Rais wa zamani anayetaka kuongoza tena Ghana
John Dramani Mahama aliwahi kuwa rais wa Ghana, na sasa anajaribu tena kuwania wadhifa huo.
Mahama, mwenye umri wa miaka 65, aliongoza Ghana kutoka mwaka wa 2012 hadi 2017 na ni miongoni mwa wanasiasa waliobobea zaidi katika taifa la Afrika Magharibi. Amewahi kushika nyadhifa mbalimbali, ikiwa ni pamoja na Mbunge, Naibu Waziri, Waziri, Makamu wa Rais, na Rais.
Siasa zilianza kuwa na umuhimu mkubwa katika maisha ya Mahama akiwa mtoto. Alikuwa na umri wa miaka saba tu, baba yake, Emmanuel Adama Mahama, aliyekuwa waziri wa serikali alikamatwa na kufungwa katika mapinduzi ya kijeshi, kisha akaenda mafichoni.
Matukio kama haya ameyaweka wazi katika vitabu alivyoandika, makala ambayo yamechapishwa na vyombo mbalimbali vya habari vya kimataifa. Pia,kitabu cha kumbukumbu yake ya maisha, My First Coup D’etat, ilipokelewa vyema na waandishi wakubwa wa fasihi ya Kiafrika, kama vile Ngugi wa Thiong’o kutoka Kenya na Chinua Achebe wa Nigeria.
Katika kuandika sera zake za uchaguzi wa mwaka huu, Mahama alieleza kuwa Ghana “iko kwenye mwelekeo mbaya na inahitaji kuokolewa.”
Hata hivyo, wakosoaji wake wanadai kuwa huenda yeye si mtu sahihi kwa wadhifa huo, hasa kutokana na matatizo ya kiuchumi na kashfa za ufisadi zilizokumba utawala wake alipokuwa rais.
Safari ya Mahama ilianzia mwaka 1958 alipozaliwa mjini Damongo kaskazini mwa Ghana. Baada ya miaka michache, alihamia Accra, mji mkuu, kuishi na baba yake. Katika kitabu cha kumbukumbu yake, Mahama anasema alikua mtoto mchangamfu mwenye hamu ya kujifunza.
Mahama alikuwa na maisha ya kifahari kiasi. Familia yao ilikuwa na nyumba nyingine katika mji wa Bole, ambapo wakati huo hawakuwa na umeme. Familia yake ilijitahidi kununua jenereta la dizeli kwa ajili ya nyumba yao ya vyumba sita, na kuifanya nyumba yao kuwa ya pekee iliyokuwa na taa wakati huo.
Alienda shule ya bweni ya Achimota, moja ya shule maarufu inayojivunia kuwaelimisha viongozi wa mataifa, wakiwemo Jerry John Rawlings wa Ghana, aliyekuwa rais wa Zimbabwe Robert Mugabe na Kwame Nkrumah, waziri mkuu wa kwanza wa Ghana baada ya uhuru.
Ni katika shule ya Achimota ambapo aliguswa na taarifa ya mapinduzi ya kijeshi ya mwaka 1966, ambapo wanajeshi waliteka majengo ya serikali na kumng’oa Nkrumah madarakani. Mahama alijawa na hofu, hasa baada ya kutokupewa taarifa yoyote kuhusu baba yake, na alihofia kuwa alikuwa ameuawa.
Baada ya mapinduzi ya pili ya kijeshi mwaka 1981, baba yake alikimbilia Nigeria. Mahama aligang’ania masomo na , akahitimu shahada ya masomo ya mawasiliano kutoka Chuo Kikuu cha Ghana na kisha akaenda Moscow kusomea katika Taasisi ya Sayansi za Jamii.
Alisema kwamba wakati wa uongozi wa Umoja wa Kisovyeti, aliweza kuona “mapungufu ya mfumo wa kijamaa.”
Aliporejea Ghana mwaka 1996, Mahama alifuata nyayo za baba yake katika siasa. Alichaguliwa kuwa Mbunge kupitia chama cha National Democratic Congress (NDC) na akaendelea kupanda vyeo katika serikali. Alipewa nafasi ya kuwa msemaji wa bunge na waziri wa mawasiliano.
