibu wa kura za maoni bado ameendelea kuwa na ushawishi kisiasa.

Andiko hilo pia linaonyesha kwamba nguvu kuu ambayo imemsaidia Netanyahu kuimarisha mamlaka yake ni “upinzani dhaifu na uliogawanyika,” kwani wapinzani wake wengi wanakataa vita, wanapinga uongozi wa Netanyahu, na “wanakosa maono mbadala ya kisiasa,” kama Landau anavyoeleza.

Mwandishi anazungumzia athari zinazoweza kutokea kufuatia kurejea kwa Donald Trump katika Ikulu ya White House na athari zake kwa sera ya Israeli chini ya utawala wa Netanyahu, akibainisha kuwa Trump na Netanyahu “wana maono yanayofanana kitaifa ambayo yanalenga kudhoofisha utaratibu wa uliozoeleka na taasisi za kimataifa, hasa kwa kuzingatia suala la Palestina.

Landau pia anaeleza kuwa viongozi wote wawili wanakubaliana kisiasa katika masuala muhimu, ikiwa ni pamoja na kuunga mkono makaazi ya Waisraeli katika Ukingo wa Magharibi, pamoja na kupitisha sera kali dhidi ya Wapalestina.

Ingawa mwandishi anadokeza kuwa utawala wa Trump unaweza kutaka kumaliza vita huko Gaza, anaelezea wasiwasi wake kwamba makubaliano yoyote ambayo yanaweza kuhitimishwa kati ya pande husika “hayatakuwa na usawa na yatakuwa na matokeo mabaya kwa Wapalestina.”

Anahitimisha kwa kuzungumzia kuendelea kwa sera za itikadi kali zinazoongozwa na Netanyahu, kwa ushirikiano na Trump na utawala wa Marekani “wenye msimamo mkali zaidi”, ambao utaweka ugumu kufikia amani ya kudumu katika eneo la Mashariki ya Kati.

Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ilitoa vibali vya kukamatwa kwa Netanyahu na Galant Novemba mwaka jana kwa tuhuma za "uhalifu wa kivita."

CHANZO CHA PICHA, GETTY IMAGES

“Je, maamuzi ya Netanyahu kuhusu vita yanaakisi vipi nadharia za Churchill?”

Makala iliyochapishwa katika gazeti la Israel la “The Jerusalem Post” inalinganisha misimamo ya Netanyahu na nafasi ya kihistoria iliyochukuliwa na Uingereza katika Vita vya Pili vya Dunia, haswa mnamo 1941 wakati baadhi ya vikosi vya Iraq vilishirikiana na Wanazi dhidi ya Uingereza.

Mwandishi wa makala hiyo, Uri Kaufman, anasimulia kwamba Jenerali wa Uingereza Archibald Wavell nchini Misri alikuwa ametuma maonyo kwamba “hakuna msaada wowote unaoweza kutolewa kwa Iraq,” lakini Waziri Mkuu wa Uingereza Winston Churchill alipuuza maonyo hayo na kuamuru mashambulizi ya kukabiliana na Iraq tena. Licha ya hatari, matokeo ya uamuzi huu yalifanikiwa na kupelekea Uingereza kutwaa tena Iraq.

Mwandishi anarejea kulinganisha kile kilichotokea baada ya Oktoba 7, 2023, na anabainisha kuwa licha ya wito wa utulivu na kujizuia uliotolewa na Rais wa Marekani Joe Biden,ndani ya Israeli na baadhi ya watu wa kisiasa, Netanyahu alikuwa akishikilia msimamo wake wazi wa kuingia Gaza, kuangamiza Hamas, na kuwarudisha mateka wa Israel.

Kaufman anaamini kwamba jeshi la Israel lilikuwa limejipanga vyema kwa shambulio hili, licha ya kutiliwa shaka na ukosoaji, kama alivyosema, akiashiria mazungumzo kufanyika ili kuwaachilia mateka, hatua anayoiona kama hatua kubwa katika mazingira ya vita.

Mwandishi anasifu uthabiti wa Netanyahu katika maamuzi yake, licha ya maonyo ya mfululizo na Marekani kusimamisha usambazaji wa silaha kwa Israeli “katika kipindi hicho muhimu.” Makala hiyo pia inabainisha kuwa Netanyahu hakupata uungwaji mkono wa kweli kutoka kwa baadhi ya viongozi wa kijeshi nchini Israel.

Mwandishi huyo anaamini kwamba yale ambayo Netanyahu aliyapata katika Ukanda wa Gaza, pamoja na “kuharibu uwezo wa Hezbollah” nchini Lebanon, ni “mafanikio yanayoonyesha kuwa Netanyahu alidhamiria kusonga mbele katika kuyafikia.”

Makala hiyo inaeleza kuwa Netanyahu amefanikiwa kuiongoza Israel katika kipindi kigumu, na kushinda ukosoaji wa ndani na kimataifa, akitegemea maamuzi ya kimkakati ya kijasiri ambayo yanasisitiza haja ya kukabiliana na harakati za makundi kama Hamas na Hezbollah, ambayo yanaonyesha uwezo wa uongozi wa kisiasa katika kukabiliana na nyakati ngumu kwa mujibu wa mwandishi.

“Uharibifu wa Gaza na matokeo yake haukuanza Oktoba 7

Idadi ya vifo vya Wapalestina huko Gaza inazidi 45,000 tangu kuanza kwa vita

CHANZO CHA PICHA, REUTERS

Katika makala yao iliyochapishwa katika Al-Quds Al-Arabi, waandishi Oded Goldreich na Assaf Kfoury walizisoma dalili za vita huko Gaza na Ukingo wa Magharibi unaoongezeka na kuwa vita vya kina vya kikanda.

Makala hiyo iliyopewa jina la “Uharibifu wa Gaza na Madhara yake Hayakuanza Oktoba 7,” inazungumzia mazingira yaliyosababisha vita hivyo, ikibainisha kwamba “kinachoonekana sasa kuwa ghasia na uharibifu ni matokeo ya miongo kadhaa ya sera za Israel zinazolenga Wapalestina wanaoungwa mkono na Marekani bila masharti.”

Makala hiyo pia inaeleza kwamba kile ambacho kimepuuzwa katika matangazo mengi ya vyombo vya habari ni “vita vya siri vilivyoanzishwa na Israel dhidi ya Wapalestina, ambavyo vimechangia wao kutengwa na dhulumiwa.

Waandishi hao wanahoji kuwa idadi kubwa ya Waisraeli walipuuza mzozo wa Israel na Palestina kabla ya Oktoba 7, 2023, au waliona kuwa ni tatizo linaloweza kuzuiwa au kupuuzwa.

Wanaangazia maendeleo ya kiuchumi ambayo Israel imeshuhudia katika miaka iliyopita, ambayo yalichangia “kuimarika kwa uchumi na ongezeko la idadi ya watalii,” pamoja na ukaribu uliotokea na baadhi ya serikali za Kiarabu ndani ya rasimu ya “Mkataba wa Ibrahimu.

Waandishi hao wanaamini kuwa mateso ya Wapalestina ndani ya Israel yanawakilishwa na ubaguzi wa kitaasisi na kutengwa kwa jamii, wakati Ukingo wa Magharibi ulikuwa ukishuhudia sera kali ya udhibiti wa mabavu iliyojumuisha makazi, ukuta uliowatenganisha, na vitendo vingi vya ukandamizaji, kulingana na maelezo yao.

Nakala hiyo pia inaangazia kizuizi cha Gaza, na inahusu “Maandamano Makubwa ya mnamo 2018, ambapo maandamano ya amani yalizimwa kwa “nguvu kubwa” na Israeli.

Aidha inasema kwamba shambulio lililotekelezwa na Wapalestina halikuwa tu kulipiza kisasi, bali ni kauli ya “kukata tamaa kutokana na ukandamizaji unaoendelea.” Nakala hiyo inahusisha shambulio hilo na wimbi la hasira na mlipuko wa ghafla wa vita, kama matokeo ya kuzorota kwa hali ya Gaza na Ukingo wa Magharibi, na “wakati ambao Waisraeli hawakutarajia,” wanaeleza

Waandishi hao pia wanapitia hatua zilizochukuliwa na Israel baada ya shambulio hilo, ambalo kulishuhudiwa ongezeko la mashambulizi ya mabomu na operesheni za kijeshi huko Gaza, huku idadi ya waathirika ikiongezeka.

Mwishoni mwa makala hayo, wanajadili sera ya Marekani katika eneo hilo, wakibainisha kwamba uungaji mkono usio na masharti wa Marekani kwa Israel umechangia “kuendeleza uvamizi wa Israel,” na wanasisitiza haja ya kutafuta “suluhisho la haki kwa mzozo wa Israel na Palestina.” na kuwahakikishia haki Wapalestina na kumaliza mateso yao.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *