Sanamu la aliyekuwa mkuu wa Wagner lazinduliwa Afrika ya Kati
Sanamu la ukumbusho la marehemu kiongozi wa kundi la mamluki la Wagner wa Urusi, Yevgeny Prigozhin, limezinduliwa nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR).
Sanamu la Prigozhin na msaidizi wake Dmitru Utkin, ambao wote walifariki katika ajali ya ndege mwaka jana, yamewekwa katika mji mkuu wa Bangui.
Wapiganaji wa Kundi la Wagner wamekuwa CAR tangu 2018, walipoalikwa na Rais Faustin-Archange Touadéra kusaidia kukabiliana na vikundi vya waasi.
Makampuni tanzu ya kikundi hicho yalipata kandarasi za kuendesha migodi ya dhahabu na almasi. Pia Wagner wanafanya kazi katika nchi nyingine kadhaa za Afrika.
Prigozhin na Utkin walikufa pamoja na wengine, tarehe 23 Agosti 2023, baada ya ndege yao ya kibinafsi kudondoka kaskazini-magharibi mwa Moscow, na kuwaua wote waliokuwa ndani.
Ilikuwa ni miezi miwili tu baada ya uasi wa kundi hilo huko Urusi. Kremlin ilikanusha uvumi kuwa ndio ilihusika na ajali hiyo.