Baada ya miaka 13, Mahama alikua Makamu wa Rais chini ya Rais John Atta Mills. Hata hivyo, baada ya kifo cha ghafla cha Mills mwaka 2012, Mahama alikula kiapo cha kuwa Rais. Aliiita siku hiyo kuwa “siku ya huzuni zaidi” katika historia ya Ghana.
Baada ya uchaguzi mkuu uliofuata, Mahama alichaguliwa kuwa Rais tena.
Je,Mahama ni kiongozi wa aina gani?Franklin Cudjoe,mchanganuzi wa masuala ya kisiasa nchini Ghana aliiambia BBC kuwa Mahama alijulikana kama mwasilishaji mzuri, lakini pia alikumbwa na changamoto kubwa za kiuchumi na kashfa za ufisadi, huku raia wa Ghana wakikumbwa na mgao wa umeme. Alijulikana kama “Mr. Dumsor” kutokana na kupotea kwa umeme mara kwa mara.
Katika uchaguzi wa 2016, Mahama alikabiliwa na mashambulizi kutoka kwa upinzani, lakini alikiri kuwa ufisadi ulikuwa tatizo kubwa. Hata hivyo, ingawa alishinda kesi ya ufisadi dhidi yake, sifa zake za kisiasa zilidhihirika kwa namna tofauti.
Kuna masuala ya ufisadi ambayo bado raia wa Ghana hawajasahau,Bwana Cudjoe anasema.
Pia aligusia kuwa kulingana na ripoti ya Mtazamo wa Ufisadi ya Transparency International (CPI), ufisadi ulizidi kuwa mbaya chini ya Nana Akufo-Addo, ambaye alimshinda Mahama katika uchaguzi wa 2016.
Ghana ilikuwa na wastani wa 45.8 chini ya Mahama lakini ilishuka hadi 42 chini ya Akufo-Addo katika orodha ya CPI ambapo sifuri ni sawa na “fisadi wa hali ya juu” na 100 ni “mambo yana nafuu”.
Mahama alijaribu kuwania urais kwa mara nyingine mwaka 2020, lakini akabwagwa na Akufo-Addo kwa mara nyingine tena.
Licha ya kushindwa huku, Mahama amebakia katika nyanja ya kisiasa kwa sasa ni kiongozi wa upinzani.
Pia Mahama anafurahia Maisha kando na siasa- amebarikiwa kuwa na watoto saba na hutumia muda mwingi kufurahia na mkewe Lordina.
Mahama pia ni mwandishi mahiri. Kando na kitabu cha kumbukumbu ya maisha , ameandika kwa vyombo vya habari kama vile The New York Times, jarida linaloongoza kwa Waamerika wenye asili ya Afrika Ebony na gazeti la serikali la Ghana la Daily Graphic.
Mahama pia ameelezea mapenzi yake kwa muziki, akisema mwanamuziki wa Nigeria wa Afrobeat Fela Kuti alimsaidia kuunda “ufahamu wa kisiasa” na kwamba Michael Jackson ni “mmoja wa wasanii wakubwa waliowahi kuishi”.
Kwa kawaida, Mahama ametumia kipigo hicho katika kampeni yake ya sasa, akieleza kuwa chini ya Akufo-Addo, Ghana imetumbukia katika mgogoro mbaya zaidi wa kiuchumi kuwahi kutokea kwa miaka mingi.
Pia amekuwa akiwakumbusha Waghana kuhusu uzoefu wake mkubwa wa kisiasa lakini ukweli unabakia kuwa – alipigiwa kura ya kuondolewa madarakani hapo awali kwani umma ulihisi utendaji wake haukuwa mzuri wa kutosha.
Mahama anatafuta kuwashawishi wapiga kura wakati huu itakuwa tofauti – hali ya mawasiliano inayotumai ujumbe wake uko wazi kiasi cha kumfanya apate nafasi ya pili katika afisi kuu ya Ghana.