‘Vitiligo ya midomo imenitenganisha na marafiki’

‘Vitiligo ya midomo imenitenganisha na marafiki’

Ni jambo linalomhusu kila mtu – tabasamu lako.

Ambalo linahusiana na midomo yako.Ikiwa unakumbana na vitiligo ya midomo, unakabiliwa changamoto kwa sababu huwezi kucheka hadharani, unahisi aibu kuwa mbele ya watu.

Kuna mambo kadhaa yanayosababisha midomo kugeuka rangi lakini wanaokabiliwa na vitiligo hasa ya midomo wanajipata katika mazingira ya unyanyapaa, baadhi yao kuogopa kutangamana na watu.

Wakati wa janga la corona,watu walivaa barakoa na iliwasaidia wengi waliokuwa na shida hii lakini baada ya Covid 19, unyanyapaa umezidi.

Alice sio jina lake halisi anaiambia idhaa ya BBC masimango anayoyapata na matusi ya nguoni kutokana na midomo yake kuwa na rangi tofauti.

“Nimekuwa na hali hii ya midomo yangu kuwa nyeusi na katikati nyekundu kwa zaidi ya miaka mitano sasa. Haijakuwa rahisi kwangu marafiki zangu wamenitenga wakisema nina Virusi Vya Ukimwi(VVU) ..sina marafiki tena”.

Naye Suzan ambaye sio jina lake halisi mwenye umri wa miaka ya 30 anasema alikuwa akiona watu wakiwa na rangi tofauti ya midomo na alishangaa ni kipi kinawadhuru asijue miaka mitano baadaye naye ataathirika na hali hii. Siku moja alijiangalia kwenye kioo akagundua midomo yake imebadilika rangi na alishtuka sana!

Na sio wanawake pekee wanaokabiliwa na hali kama hii pia wanaume wanapitia masimango kutoka kwa jamaa na marafiki. Baadhi ya watu waliozungumza na BBC wanaeleza kuwa wamekuwa wakishukiwa ni walevi kupitiliza na wavuta sigara.

Baadhi ya waathiriwa wa ugonjwa huu wanasema wakiwa miongoni mwa watu wanajipata wakiziba midomo yao ili wasiangaliwe vibaya.

Na kutokana na hili wanasema ni gharama kutafuta matibabu wakiamini kuwa haina tiba waliojaribu baadhi ya krimu za kupunguza rangi hiyo kuonekana.

“Zile pesa nimeharibu kutafuta matibabu ,inanivunja moyo na imebidi niwe na ujasiri niishi na hali hii,” anasema muathiriwa.

Vitiligo ya midomo ni nini?

Vitiligo ni hali inayosababisha mabaka mwilini ambayo husababishwa na ukosefu wa seli zinazosaidia mwili kuwa na rangi yake ya kawaida.

Vitiligo, hata ikiwa ndogo huwaathiri wagonjwa wanaokabiliwa nayo na inaweza kusababisha wasiwasi mkubwa wa kihemko ikiwa halitapewa matibabu.

Vitiligo ya midomo ya chini ya upande ni aina maalum ya vitiligo ya mdomo ambayo huathiri 16% ya wagonjwa wote wa vitiligo.

Huanza kama doa kwenye sehemu ya pembeni ya mdomo wa chini na kuenea katikati kama mstari mwekundu kando ya mpaka wa mdomo.

Vitiligo ya midomo ni kubadilika kwa ngozi ambayo husababishwa na matatizo ya kinga na pia huwa inatokea iwapo una jenetiki zinazokua hali hii .

Lakini kubadilika kwa rangi ya midomo kuwa nyekundu au nyeusi ,sio vitiligo na husababishwa na maambukizi ya midomo ,au kunywa vitu vikali au moto na pia uzio.

Hata hivyo midomo ikibadilika rangi na kuwa buluu inaashiria huna oksigeni yakutosha na huenda ukawa una ugonjwa wa moyo au mapafu ,mtaalam asema.

Daktari pia anaendelea kueleza kuwa iwapo rangi ya midomo ina vidoa vyeusi ni ishara una ugonjwa wa tumbo ambayo kwa jina la kimatibabu ni melamolaic ambayo inaweza kuwa na viini vya kansa.

Na ukiwa na rangi ya midomo ni nyeupe inaashiria huna damu ya kutosha na vitamini vya madini ya chuma mwilini.

Midomo

CHANZO CHA PICHA, VGK

Dalili vitiligo kwenye midomo ni zipi?

Vitiligo kwenye midomo mara nyingi huanza na vidonda vidogo vya ngozi vilivyo na rangi tofauti.

Ingawa vidonda hivi vya rangi nyeupe vinaweza kuonekana mahali popote kwenye midomo, mara nyingi huonekana kwenye mdomo wa chini upande wa pembeni.

Awali, vidonda vidogo vya rangi nyeupe huonekana na kisha kuenea polepole kwenye sehemu nyingine za mwili.

Muda wa kuenea hutofautiana kwa watu tofauti na unaweza kuchukua miezi au hata miaka. Sababu mbalimbali zinajulikana kuchangia kuanza na kuenea kwa vitiligo.

Wakati vitiligo inaanzia kwenye uso, inaweza kuonekana sehemu yoyote kama vile midomo, macho, mashavu, paji la uso, kidevu, shavu la sikio, na hata ndani ya masikio.

Vitiligo la eneo maalum huanza na vidonda vidogo.

Wakati mwingine, vidonda vya rangi nyeupe vinaweza kuonekana kwenye midomo na sehemu za siri.

Hali hii inaitwa mucosal vitiligo. Ikiwa vidonda vya rangi nyeupe viko tu kwenye midomo na vidole, inaitwa lip-tip vitiligo.

Ni kipi kinasababisha vitiligo kwenye midomo?

Ingawa sababu halisi ya vitiligo haijulikani, kuna sababu nyingi za kimazingira na za kijenetiki zinazoweza kusababisha hali hii ya ngozi.

Hizi ni baadhi ya sababu zinazojulikana:

  • Matatizo ya kinga ya mwili

Hapa, kinga ya mwili ya mtu anayekumbwa na vitiligo inaweza kutengeneza viambato vinavyoshambulia na kuharibu seli zinazozalisha melanin (melanocytes). Uharibifu wa melanocytes unazuia uzalishaji wa melanin, hivyo kusababisha kupotea kwa rangi kwenye ngozi, na hii inaweza kupelekea vitiligo.

  • Urithi

Utafiti uliofanywa kuhusu urithi wa vitiligo kwa watu 150 wanaokabiliwa na tatizo hili, ulionyesha kuwa sababu za kijenetiki zinachukua nafasi muhimu katika kuanzisha vitiligo. Takriban 30% ya watu wenye hali hii wana historia ya familia inayohusiana na tatizo hili.

  • Maambukizi

Baadhi ya maambukizi ya virusi au bakteria kama vile kaswende, ukoma, lichen planus, nk, yanaweza pia kusababisha vitiligo.

  • Mambo ya Nervo (Neurogenic Factors)

Utafiti mmoja uliofanywa mwaka 2012 kuhusu hali inayowezekana ya kuchochea neva za genitiki ya uvimbe katika vimelea vya vitiligo ulionyesha kuwa mambo ya neurogenic kama vile ‘neuropeptides’ na vitu vingine vya ukuaji wa neva vinahusika katika hisia. Mambo haya yanaweza pia kuwa na sumu kwa melanocytes na kusababisha kuanzishwa kwa vitiligo kwa watu wenye hatari.

  • Mwili kujiumiza(Self-Destruction)

Wakati mwingine, matatizo katika melanocytes yanaweza kuzuia uzalishaji wa melanin na kusababisha vitiligo.

  • Mazingira ya Kazi

Baadhi ya kazi zinahitaji mtu kukutana na kemikali fulani au mionzi ya UV kutoka kwa jua mara kwa mara. Hali hizi za nje zinaweza kuchochea vitiligo.

Vitiligo nnavyotokea kwenye midomo

Rangi ya ngozi ya mwili inatokana na melanin, rangi inayozalishwa na seli zako.

Vitiligo hutokea wakati seli zinazozalisha melanin (melanocytes) zinapokufa au kupoteza uwezo wa kufanya kazi.

Utafiti uliofanywa kuhusu vitiligo kwenye mdomo wa chini wa pembeni ulionyesha kuwa asilimia 16.39% ya wagonjwa wa vitiligo walikuwa na vitiligo kwenye sehemu hiyo ya mdomo.

Vitiligo inaweza kutokea kutokana na hali ya ukosefu wa kinga mwilini, urithi, au sababu zingine.

Bila chembechembe zinazotoa rangi ya asili ya midomo, vidonda vyeupe au vya rangi ya shaba huanza kuonekana.

Hakuna sehemu maalum ambapo vitiligo huanzia.

Inaweza kuanza kwenye midomo au maeneo ya karibu, au unaweza kuona vidonda vya rangi nyeupe kwanza sehemu nyingine za mwili na baadaye kwenye midomo yako.

Tiba ya vitiligo ya midomo

Dkt Salim M Ishmael, mwanzilishi mwenza wa Medics for Kenya na pia daktari amependekeza kuwa iwapo hali hii inakupa wasiwasi au ni uchungu kuvumilia unahitajika kupata matibabu.

Dkt. Salim anasema, “unaweza kufanyiwa matibabu ya mionzi ,au upasuaji ama krimu za tropiki”. “Lakini kile tunapendekeza mara ya kwanza iwapo unabadilika rangi ya midomo inaweza kuwa ni mzio na unapaswa kuumia sphere 50 plus lip balm na pia ufuate miko na kutumia vitamini nyingi” ,Salim anaeleza.

Wataalam wa masuala ya sosholojia wametoa wito kwa watu kutokuwa na dhana hasi kwa watu wanaougua ugonjwa huu kwani sio kifo na haiambukizani.

Ingawa huna amani na hali hii ya rangi ya midomo pata ushauri wa matibabu ili kukabiliana na hali hii.

Ufitinema Aime Gerard

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *